Ni
kweli kwamba tofauti ya mawazo baina ya mabingwa wa Ushairi wa Kiswahili kuhusu
maana ya ushairi ni msisitizo tu kutokana na
wataalamu mbalimbali wa ushairi kufasili maana za ushairi kwa utofauti.
Kwa
mujibu wa Wamitila (2010) anadai kuwa Ushairi ni utanzu ambao una historia
ndefu katika Fasihi ya Kiswahili ingawa mpaka leo hakuna makubaliano kuhusu
utungo wa kwanza uliandikwa lini. Wataaalamu wanakubaliana kuwa utanzu huu una
historia ndefu. Anaendelea kusema kuwa Ushairi wa Kiswahili umegawanyika katika
makundi makuu mawili amabayo ni mashairi ya kijadi au ya kimapokeo ambayo
hutungwa kwa kuzingatia arudhi au kaida za utunzi kama vina, mizani, idadi
maalumu ya mishororo katika ubeti na vipande. Pia Mashairi ya kisasa au huru
ambayo hukiuka kaida hizo na badala yake kutegemea mbinu nyingine za kishairi
kama uruwazi wa kimuundo kuwasilisha ujumbe wake.
Wataalamu
mbalimbali wa Ushairi wa Kiswahili hutofautiana katika maana zao za Ushairi.
Kwa kiasi kikubwa wataalamu hawa wamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni
wana Mapokeo na wana Usasa. Kwa kuanza na Wanamapokeo wanatoa maana za ushairi
na kuonesha msisitizo pamoja na kutofautiana katika maana zao kama ifuatavyo.
Kwa
mujibu wa Shaban Robert (1968) anafasili Ushairi ni sanaa ya vina
inayopambanuliwa kama nyimbo, mashairi na utenzi. Ushairi una ufasaha wa maneno
machache au muhutasari. Anaendelea kusema kuwa Shairi ni wimbo mkubwa, wimbo ni
shairi dogo na utenzi ni upeo wa Ushairi. Anazidi kufafanua kuwa kina ni
mlingano wa sauti za herufi, kwa maneno mengine huitwa mizani ya sauti na
ufasaha na uzuri wa lugha, mawazo, maono na fikra za ndani zinapoelezwa kwa
muhutasari wa ushairi huvuta moyo kwa namna ya ajabu.
Katika
fasili ya Shaban Robert anasisitiza kuwa shairi lazima liwe na urari wa vina na
mizani na hutumia maneno machache yenye ufasaha. Pia anadai kuwa mtu anaposoma
shairi huguswa ndani ya moyo kutokana na lugha ilivyotumika kwenye shairi hilo.
Kwa
mujibu wa Abdilatifu Abdalah (2003) anafasili Ushairi kuwa ni utungo ambao
katika kila ubeti wake kuna ulinganifu wa vina vitukufu vilivyopangwa kimoja
badala ya chenzie wenye vipande vilivyo na ulinganifu wa mizani zisizopungufu
wala zilizozidi. Vipande hivyo viwe vimetandwa na maneno ya mkato maalumu na
lugha nyoofu, tamu na laini, lugha ambayo ni telezi kwa ulimi kwa kuitamka,
lugha ambayo ina uzito wa fikra, tamu kwa mdomo na yenye kuathiri moyo
uliokusudiwa na kama ulivyokusudiwa.
Hivyo
Abdilatifu kama mtaalamu wa kimapokeo pia anasisitiza kuwa shairi huwa na
ulinganifu wa vina na mizani, pia anasisitiza kuwa shairi lazima liwe tamu na
utamu huo hutokana na maudhui yaliyopo kwenye shairi lenyewe.
Mathias
Mnyampala (1970) anafasili Ushairi kuwa ni maneno yenye hekima tangu kale,
ndicho kitu bora sana katika maongezi ya dunia kwa kutumia maneno ya mkato na
lugha nzito yenye kunata iliyopangwa kwa urari na vina maalumu kwa shairi.
Anasisitiza
katika urari wa vina na mizani huku akiegemea kwenye maneno yenye hekima yenye
lugha ya mkato na lugha nzito zenye kunata. Maneno yenye hekima ni maneno yenye
kufundisha, kuasa, kuonya na kuburudisha jamii. Lugha nzito ni lugha ambayo
hutumia misemo, nahau, tamathali za semi katika kufikisha ujumbe.
