Swali hili litajibiwa kwa kuanza na fasili
mbalimbali za ushairi kama wanavyozifasili
wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo:
Mnyampala, (1970). Anasema kuwa, ushairi ni msingi
wa maneno ya hekima tangu kale ndicho kitu kilicho bora sana maongozo ya dunia kwa
kutumia maneno ya mkato na lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari wa
mizani na vina maalumu.
Mulukozi na Kahigi, (1982). Wanaeleza kuwa ushairi
ni sanaa inayopambanuliwa kwa mpangilio maalumu na fasaha na wenye muwala, kwa
lugha ya picha, sitiari au ishara katika usemi, maanadishi au mahadhi ya wimbo
ili kuleta wazo au mawazo, kufunza ua kueleza tukio au hisia fulani kuhusu
maisha au mazingira ya binadamu kwa njia inayogusa moyo.
wazo kwa njia ya mkato, na kwa namna inayoteka hisia
za msomaji au msikilizaji. Maneno ya mshairi huteuliwa kimakusudi (ili yalete
taswira maalumu akilini mwamsomaji au msikilizaji).
BAKITA (2015) wanasema kuwa ushairi ni utanzu wa
fasihi unaojihusisha na utungaji wa mashairi, tenzi, ngojera na nyimbo.
Hivyo basi, kutokana na fasili zilizotolewa na
wataalamu maana ya jumla ya ushairi ni kazi ya sanaa yenye kuandikwa au kuimbwa
kwa kufuata kanuni za ushairi au kutofuata kanuni za ushairi ikiwa na maana
kuwa ushairi waweza kuwa wa kimapokeo au wa kisasa ilimradi ushairi huo uwe na
ujumbe.
Kwa mujibu wa Senkoro, (1988) ushairi wa Kiswahili
ni ule ushairi uliotungwa kwa lugha ya Kiswahili, na ambao unawahusu watu
watumiao lugha ya Kiswahili maishani mwao. Aidha, Njogu na Chimerah (2008)
wanaendelea kueleza kuhusu chanzo na asili ya
ushairi wa Kiswahili kuwa ni nyimbo zilizoimbwa katika magoma ya harusi,
pungwa, sherehe za jando na unyago, kufanya kazi hasa pale kazi ilipohitaji
ushirikiano. Awali nyimbo hizi hazikuwa na vina wala mizani bali zilifuata
mdundo (ridhimu) wa ufanyaji kazi au muktadha mpana wa uimbaji. Pia, chimbuko
la Kiswahili lilianza mnamo karne ya kumi kwani kipindi hicho ushairi wa
Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandika.
Ni kweli kuwa ushairi wa Kiswahili umeathiriwa na
Waarabu na Uaislamu, rai hii imedhihirishwa kama ifuatavyo;
Ushairi wa Kiswahili kutumia maneno na hati za
kiarabu. Kwa mujibu wa Senkoro (1988) anaeleza kuwa ujio wa waarabu ulileta
athari kadhaa katika ushairi wa Kiswahili. Waaarabu walipokuja katika upwa wa
Afrika Mashariki walianza kuandika mashairi yako kwa kutumia hati za Kiarabu.
Hapa ndipo tunapoanza kupata ushairi andishi wa Kiswahili. Waarabu waliwafunza
Waswahili kusoma na kuandika kwa kutumia hati za kiarabu. Waswahili nao walinza
kuhifadhi mambo yao katika maneno hayo maandishi kwa kutumia hati hii ya
Kiarabu.
Pia, msamiati wa kiarabu na uislamu umeathiri
ushairi wa Kiswahili. Maneno mengi ya kiarabu yamo katika ushairi wa Kiswahili.
Mulokozi na Sengo (1995) wanataja istilahi kadhaa zilizotokana na ujio wa
waarabu ambazo ni shairi, mizani, ubeti, tathilitha, tarbia na takhmisa. Kutokana
na istilahi hizi zinazotolewa na Mulokozi na Sengo ni wazi kuwa ushairi wa
Kiswahili umeathiriwa na Waarabu na Uislamu.
Vilevile suala la maudhui limeathiri ushairi wa
Kiswahili. Mulokozi na Sengo (1995) wakimnukuu Lyndon Harries wanaeleza kuwa
maudhui yaliyopatikana katika ushairi wa Kiswahili yalitokana kwa kiasi kikubwa
na ushairi wa Kiarabu, kutokana na dini ya kiislamu maudhui ya mashairi
yalisawili dini hiyo. Mfano maudhui ya ushairi wa Kiswahili yaliyotokana na
ushairi wa Kiarabu ni yale ya kutoka katika tungo za ushairi andishi wa
Kiswahili kama vile Tambuka na Mwengo bin Athman (1728). Kwa maelezo ya
wataalamu hawa inaonesha kuwa maudhui katika ushairi wa Kiswahili yalitokana na
dini ya Uislamu.
