Ni
kweli kwamba dhana ya Falsafa hutoshelezwa na matawi yake kwa namna mbalimbali.
Wataalamu wametoa maana mbalimbali za Falsafa ambazo kwa namna moja au nyingine
zinatosheleza matawi yake. Kiontomolojia neno Falsafa limetokana na maneno
mawili ya kigiriki Philo lenye maana Kupenda na Sophia lenye maana Hekima.
Hivyo zifuatazo ni fasili mbalimbali kuhusu dhana ya falsafa kwa mujibu wa
wataalamu mbalimbali.
Kwa
mujibu wa Sadipo (1973) anafasili Falsafa ni mawazo, fikra na udadisi kuhusu
dhana na kanuni zinazotusaidia kuongeza uzoefu kuhusu maadili, dini, maisha ya
kisiasa, sheria, saikolojia, historia na sayansi ya jamii. Tunaona kuwa Fasili
hii ina mapungufu kwa sababu inachukulia Falsafa kama kanuni zinazotusaidia
kuongeza uzoefu lakini sio kanuni zote katika maisha humuongezea mtu uzoefu
kuhusu maadili na vitu vingine kwa sababu kuna baadhi ya kanuni humnyima uhuru
mwanadamu na kumgandamiza.
Pia
Ankipelu (1981) amefafanua maana ya falsafa katika mitazamo miwili ambayo ni
Falsafa kama mtazamo na Falsafa kama taaluma. Katika Falsafa kama mtazamo
anafafanua kuwa Falsafa ni mtazamo na muono wa mtu binafsi juu ya maisha. Hii
hufanya mtu awe na dhana fulani, imani, na fikra fulani juu ya kitu. Anaendelea
kusema kila mtu anakitu anachokiona kuwa ni kizuri au kibaya na anachokipenda au asichokipenda ingawa hali hiyo hutegemea
makuzi ya mtu huyu. Fasili hii inataka kutuaminisha kuwa Falsafa ni suala la
mtu binafsi tu hivyo ikiwa kuna miono au mitazamo itakayotolewa na kikundi cha
watu wenye imani moja basi haitakuwa Falsafa kitu ambacho si sahihi.
Pia
Akinpelu anaendelea kufasili dhana ya Falasafa kama taaluma kwa kusema ni
mafunzo au nidhamu ya kitaaluma ambayo wanazuoni huwekeza maarifa, muda na
nguvu zao. Hufunuliwa na kueleweka kwa kufuata utaratibu fulani wa mawazo yenye
maana na mawazo huwepo kujaribu maswali mbalimbali yahusuyo binadamu. Ni kweli
kuwa Falsafa huweza kuwa ni mafunzo kwa kuwa pengine hutolewa kwa mafunzo
fulani maalumu lakini yeye anajikita katika mafunzo na hajaweka wazi kuwa nini
kinatokea baada ya hayo mafunzo ambayo yeye anayaita kuwa ni Falsafa na hayo
mafunzo yanakuwa yanahusu nini hasa.
Alexander
Nehemas (1985) anafasili Falsafa kuwa ni uwezo na maarifa aliyonayo mtu yanayohusu
kujua mambo mengi tofautitofauti. Mambo hayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya.
Nehemas anazungumzia uzuri na ubaya,yaani ukiwa na uwezo wa kuyafahamu mambo
haya basi wewe ni Mwanafalsafa lakini sio kweli kwamba ukiweza kujua mema na
mabaya tu basi inatosha kuwa Mwanafalsafa kwa sababu muda mwingine kuna wakati
mwanadamu anapaswa kutatua matatizo mbalimbali na sio tu kuyajua kama anavyodai
Nehemas.
Thomas
Pogge (1989) anaeleza Falsafa ni mtazamo wa ndani wa upendo wa hekima na
maarifa. Hekima ni uwezo wa kuuelewa ulimwengu na yaliyomo na yanayotokea, hiyo
ndio Falsafa. Yeye anasisitiza kuhusu maarifa lakini kuwepo na upendo. Swali ni
je, upendo ni nini? Au tunawezaje kujua kuwa huu ni upendo na huu sio upendo?.
Fasili hii inaibua maswali kadhaa ambayo yanaleta mkanganyiko mwingine kwa
sababu hakuna ishara yoyote ambayo itatuambia sasa haya ni maarifa ya upendo
hivyo iwepo Falsafa na haya sio maarifa yenye upendo kwa hivyo sio Falsafa. Kwa
maana hiyo suala la msingi hapa liwe ni uwepo wa maarifa na hekima pekee sio
lazima yawe ya namna fulani.
Odera
(1990) anasema Falsafa ni taaluma ambayo kanuni za msingi kuhusu asili,
binadamu na jamii huchunguzwa na kujadiliwa.Odera anazungumzia taaluma ambayo
mtu anapaswa kuwa nayo ili kuchunguza jambo fulani na kanuni zake bila kuzitaja
hizo kanuni ni zipi hasa ambazo kimsingi inawezekana kuwa hizo kanuni zenyewe
ndizo Falsafa. Kwa maana hiyo, hizo kanuni zinapaswa kuwa ndizo Falsafa yenyewe
kwa kuwa ndiyo inayomwongoza binadamu kuishi.
