Mbinu za Kubainisha Fonimu
Jozi ya Mlinganuo Finyu
Hii ni jozi ya
maneno inayotokea pale maneno mawili au zaidi yanakuwa na idadi sawa ya sauti
na ubadilishaji wa sauti moja katika mazingira yale yale utokeaji wa kifonetiki
wa sauti hizo katika neno huleta tofauti ya maana. Ikiwa sauti fulani tofauti
zitajitokeza katika neno hilo hilo na katika mazingira yale yale ya kifonetiki
na kubadili maana ya neno basi zinzchukuliwa kuwa ni fonimu mbili tofauti.
Mfano: bata-pata, kata-kaka, data-dada,
nk. Katika maneno haya ile sifa ya kifonetiki inayofanya sauti hizo ziwe
tofauti na kusababisha tofauti ya maana huchukuliwa kuwa nis sifa bainifu
katika lugha ya Kiswahili. Ikiwa tutaweka sauti yenye mpumuo, kwa mfano, sauti
sighuna maana haitabadilika ila itachukuliwa kuwa ni ukoseaji katika matamshi
na ila sauti hizo ni za fonimu moja kwani maana haitabadilika /katha/
- /kata/, /raha/ - /ma|itin/, /|aha/, nk. Katika Kiswahili tunaweza kusema kuwa kwa
kuwa sauti hizi hazileti tofauti ya maana basi ni ukengeufu tu wa matamshi ya fonimu
ile ile moja (kama vibadala vyake).
**Taja na
kufafanua sifa nne za jozi mlinganuo finyu: Idadi sawa za sauti, sauti
zinazobadili maana ziwe katika mazingira sawa ya kifonetiki, maana ibadilike,
sauti zinazobadili maana ziwe za aina moja (irabu kwa irabu, konsonanti kwa
konsonanti)*
Mtawanyo wa Kimtoano/Kamilishani
Huu ni mtawanyo
wa sifa za kifonetiki za sauti katika neno unaotokea pale ambapo sauti fulani
ikitokea katika mazingira fulani ya kifonetiki katika neno sauti nyingine ya
kundi hilo haiwezi kutokea. Dhana ya kukamilishana katika mtawanyo huu ina
maana kwamba sauti fulani (Y) haiwezi kutokea katika mazingira fulani (A) na
hivyo sauti nyenza hutokea ili kuikamilisha nyenziye iliyokwamishwa na
mazingira hayo katika kuelezea maana ile ile. Sauti zinazobadilishana mazingira
ya utokeaji wake katika neno huitwa alofoni au vibadala vya kimazingira.
Alofoni ni udhihirishwaji tofauti tofauti wa kifonetiki wa fonimu moja. Sauti
za namna hii pia huwa na kiwango kikubwa cha mfanano wa kifonetiki. Kwa
mfano: Ujitokezaji wa nazali katika Kiswahili zinapokuwa zinaambatana na
konsonanti nyingine. Mbao, nguo, ncha, nyayo, mvua, nk.
Mlandano (Mfanano) wa Kifonetiki
Hockett (1972:103)
kama anavyonukuliwa na Hyman (1975:64) anasema kuwa ‘kama sauti a na b ni memba
wa fonimu moja basi wanachangia sifa moja au zaidi. Sauti za familia moja zina
ufanano/mlandano mkubwa wa sifa za kifonetiki. Kwa mfano: Sauti /b/ na /B/
katika Kinyamwezi : ‘waBona’ (umeona) = ‘wambona’ (umeniona). Zote ni [+kons,
+mid, +ghuna] na tofauti ni [ufulizwa]. Kwa hiyo, /b/ na /B/ ni
alofoni za fonimu moja. Kwa mujibu wa kigezo hiki inaonyesha kwamba hata kama sauti
zinatokea katika jozi ya mlinganuo finyu na kubadili maana au kutokea katika
mtawanyo kamilishani kama ziko tofauti kabisa kifonetiki basi haziwekuwa sauti
za fonimu moja. Hata hivyo, kigezo hiki pekee hakitoshi kutumika kubainisha
fonimu na alofoni zake au fonimu mbili tofauti (taz. Hyman, 1975:64-65;
Massamba, 2012:75-76). Katika Kiswahili tunaweza kuuona utata wa kigezo hiki
katika kuelezea ufonimu na ualofoni wa /l/ kuwa [l] na [d]; na /r/ kuwa [r] au
[d]. Kwa mtu asiyekuwa na uelewa wa kiisimu hawezi kuelezea kuwa [l] na [d]
kuwa ni alofoni za fonimu moja katika maneno kama ‘refu’ na ‘ndefu’; ‘ulimi’ na
‘ndimi’ ingawa zote ni za ufizi. Pia haijabainishwa kuwa sauti hizo zinatakiwa
zifanane kwa kiwango gani cha kifonetiki. Hivyo, Hyman (1975) anasema kuwa ni
muhimu kuuchunguza mfumo mzima wa fonolojia inayochunguzwa.
Kigezo cha Mpishano Huru
Mpishano huru
hutokea pale ambapo sauti mbili zinaweza kutokea katika mazingira yale yale kwa
kubadilishana bila kusababisha mabadiliko ya maana ya neno. Katika hali hii
sauti hizo huitwa vibadala huria au vibadala vya hiari vya kifonetiki. Trubetzkoy
(1969) anasema kuna vibadala huria vya aina mbili: Vya Kimajumui na
Kibinafsi. Vibadala vya Kimajumui ni vile ambavyo havichukuliwi kuwa ni
kama kosa au dosari katika matamshi. Mzungumzaji huyo huyo mmoja anaweza
akatamka kwa kibadala hiki wakati huu na baadae kwa kibadala kingine: Kwa
mfano: Kichuguu, kusuguu, suala/swala; kheri-heri. Ubadilikaji wake
unategemea hali ya mtu na wazungumzaji wote wanaweza kutumia vibadala hivyo
kulingana na mazingira. Vibadala vya kibinafsi ni vile vilivyosambaa miongoni
mwa baadhi ya wanajamii lugha husika. Katika hali kibadala kimoja huchukuliwa
kuwa ni utamkaji sanifu/mzuri na vibadala vingine huchukuliwa kuwa ni mkengeuko
wa kilahaja, kijamii (sifa, umaarufu, umjini-mjini) au kimaumbile. Mfano: /|/ na
/r/; /a/ na /«/ katika neno /raha/ na /|«ha/;
/kurara/ na /kulala (katika lugha yao pengine /r/ na /l/ ni alofoni); /ntoto/ na /mtoto/, tatu na /thatu/;
nk. Katika Kiswahili kuna vibadala ambavyo vinaonekana kuwa ni sauti za
fonimu mbili tofauti na hutokea katika mpishano huru kama vile; kisuguu-kichuguu,
kichogo –kisogo, kiberiti-kibiriti, kheri na heri. Vibadala hivi pia
vinaonekana kuwa vinafanana kifonetiki kwa sehemu kubwa. Kama vibadala hivyo,
kimojawapo hakimo kabisa katika orodha ya fonimu za lugha husika basi
huchukuliwa kuwa ni vya fonimu moja. Swadesh (1934) kama anavyonukuliwa na
Fudge (1973:36) amevigawa vibadala huria kuwa ni vya Kijumla na Kimahususi. Vya
kimahususi ni vile vinavyotumika katika neno moja au maneno machache kadhaa na
vile vya kijumla ni vile vinavyoweza kutumika katika maneno yote ya kundi
fulani. Mifano katika Kiswahili maneno yote yanaoanza na /m/ na kufuatiwa na
/h/ huwa yanaififiza /h/ au kuidondosha katika usemaji wa haraka haraka na
badala yake wanaiyeyusha /u/ iliyokuwepo katika umbo la ndani na kutamka /w/:
Mfano mhuni, muhogo (mhongo), mhanga, mhandisi, mheshimiwa, mheshimu, nk.
(Kijumla). Kimahususi (kiberiti-kibiriti, kheri-heri, ahsante-asante,
ghuna-guna, nk).
Ulinganifu wa Ruwaza
Kigezo hiki
kinadai kuwa, tunaweza kupata namna ya kubaini fonimu na alofoni kwa kuangalia
ujitokezaji wa sauti fulani katika mfumo mzima wa fonolojia ya lugha husika.
Kama sauti fulani inajitokeza kwa namna fulani katika mazingira fulani basi iwe
hivyo katika mfumo mzima wa fonolojia ya lugha husika. Kwa mfano hakuna
mahali katika Kiswahili Nazali /N/ ikifuatiwa na konsonanti fulani haitafuata
mahali pa matamshi pa konsonanti hiyo. Kwa hiyo mtawanyo huo wa kimtoano
uwe katika mfumo mzima wa fonolojia ya Kiswahili. Pia katika Kiswahili tunasema
sifa ya mpumuo si bainifu, basi iwe hivyo katika mfumo mzima ndipo tutasema
katika lugha hii sauti yenye mpumuo ni alofoni ya fonimu husika. Kama pia
tunavyosema kuwa katika Kiswahili hakuna irabu unganifu, basi iwe hivyo katika
mfumo mzima; fonimu za upili (kama ts, dz, bl, bd, pw, nk) basi iwe
katika mfumo mzima. Au ikiwa katika lugha ya Kiswahili kuna sauti /C/ basi isitokee kwamba katika baadhi ya
maneno kukawa na mfuatano wa /t/ na /S/,
yaani /tS/ ( [ tSati]
badala ya [Cati] ). Ndiyo
maana katika mfuatano wa nazali na sauti za kaakaalaini katika mfumo mzima wa
fonolojia ya lugha ya Kiswahili nazali hupata sifa za kuwa nazali ya
kaakaalaini na ili uipate nazali hiyo ni lazima iwe katika mfuatano huo katika
mfumo mzima wa fonolojia ya Kiswahili. Ikitokea vinginevyo basi kunakuwa na
mkengeuko wa fonolojia ya Kiswahili sanifu. Hata hivyo kigezo hiki tu hakitoshi
kwani kuna mifuatano mingine bado ina utata kama vile /ng/, mahali pengine ni /N/ na
mahali pengine ni /Ng/.
Aidha, mfuatano wa nazali na konsonanti nyingine unazaa konsonanti za upili,
mfano; /nd, ng, mb/ nk au ni konsonanti moja yenye kutanguliwa na unazali?;
mfano /nd/ (kuna utata). Kigezo kimoja tu hakitoshi kubainisha
fonimu na alofoni ila vitumike vyote viwili.
Kigezo cha Kubadilishana kwa sauti
Kigezo
hiki hutumika kwa kujaribu kubadilisha sauti fulani na sauti nyingine halafu
unaangalia kama ubadilishaji huo unaleta mkengeuko mkubwa katika utamkaji au
la. Kama mkengeuko si mkubwa/wa kawaida basi sauti hiyo itachukuliwa kuwa ni
alofoni ya fonimu moja na ukiwa mkubwa basi itakuwa ni fonimu tofauti. Hata
hivyo, kigezo hiki hutegemea sana hisia za mzawa wa lugha hiyo. Mfano:
Katika Kiswahili= Uu ni wangu (Huu ni wangu); [¬fE] (uje) (eje au oje)
Hapa
tunaweza kuhitimisha kuwa ni muhimu sana kutumia vigezo vyote pale unapojaribu
kuzibainisha fonimu za lugha fulani. Swadesh (1934) (taz. Fudge 1973:35-46)
anasema kuwa katika kujifunza fonimu za lugha fulani ni muhimu ufanye
yafuatayo: Uzibainishe, ujue tabia za utokeaji wake na mabadiliko yake katika
mazingira fulani, ujuea msambao wake na kisha ujifunze mfumo mzima wa fonimu
hizo katika lugha husika.
Inapendeza.....👏🏾👏🏾👏🏾👏🏾
ReplyDeleteUbarikiwe
DeleteUchambizi nimeuelewa vizuri ila ulipaswa kutuonesha uhusiano au usaidianaji wa mbinu hizo katika kubaini fonimu.Asante
ReplyDeleteAsnte kwa kuonyesha uchambuz huo lakin sasa kama kichwa cha swal knavosema mbinu za kubaini fonimu na alofoni ,,je kupitia izo mbinu unabaishaje???
ReplyDeleteNimependa sana udadafuzi huu kwani umenipa mwanga maana nilikuwa najiuliza sana nifanyeje ili nibaibi fonimu za lugha yangu
ReplyDelete