Kwa
mujibu wa Amri Abeid (1996) anafasili Ushairi ni wimbo, hivyo kama shairi
haliimbiki halina maana. Tunaona kuwa mtaalamu huyu msisitizo wake mkubwa
katika Ushairi ni uimbikaji wa shairi kuwa kama shairi haliimbiki basi shairi
hilo halina maana kabisa.
Mathalani
wanausasa pia wamefasili maana ya Ushairi na kuonyesha msisitizo pamoja na
tofauti katika maana zao kama ifuatavyo.
E,
Kezilahabi (1975) anadai kuwa Ushairi ni tukio au wazo ambalo limeonyeshwa
kutokana na upangaji mzuri wa maneno ya ili kuonyesha ukweli fulani wa maisha.
Hivyo tunaona kuwa msisitizo wake mkubwa uko katika maudhui ambayo yanaonesha
uhalisia Fulani wa maisha. Pia anasisitiza katika upangaji mzuri wa maneno.
Kwa
mujibu wa Mulokozi (1976) anafasili Ushairi ni mpangilio maalumu wa maneno
fasaha yenye muwala, kuwa lugha ya mkato katika usemi, maandishi au mahadhi ya
wimbo ili kueleza wazo au mawazo, kufunza au kueleza jambo au hisi Fulani
kuhusu maisha ya binadamu kwa njia inayoburudisha na kugusa moyo.
Tunaona
kuwa msisitizo wa Mulokozi katika fasili yake uko kwenye kufundisha watu na
kuburudisha watu. Pia anasisitiza kuwa shairi hugusa moyo kutokana na maudhui
au mambo yanayozungumzwa na kuamsha hisia.
Kwa
mujibu wa Wamitila (2010) anafasili shairi kuwa ni utungo wa sanaa ya lugha na
mpangilio maalumu wa mishororo au wa kisauti na kwa maneno mateule kwa kutumia
mbinu za kibalagha na kimtindo zinazomwezesha mtunzi kuwasilisha ujumbe kwa
ufupi na kwa mkokotozo mkubwa unaoeleza kisa, hisia, tukio au hali kwa lugha ya
mvuto.
Tunaona
kuwa katika fasili ya Wamitila anasisitiza zaidi katika vipengele vya fani na
maudhui kwani utumiaji wa lugha zenye mnato na mbinu nyingine ni sehemu ya
vipengele vya fani na maudhui. Pia anadai kuwa shairi hutumia lugha ya mvuto
ili kuweza kumvutia msomaji.
Pia
Njogu na Chimera (1999) wanafasili Ushairi kuwa ni sanaa ya lugha inayoeleza
jambo kwa njia ya mkato na kwa namna inavyoteka hisia za msomaji au
msikilizaji. Hivyo tunaona kuwa wataalamu hawa wanasisitiza katika usanaa wa
lugha kwenye Ushairi na utekaji hisia na lugha ya mkato katika Ushairi.
Ingawa
wataalamu wa ushairi wamefasili maana ya ushairi kwa msisitizo, pia washairi
wanatofautiana katika vipengele au mambo mbalimbali yanayohusu ushairi.
Yafuatayo ni mambo mengine yanayohusu ushairi;
Muktadha.
Kwa
mujibu wa Wamitila (2010) Muktadha ni kipengele kinachosaidia kufasili maana ya
ushairi, maana ya ushairi inaweza kutazamwa kwa kuchunguza muktadha wa
wasomaji, wakati au eneo na mwandishi au
kazi yenyewe ya fasihi. Muktadha huo huo unaweza kuwa asili ambao ni wa
kiusemaji au muktadha pokezi ambao ni wa kulipokea tamko ni wa kuipokea tamko.
K-Marx na Georg Lukas wanasema kuwa maana ya kazi ya kifasihi lazima itilie
maanani uhalisia wa kijamii. Mfano mabadiliko ya kijamii, mivutano ya kitabaka,
mifumo ya uzalishaji mali na mivutano ya kihistoria. Muktadha wa ushairi
umegawanyika katika sehemu tatu, kuna muktadha wa mahali huu unaonyasha
mabadiliko ya mahali au mazingira. Mfano kuna ushairi uliotungwa kabla ya
wakoloni, kipindi cha ujima, wakati wa ukoloni na ushairi uliotungwa kipindi
cha harakati za kupigania uhuru. Pia kuna muktadha wa mahusiano kibinasfi huu
unaelekeza kwenye wahusika wa utungo maalum. Utungo wa kishairi unaweza
kuangalia matumizi ya nafsi yaani inaweza kuwa nafsi ya kwanza au ya tatu.
