Flower
Flower

Tuesday, July 7, 2020

Mofolojia

Katika kujibu swali hili tumeligawa katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo istilahi zilizojitokeza katika swali zitafasiliwa kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, sehemu ya pili ni kiini cha swali na sehemu ya tatu ni hitimisho la swali.
Mgullu (1999) akimnukuu Hartiman na Mathew (1972), Richard (1985) na Mathew (1978) wanaeleza kuwa mofolojia ni taaluma ya isimu ambayo huchunguza maumbo ya maneno na hususa ni maumbo ya mofimu.
Massamba (2009) anaeleza kuwa mofolojia ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchambuzi na uchanganuzi wa kanuni na mifumi inayohusu upangaji wa mofimu mbalimbali ili kuunda maneno katika lugha.
Besha (2007) anafasili dhana ya mofolojia kuwa ni taaluma inayojishughulisha nakuchambua maumbo ya maneno katika lugha.
Habwe na Karanja (2012) wanaeleza kuwa dhana ya mofolojia ni tafsiri ya neno la kiingereza “Mophology”. Neno hilo limetokana na neno la Kiyunani “Morphe” lenye maana ya maumbo au umbo. Hivyo walifasili dhana ya mofolojia kuwa ni neno linalotumiwa kumaanisha utanzu wa isimu unaoshughulikia maumbo kwa ujumla.
Kwa ujumla dhana ya mofolojia ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo mbalimbali ya maneno katika lugha na kipashio chake cha msingi ni mofu, ambapo mofu ni kiapshio cha kimofolojia kinachowakilisha mofimu.
Mgullu (2010) amefasili dhana ya uainishaji wa lugha kuwa ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uainishaji wa lugha kwa misingi mbalimbali. Pia alibainisha misingi mitatu ya uainishaji wa lugha, ambayo ni msingi wa kimuundo/ sintaksia unaochunguza mpangilio wa vipashio katika sentensi. Mfano katika lugha ya Kiswahili sentensi huanza na kiima, kiarifu na yambwa (K+A+Y), msingi wa kiuamilifu ambao hubainisha lugha kwa kuchunguza matumizi au kazi ya lugha fulani katika jamii. Ambapo kwa kutumia msingi huu tunapata lugha rasmi na lugha kienzo (isiyo rasmi) na msingi wa tatu ni msingi wa kimaumbo/ kimofolojia ambao hubainisha lugha kwa kuchunguza mapangilio wa mofu katika maneno ya lugha fulani. Kulingana na swali hili tutajikita katika msingi wa uainishaji lugha kimaumbo/ kimofolojia, ambao huchunguza mpangilio wa mofu katika maneno. Aidha Mgullu (keshatajwa) anasema kuwa uainishaji wa lugha kwa kutumia msingi wa kimofolojia, umeainisha lugha kwa kuzingatia maumbo ya lugha mbalimbali za jamii na uainishaji huu unatupatia aina tano za lugha ambazo ni lugha tenganishi, lugha ambishi, lugha ambishi mchanganyiko, lugha ambishi bainishi na lugha muundo ghubi.
Mathew (1991) anaeleza kuwa lugha tenganishi ni ile ambayo maumbo ya maneno yake huonekana kama mofu moja moja tu. Anaendelea kueleza kuwa mfano wa lugha hizo ni Kituruki, Kichina na Kiingereza. Mathalani katika lugha ya Kiingereza maneno kama “with, what na Rice” ni mfano wa lugha tenganishi kwa sababu maneno hayo hayawezi kuongezwa viambishi vya aina yoyote. Pia Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha tenganishi ni aina ya lugha ambazo maumbo yake hayaambishwi, hayanyambuliwi, hayabadiliki na hayana viambishi vyovyote. Hii inamaanisha kuwa maana za tungo hudhihirika na kutofautishwa kwa kutumia mpangilio wa maneno ambapo maneno katika lugha za jamii huwa na mofu moja tu ambayo huwakilisha mofimu moja. Kutokana na maana hii tunaona kuwa mfano wa lugha ya Kiingereza uliyotolewa na Mathew (keshatajwa) una udhaifu kwa sababu kuna baadhi maneno ya Kiingereza ambayo huweza kunyambulika kwa kuongezewa viambishi mbalimbali. Mfano “do – done”. Hivyo lugha tenganishi ni lugha ambayo maneno yake huundwa kwa mofu moja huru ambayo huwa na maana kamili. Mfano wa lugha hizi ni Kichina na Kivietinamu.
Massamba (2004) anaeleza kuwa lugha ambishi ni lugha ambayo maneno yake hutumia viambishi kuwakilisha dhana mbalimbali. Naye Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha ambishi ni lugha ambazo maneno yake huambika viambishi mbalimbali ambavyo huwakilisha maana mbalimbali za kisarufi na lugha hizi hupokea viambishi katika mashina yake au katika mizizi yake. Mfano wa lugha hizi ni Kiitaliano, Kiingereza na Kiswahili. Mathalani katika lugha ya Kiingereza mofu “S” inaweza kuwekwa kwenye maneno mbalimbali na kuwa na dhima tofauti tofauti kama ifuatavyo;-
Play                           palys (njeo)
           Sara                           Sara’s (umilikishi)
Eye                            eyes (wingi)