Aidha, mianzo ya mashairi ya kiarabu imeathiri
ushairi wa Kiswahili, Harries (1962). Anaeleza kuwa mianzo mingi ya Kiswahili
ilikuwa na aya mbalimbali za Qur’an. Vilevile kutokana na hilo hata aya za
Qur’an Tukufu na dua za Kiislamu zikaanza kuingizwa katika ushairi wa
Kiswahili. Sio hivyo tu, bali pia hata muundo wa mashairi ya Kiarabu ukaanza
kutumika katika mashairi ya Kiswahili. Mfano mzuri ni shairi la “Haki za
Binadamu” kutoka katika diwani ya Mutua (2006) anaeleza:
“Kwa jina
lake Jalia, muumba wa nchi na mbingu
Aloumba
nisia, na wengi viumbe chungu
Rabi Mola
metimia, kwake hakuna tewengu”.
Hivyo basi mianzo ya maneno katika shairi hili
linadhihirisha ushairi wa Kiswahili ulivyoathiriwa na waarabu na Waislamu.
Lakini pia, ushairi wa Kiswahili kuibuliwa na
wafuasi wa Waarabu unadhihirisha athari katika ushairi wa Kiswahili, Kwa mujibu
wa Samwel na wenzake (2013) wanaeleza kuwa ushairi wa Kiswahili uliibuliwa na
kuenezwa na wafuasi wa waarabu. Washairi wengi wa mwanzo wa ushairi wa
Kiswahili walikuwa na mahusiano ya karibu na waarabu, mahusiano hayo yanaweza
kutokana na unasaba au mambo mengine ya kijamii kama vile dini na ndoa.
Inadaiwa kuwa washairi wengi wa mwanzo wa ushairi wa Kiswahili kama si kuwa na
damu ya Kiarabu, kuzaliwa kutokana na ndoa ya mwarabu na mswahili, walikuwa
wafuasi wa dini ya Kiislamu. Washairi hao ambao ni Waislamu na wanamajina ya
Kiarabu ni kama vile Shabaan Robert, Amri Abed, Sayyid Abdallah bin Ali,
Mohamadi Kijumwa na wengineo ni waislamu na wafuasi wa Waarabu.
Pamoja na hoja zilizotolewa na wataalamu juu ya
ushairi wa Kiswahili kuathiriwa na Waarabu na Uislamu, hoja hizi zina udhaifu
kwani ifahamike kwamba wapo washairi wengine Wakristo waliokuwapo karibu
kipindi sawa na kuwapo kwa washairi wa Kiislamu, miongoni mwa washairi hao ni
Mathius Mnyampala, pia si kweli ushairi ulikuwa unazungumzia Uislamu lakini wao
wenyeji walikuwa na ushairi ulikuwa unazungumzia maisha yao ambayo yalikuwepo
kabla ya ujio wa Uislamu. Vilevile suala la maneno mengi kuwa ya Kiarabu
halitoshi kwani lugha kukopa maneno kutoka lugha nyingine ni suala la kawaida
kabisa.
Kwa ujumla ushairi wa Kiswahili umeathiriwa na Waarabu
na Uislamu lakini kuna baadhi ya wanazuoni wanaothibitisha kuwa ushairi wa
Kiswahili ulikuwepo hata kabla ya ujio wa Waarabu na Uislamu karne ya 10 BK
ushair wa Kiswahili ulikuwa ukitungwa na kughanwa kwa ghibu bila kuandikwa na
asili ya ushairi wa Kiswahili ni tungo simulizi hasa ngoma na nyimbo.
MAREJELEO
BAKITA
(2015). Kamusi Kuu ya Kiswahili, Longhorn
Publisher Limited. Nairobi, Kenya.
Chimerah,
R na Njogu, K. (2008). Ufundishaji wa
Fasihi Nadharia na Mbinu. Jommo Kenyatta:
Nairobi.
Harries,
L. (1962). Swahili Poetry. Oxford
University Press, London.
Mnyampala,
M. (1970). Diwani ya Mnyampala. Dar
es Salaam Kampala/Nairobi: East African
Literature Bureua
Mulokozi,
M. M. na Kahigi, K. K. (1982). Fasihi ya
Kiswahili. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Dar es Salaam.
Mulokozi,
M. M na Sengo, T. S. Y. (1995). History
of Kiswahili Poetry A.D 1000 – 2000,
Institute of Kiswahili Research. Dar es Salaam.
Mutua,
B. E. (2006). Kioo cha Ushairi,
Taaluma Publishers: Eldoret.
Samwel,
M, Seleman, A.J. na Kibiero, A. J. (2013). Ushairi
wa Kiswahili, Nadharia,
Maendeleo, Mwongozo
kwa Walimu wa Kiswahili na Diwani ya Mea. Meveli
Publishers (MVP). Dar
es Salaam.
Senkoro,
F. E. M. K. (1988). Ushairi-Nadharia na
Tahakiki. Dar es Salaam University Press.
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com