David
Papineau (1993) anaeleza Falsafa ni fikra za ndani kabisa kuhusu maswali magumu
ambayo yapo. Mara nyingine unaweza ukadhani kama wanasayansi wanaweza kuyajibu
kwa ushahidi lakini hata ushahidi huo ukakosa ushahidi wa uwepo wake. Hivyo
tunaona kuwa suala la msisitizo katika fasili hii ni fikra za ndani kwa mujibu
wa Papineau akimaanisha kuwa hizi ni fikra tu na ikiwa ni fikra tu za ndani
basi ni vigumu kujua kama huyu mtu anawaza kuhusu jambo fulani. Kwa maneno
mengine ni kuwa, maswali hayawezi kupata majibu kwa kuwa majibu yamebaki kuwa
fikra tu za mtu binafsi ambazo watu wengine hawawezi kuziona. Labda hoja ya
msingi ibaki kuwa fikra lakini fikra hizo ziwasilishwe na muhusika kwa ajili ya
kupata majibu ya maswali mbalimbali.
Simon
Blackburn (1994) anafafanua Falsafa kuwa ni mchakato wa kutengeneza mawazo
yaliyo katika utaratibu maalumu yanayotoa tafakuri juu ya ulimwengu, kile
kinachofanya uwe vile tunavyoona. Hujaribu kutazama sababu, muda, hiyari, anga
na mengine mengi. Mwanafalsafa huyu anaeleza kuwa ni mawazo yaliyo katika
utaratibu malumu kitu ambacho ni sahihi lakini hajafafanua zaidi kuwa nini
kifanyike baada ya kuzifahamu sababu hizo na kuna kweli gani kuhusu sababu
hizo. Kwa hiyo ingekuwa vyema zaidi kama mawazo na sababu hizo ambazo
zimepatikana kama anavyosema Blackburn zingepimwa kama kuna ukweli wa sababu
hizo ndipo mawazo hayo yawe Falsafa ikiwa hicho hasa ndicho alicholenga
kukisema.
Paul
Snowdon (2014) anafasili dhana ya Falsafa kuwa ni jumla ya majibu yote
yanayotolewa juu ya maswali mbalimbali yanayohoji uhalisia wa ulimwengu na
maarifa yake kwa kutafuta ushahidi. Snowdon anajikita zaidi katika majibu kitu
ambacho ni sahihi kwamba majibu ndiyo yanayofanya watu wafahamu vitu mbalimba.
Pamoja na hayo, mwandishi huyu hakutazama upande mwingine wa sarafu kuwa
hakuchunguza hata ni nini kimetumika kuleta majibu hayo. Vilevile sio majibu
pekee ndiyo yanahitajika katika ulimwengu, muda mwingine hata mafunzo tu
yanahitajika juu ya ulimwengu. Hivyo alipaswa kujua kuwa hata majibu hayo
yalitumia mawazo na maarifa fulani kupatikana ambayo nayo yanaweza kuwa
Falsafa.
Hivyo
kutokana na fasili za wataalam mbalimbali kwa mawazo yetu tunaona kuwa Falsafa
ni Maarifa, miongozo yenye hekima na mawazo ambayo jamii au mtu huamini kuwa ni
kweli na kufanya kuwa moja ya misingi katika maisha yake. Vilevile kupitia
maarifa hayo ndipo tunaweza kupata utatuzi wa maswali na changamoto mbalimbali
zinazohusu jamii na ulimwengu kwa ujumla. Changamoto hizi zinaweza kuwa ni za
kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni.
Baada
ya kuangalia fasili za wataalamu mbalimbali kuhusu Falsafa pamoja na mtazamo
wetu, yafuatayo ni matawi ya Falsafa na jinsi yanavyotosheleza dhana za Falsafa
za wataalamu mbalimbali.
Metafizikia.
Kwa
mujibu wa Akinpelu (1981) anasema neno metafizikia linatokana na maneno mawili
yani “meta” lenye maana baada na “Fizikia” lenye maana Ulimwengu. Haya
yalisemwa na Andronicus ambaye alikuwa anafuata mafundisho ya Aristotle kuhusu
mipaka ya ulimwengu. Pia Joseph Omoregbe (1999) anaweka wazi kuwa Metafizikia
hutazama nanma ulimwengu ulivyo na matatizo yake na namna ya kuyatatua na
ukweli wa mambo kuhusu ulimwengu. Hivyo tunaona kuwa tawi la metafizikia
lenyewe likiunga mkono fasili iliyotolewa na Bluckburn (ametajwa) ambapo
huchunguza namna ulimwengu ulivyo pamoja na mipaka yake. Anaelezea mambo yanayohusu
juu ya kuwapo kwa ulimwengu na kile kinachofanya uwe vile tunavyouona
ulimwengu, kwa hiyo tunaona fasili ya bluckburn imetoshelezwa na tawi la metafizikia.
Mantiki.