Katika mifano hii mofu “S” imedokeza dhima mbalimbali. Vilevile lugha ya Kiswahili huruhusu uambikwaji wa viambishi mbalimbali katika maneno ambavyo hudokeza dhima mbalimbali. Mfano mashina kama vile “piga, cheza na soma” ikiongezewa viambishi inaweza kuwa kama ifuatavyo;-
Piga       -     pigia, pigisha, alipigwa, pigana na pigishwa
Cheza    -     chezea, chezesha, alichezwa, chezeana na chezeshwa
Soma     -     somea, somesha, alisomeshwa, someshana na someka
Kutokana na mifano hiyo inaonesha kuwa baada ya kuambika viambishi kwenye mashina yamedokeza dhima ya kauli mbalimbali ikiwemo kauli ya kutenda, kutendwa, kutendeka, ktendea, kutendeana na kutendewa.
Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha ambishi mchanganyiko ni lugha ambazo huambikwa mofu mbalimbali katika mizizi ama mashina kisha mofu hizo huchanganyika na mizizi kiasi ambacho ni vigumu kutenganisha Dhahiri kuwa mofu ni zipi na mizizi ni ipi, kwani mofu na mizizi huungana na kuwa kitu kimoja. Kuunganika kwa mofu na mizizi huweza kubainishwa na michakato ya kimofofonolojia, ambapo Rubanza (1996) anaeleza kuwa mofofonolojia ni kanuni ambazo huelezea mazingira ambapo mofu hutokea. Mathalani kanuni hizo ni udondoshaji, uyeyushaji, ukakaishaji na usilimisho pamwe wa nazali. Mfano wa lugha hizi ni Kiingereza na Kilatini. Katika lugha ya Kiingereza, maneno yenye umoja na wingi huweza kubadilika lakini nivigumu kutenga mofu na mizizi husika. Mifano ifuatayo inadhihirisha dai hili;-
Umoja                                 Wingi
                                                   Man                                     Men
   Woman                                 Women
                                                    Foot                                      Feet
  Mice                                    Mouse
Hivyo katika mifano hiyo, licha ya maneno yaliyokatika umoja kubadilika katika wingi bado ni vigumu kutenga mofu na mzizi wa neno husika.
Massamba (2004) anafasili lugha ambishi bainishi ni lugha ambayo maneno yake huundwa kwa mwandamo wa mofimu katika safu moja kuandamia mzizi, ambazo zinatenganishika kwa utaratibu ulio wazi na kila moja huwa na uamilifu mmoja tu. Pia Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha ambishi bainishi ni lugha ambazo maneno yake huweza kuwekewa viambishi mbalimbali, yaani mizizi na viambishi huwa havichanganyiki kwani ni rahisi kabisa kuweza kuonesha kuwa viambishi ni vipi na mizizi ya maneno ni ipi. Mfano wa lugha hizi ni Kiswahili. Mifano ifuatayo inadhihirisha dai hili;-
Analima                           a- na- lim- a
Atapika                             a- ta- pik- a
    Alipikiwa                          a- li- pik- iw- a
Hivyo kutokana na mifano hiyo, mizizi na viambishi vya maneno vimejidhihirisha wazi.
Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha muundo ghubi ni lugha ambayo huundwa kwa kuweka pamoja mfululizo wa mofu au wa maneno katika lugha moja. Na maneno ya lugha hii huwa na uchangamani zaidi kwani mzizi huunganishwa ili kujenga neno moja lenye muundo changamani. Mfano wa lugha hizi ni lugha ya Kieskimo.
Licha ya mofolojia kuwa na dhima yya kuainisha lugha, pia huweza kuwa na dhima nyingine kama zilivyofafanuliwa na Mathew (1991),
Mofolojia husaidia kubainisha vipashio vinavyounda maneno na dhima zake. Mfano neno Anacheza hujibainisha na kuwa (a- na- chez- a) ambapo mofu a- kiambishi awali cha nafsi ya tatu umoja, -na- kiambishi cha wakati uliopo, -chez- ni mzizi wa neno na –a ni kiambishi tamati maana.
Mofolojia husaidia kuunda maneno mbalimbali. Mfano neno piga likiongezwa viambishi huweza kuunda maneno mengine mapya kama ifuatavyo, anapiga, atapigwa, wanapigana, pigika na pigia.
Kwa ujumla licha ya uainishaji lugha kwa kutumia msingi wa kimofolojia lakini pia kuna misingi mingine ambayo ina mchango mkubwa sana katika suala zima la uainishaji wa lugha. Misingi hiyo ni pamoja na msingi wa kiuamilifu na msingi wa kimuundo/ kisintaksia.


MAREJELEO
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es salaam: Macmillan Aidan Ltd.
Habwe, J. na Karanja, P. (2012). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Massamba, P. B. (2004). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA). Sekondari na Vyuo.  Dar es salaam: TUKI.
……………….. (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es salaam: TUKI.
Mathew, P. H. (1991). Mophology (Second Edition). United Kingdom. Cambridge University Press.
Mgullu, R. S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Kenya Ltd.
Rubanza, Y. I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.







No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny