Hatua muhimu katika kutafsiri
Tunapofanya tafsiri kuna hatua muhimu kuu sita kwa mujibu wa Mwansoko na
wenzake (2006). Hatua hizo ni kama ifuatavyo:
1. Hatua ya maandalizi. Hatua
hii inahusisha mambo matatu ambayo ni:
a) Kupitia tena sehemu muhimu za
matini chanzi, kwa mfano; istilahi, majina ya wahusika, majina ya kijiografia,
maeneo au kauli zisizofasirika kirahisi.
b) Kupata marejeleo ili kutafuta
visawe vya kisemantiki
c) Kutafuta na kuandika visawe
hivyo.
2. Hatua ya pili baada ya
maandalizi ni uhawilishaji (transferring/transference). Katika hatua hii
mfasiri uhawilisha ile taarifa kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye matini
lengwa, hapa mfasiri anatakiwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa na lugha
chanzi. mfano; “My new car is broken”-langu jipya gari ni vunjika. Tafsiri ya
Kiswahili sanifu inapaswa kuwa “Gari langu jipya limeharibika”
Uhawilishaji maana yake ni kuhamisha maana, ujumbe nk. kutoka lugha
chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa, lengo la
matini au mwandishi, umbo la matini, mtindo nk.
Mbinu ya tafsiri ambayo inatumika katika hatua hii ya uhawilishaji ni
tafsiri ya neno kwa neno.
3. Hatua ya tatu ni kusawidi
rasimu ya kwanza (drafting). Uhawilishaji wa visawe kutoka lugha chanzi kwenda
lugha lengwa unapokamilika kinachopatikana ni rasimu ya kwanza ya tafsiri.
Rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo haifai
kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima ipitiwe
tena upya na kurekebishwa au kudurusiwa/durusu (review) rasimu (draft).
4. Hatua ya nne ni kudurusu
rasimu ya kwanza ili kuunda rasimu ya pili. Mfasiri hupata fursa ya kwanza ya
kuitathimini na kuifanyia marekebisho tafsiri yake mwenyewe. Kazi ya kudurusu
haipaswi kufanywa haraka. Wataalam wengine kama vile Larson (1984) anasema
rasimu ya kwanza ni lazima iachwe kwa muda wa wiki moja.
Udurusu unahusisha shughuli zifuatazo:
·Kusahihisha makosa ya kisarufi, miundo isiyoeleweka vizuri.
·kunyoosha sehemu zenye tafsiri ya mzunguko na zenye matumizi potofu ya
visawe. Mfano; “He rarely visits me these days – Siku hizi ni aghalabu-nadra
sana yeye kunitembelea.”
·Kurekebisha sehemu zenye muunganiko tenge/mbaya ambazo zinazuia
mtiririko mzuri wa matini.
·Kuhakiki usahihi na kukubalika kwa maana zinazowasilishwa katika matini
lengwa. Hapa tunaangalia kama kuna mambo yameongezwa, yamepunguzwa au
yamepotoshwa/kubadilishwa.
·Kuhakiki kukubalika kwa lugha uliyotumia katika tafsiri yako kwa
kuzingatia umbo na mada ya matini chanzi.
·Kuona iwapo mada au ujumbe mkuu wa matini chanzi unajitokeza waziwazi
katika matini lengwa.
5. Hatua ya tano ni kusomwa
rasimu ya pili na mtu mwingine. Msomaji wa rasimu ya pili anaweza kuwa mfasiri
au shabiki wa tafsiri, mhakiki au mhariri wa tafsiri anaweza kuwa mteja wa
tafsiri husika au mtu mwingine yeyote unayemwamini.
Namna ya kumpa mtu akusomee rasimu:
·Kumpa bila kumjulisha kwamba ni tafsiri
·Unampa matini chanzi na matini lengwa ili alinganishe.
Inapendekezwa kwamba mtu huyo asome kwa
sauti ili uweze kubaini mapungufu.
6. Hatua ya sita ni kusawidi
rasimu ya mwisho. Katika hatua hii mfasiri atafanyiakazi maoni na mapendekezo
ya msomaji ambaye alimpa kazi yake. Matokeo ya kufanyiakazi maoni ya mteja
hutupelekea kupata rasimu ya mwisho ambayo ndiyo humfikia mteja, hadhira,
wachapaji nk.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com