Kwa
mujibu wa Luke Mastin (2008) anasema hii ni taaluma inayohusu fikra. Taaluma hii
huwa na miundo ya fikra juu ya dhana mbalimbali, na huweza kuchunguza kanuni au
hoja zilizo sahihi na zisizo sahihi.Hufafanua fikra hizo kwa kufuata utaratibu
fulani wa mawazo yenye maana na mawazo hayo huwepo kujaribu kujibu maswali
mbalimbali yahusuyo binadamu. Hivyo tunaona tawi hili linatosheleza dhana ya
falsafa ya Akinpelu anaesema Falsafa humfanya mtu awe na dhana fulani, imani na
fikra fulani juu ya kitu.
Maadili.
Mastin
(2008) anasema ni taaluma inayochunguza kuhusu lipi la kufanya na lipi si la
kufanya. Tawi hili linachunguza mwenendo wa mtu au jamii kimaadili. Huelekeza
ni namna gani watu wanapaswa kuishi, yapi ni maadili mema na yapi ni mabaya. Tawi
hili kwa ujumla huchunguza mwenendo wa mtu na jamii kimaadili. Tawi hili
linatosheleza fasili iliyotolewa hapo awali na Nehemas (ametajwa) alipoeleza
kuwa falsa ni taaluma yenye maarifa ya kumruhusu mtu kujua mambo mengi tofauti
tofauti ambapo mambo hayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya.
Ujumi.
Kwa
mujibu wa Baumgarten (1986) akimnukuu Leibniz anasema ni tawi la falsafa
linaloshughulika na dhana ya uzuri, ubaya na ukweli wa kitu fulani au mtu
fulani. Hupambanua juu ya hisia fulani katika ufahamu wa wanaadamu na usahihi
wake katika kutoa tafsiri hasa ya uzuri wa kitu. Hapa ana maana kuwa, kila mtu
anaweza kulichukulia jambo fulani katika mtazamo wake. Wapo watu wanaoweza
kulichukulia jambo fulani kimtazamo hasi hali ambayo haiwezi kuuondoa mtazamo
wa watu wengine wanaolichukulia jambo hilo katika mtazamo chanya. Tawi hili
linatosheleza fasili ya Akinpelu ( ameshatajwa) anasema kwamba falsa ni mtazamo
na muono wa mtu juu kitu fulani juu ya uzuri wa kitu fulani. Anaongeza kwa
kusema,kila mtu ana kitu anachokipenda na asichokipenda na hutegemea makuzi ya
mtu huyo.
Epistemolojia
Kwa
mujibu wa Harnad (2005) katika kitabu cha Stanford
Encyclopedia of Philosophy anasema
kuwa Epistemolojia ni taaluma inayohusu upatikanaji wa maarifa na kuyachunguza
maarifa hayo. Epistemolojia hujaribu kujibu baadhi ya maswali ambayo huhoji
chanzo na chimbuko la maarifa na ukweli wa maarifa hayo. Pia huchunguza mfumo
mzima wa maarifa na mipaka yake. Kwa mujibu wa maelezo haya tunaona wazi kuwa
fasili hii ya Epistemolojia inatosheleza fasili ya Falsafa ya Snowden
(ameshatajwa) kwamba Falsafa ni jumla ya majibu yote yanayotolewa juu ya
maswali mbalimbali yanayohoji uhalisia wa ulimwengu na maarifa yake kwa
kutafuta ushahidi wa mambo hayo.
Kwa
ujumla tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa Falsafa inahusika moja kwa moja na
maisha ya binadamu na ni wazi kuwa Falsafa haiwezi kutenganishwa na maisha ya
binadamu. Historia ya Falsafa inaenda sambamba na historia ya binadamu
ulimwenguni hata kabla wasomi na wanazuoni hawajagundua kuwa hiyo ndiyo Falsafa.
Hii ni sawa na kusema kuwa ili maisha ya binadamu yakamilike yanahitaji
misingi,maarifa na kanuni fulani katika maisha yake ambayo inaweza kutatua
changamoto mbalimbali za binadamu ambayo ndiyo Falsafa yenyewe.
MAREJELEO
Akinpelu, J. A.
(1981). Introduction to Phylosophy
Education. London: Madhullan Publisher
Ltd.
Baumgarten,
A. (1986). Sacrifice in Religious
Experience. Leiden: Brill Publisher.
Blackburn,
S. (1994). The Oxford Dictionary of
Philosophy. British: Oxford University Press.
Harnad
& Stevan. (2005). Encyclopedia of Philosophy. China: Macmillan
Mastin,
L. (2008). A Cultural Journey through the
English Lexicon. IGI Global
Nehemas,
A. (1985). Life as Literature. Havard
University Pre
Odera,
H. (1990). Trends in Contemporary African Philosophy. Nairobi: Shirikon Publishers
Omeregbe,
J. L. (1999). Metaphysics Without Tears.
Lagos: Research Publication.
Papineau,
D. (2009). Philosophy. Duean Barid
Publisher
Paul,
F. (2014). Persons, Animals, Ourselves.
Oxford University Press.
Pogge,
T. (1989). Realizing Rawls. New York.
Cornell University Press.
Sadipo.
(1973). Woman and African Society. France: Strabourg.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com