Muktadha
mwingine wa ushairi ni wa kimwingiliano matini huu unavuka mpaka wa ushairi
mmoja maalum na kuhusisha muktadha wa shairi au utungo mwingine ambao
unadokezwa au kuelekezwa kwa njia moja au nyingine katika shairi linalohusika. Muktadha
wa kimwingiliano matini unapanua muktadha finyu wa ushairi na kuonyesha jinsi
ambavyo shairi lililotangulia kwa kukamilishana, kujihusisha kwenye usemezano wa
aina fulani au hata kuukana au kuukanusha mwelekeo, mtazamo na mwonoulimwengu
wake.
Utamaduni.
Ni kipengele kingine kinachoelezea ushari,
wataalamu wengi wa ushairi wameelezea utamaduni au asili ya ushairi. Mfano
Knappert (1979) “Four centuries of Swahili verse” anasema; ushairi wa Kiswahili
ulichipuka kutokana na nyimbo na ngoma za waswahili na ulianza katika karne ya
17. Na Jumanne, M. N (1993) anasema ushairi umetokana na jamii ya wanadamu
wenyewe na umesheheneza ukwasa mkubwa wa lugha ambayo imekuwa ikitumika tangu
enzi za kuishi mapangoni, enzi za ujima, uvamizi wa wakoloni na harakati za
kupigania uhuru. Pia kwa mujibu wa Senkoro (1987) anadai kuwa Ushairi asili
yake ni watu wa pwani.
Msisitizo
Ni
kipengele kinachoelezea ushairi. Wataalamu wengi wa ushairi wa kimapokeo
wanasisitiza matumizi ya vina na mizani na wanamamboleo wanasisitiza kuwa
shairi lazima liimbike. Pia wanazuoni wa kimapokeo na wanamamboleo, mfano
Shaaban Robert (1958), Topani (1974) na Kahigi (1982) wote wanasisitiza kuwa ushairi
lazima uilenge jamii kwa kuibuia hisia za jamii hiyo husika.
Kanuni
Wanamapokeo
wao wamejikita katika kufuata kanuni na sheria za ushairi. Mfano Shabaan Robert
(1968) anasisitiza katika kufuata urali wa vina na mizani huku wanausasa
hawafuati kanuni hizo za utunzi wa mashairii. Mashairi ya kimapokeo yote
yanazingatia kanuni za uandishi wa mashairi. Mfano matumizi ya urari wa vina na
mizani, kuwepo na kina, bahari au mshororo. Mashairi ya kisasa hayazingatii
kanuni hizi za matumizi ya vina na mizani bali yanaangalia matumizi ya arudhi
yaani shairi ili liwe shairi lazima liimbike.
Kwa
ujumla wataalamu wote wanamapokeo na wanamamboleo wanafanana katika maana zao
za ushairi kwa kiasi fulani kwa kuwa wote wanasema kuwa shairi lazima liibue hisia
kwa jamii husika na shairi lazima liimbike. Hivyo mashairi yawe ya kisasa au
yakimapokeo ni mashairi tu kwa kuwa yote yanalenga kunufaisha jamii kwa lengo
la kuelimisha jamii, kuburudisha jamii na kutunza amali za jamii.
MAREJELEO
Abeid, A.
(1954). Sheria za Kutunga Mashairi na
Diwani ya AMR. Nairobi: EALB.
Abdilatifu,
A. (1973). Sauti ya Dhiki. Oxford
London.
Kezilahabi, E. (1975). Ushairi wa Mapokeo na wa Wakati ujao.
Katika Mbonde J.P 121-137
Knappert, J. (1979). Four centuries of Swahili Verse. Heinemann. London.
Mayoka, J.K. (1993). Mgogoro wa
Ushairi na Diwani ya Mayoka. Ndanda Mission
Press.Tanzania.
Mulokozi, M.M. (1976). Fasihi ya Kiswahili. Chuo Kikuu cha
Dar-es-Salaam. Dar-es-Salaam
Mnyapala, M. E. ( 1970). Ngonjera za Ukuta. Dar es Salaam: Oxford
University Press.
Robert, S (1968). Kielelezo cha Insha. Nelson London.
Senkoro, F.E.M.K. (1987). Ushairi, Nadharia na Tahakiki.
Dar-es-Salaam: DUP.
Topan,F.
(1974). “Dibaji” katika Kezilahabi, ukurasa:x
Wamitila,
K.W. (2010). Misingi ya Uchanganuzi wa
Fasihi. Nairobi Kenya: Vide-Muwa.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com