Flower
Flower

Friday, November 24, 2017

FONOLOJIA




1.2       Fonolojia ni nini
Fonolojia ni tawi la Isimu linalojishughulisha na ujifunzaji wa mfumo wa sauti za lugha maalumu asilia. Huangalia jinsi sauti zinavyotumika katika maneno ya lugha maalumu ili kuleta maana. Hivyo huangalia muundo na uamilifu wa sauti hizo katika mfumo wa lugha maalumu kwani kila lugha ina mfuatano wake wa sauti katika kuunda maneno yake. Kwa hiyo, kila lugha ina fonolojia yake ingawa kuna sifa chache zinazofanana, na hii hutokana na kwamba lugha zote huchota sauti toka bohari moja la sauti. Fonolojia hizi hutofautiana kwa kiasi kikubwa kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, kila moja huchota sehemu ndogo tu ya sauti toka katika bohari la sauti kitu ambacho hupelekea kuwepo na tofauti ya baadhi ya sauti.
Pili, mpangilio wa mfuatano wa sauti  hutofautiana katika kila lugha. Katika Kiswahili baadhi ya mfuatano wa sauti hauwezi kutokea mwanzoni mwa neno; mfano *#nwa-,
Tatu, michakato na kanuni zinazoathiri mabadiliko ya sauti (muundo wa sauti) hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Huweza kufanana baadhi lakini si michakato yote.
Nne, sifa bainifu ya sauti katika lugha fulani si lazima iwe bainifu katika lugha nyingine   (pia urefu wa irabu, mpumuo, mkazo kutofautisha maana, toni, n.k. hutofautiana baina ya lugha na lugha).
Tano, uziada na umsingi wa sifa bainifu za sauti. Katika lugha moja sifa fulani huweza kuwa ni ya msingi na kinyume chake. Mfano mpumuo katika Kiswahili sanifu ni sifa ya ziada lakini katika Ki-Mtang’ata ni sifa ya msingi kwa maana kwamba hutofautisha maana ya neno na neno.
Sita, kila lugha ina muundo wake wa silabi. Lugha fulani huweza kuwa na silabi huru na nyingine silabi funge.
Saba, kila lugha ina mfumo wake wa irabu nyingine irabu tatu, nyingine 4, 5, 6, 7 n.k.
Nane, Pia katika suala la fonimu na alofoni. Alofoni katika lugha fulani huweza kuwa ni fonimu inayojitegemea katika lugha nyingine na kubadili maana.

Maarifa ya fonolojia ambayo mtu hujifunza ni:
1.     Maarifa ya sauti (vipandesauti) za lugha X (konsonanti na irabu)
2.     Maarifa ya muunganiko unaokubalika wa sauti hizo katika lugha X (sauti ipi haiwezi kufuatana na ipi)
3.     Maarifa ya Vipengele Arudhi vya lugha X (silabi, mkazo, toni, kiimbo, nk)
4.     Maarifa ya kimofofonolojia ya lugha X (kwa mfano: kwa nini kuna MU, MW na M kama alomofu za mofu moja ya umoja katika ngeli ya kwanza)
5.     Mabadiliko ya sauti na Michakato (kanuni/taratibu/mashartizuizi) vinavyojitokeza pale ambapo sauti zinapokaribiana, na ni sauti zipi hizo na katika mazingira gani.

1.3       Uhusiano Uliopo Baina ya Fonetiki na Fonolojia

Fonolojia na fonetiki ni matawi tofauti ya isimu fafanuzi lakini yenye uhusiano mkubwa sana. Katika kuangalia uhusiano baina ya fonetyiki na fonolojia, tutaangalia kuingiliana na kutofautina kwa matawi haya.

1.3.1    Tofauti kati ya Fonetiki na Fonolojia    
  1. Fonolojia hushughulikia sauti katika lugha maalumu wakati fonetiki hushughulikia sauti zote za lugha za binadamu
  2. Fonolojia inahusu mfumo wa mfuatano wa sauti katika kuunda maneno ya lugha fulani maalumu; mfano: /­a­a/ ; ‘nyanya’ ikiwa fonetiki inahusu sifa za kifonetiki za sauti moja moja [p], [a], [j], nk
  3. Fonolojia inahusisha na michakato na kanuni za kifonolojia (udondoshaji, uyeyushaji, nk) ikiwa Fonetiki haihusishi masuala ya kanuni na michakato
  4. Fonolojia huchunguza sifa bainifu tu, yaani zile zenye maana katika lugha husika katika kujifunza fonolojia ya lugha fulani wakati fonetiki hujumuisha sifa zote za kifonetiki za sauti katika kujifunza fonetiki ya lugha za binadamu
  5. Fonolojia ina ukomo wa orodha wa sauti lakini fonetiki haina ukomo wa orodha ya sauti (au orodha yake ni ndefu sana)
  6. Kipashio cha kifonolojia ni fonimu kinachowakilishwa katika mabano mshazali /p/ lakini kipashio cha fonetiki ni foni kinachowakilishwa katika mabano upinde [p]
  7. Fonolojia inahusisha vipengele dhahania vya kisaikolojia, yaani ‘ile maana iliyomo katika akili ya mzungumzaji na husaidia kuona jinsi akili ya mzunguzaji na msikilizaji zinavyofanya kazi katika utumiaji wa sauti hizo. Fonetiki yenyewe inahusu sifa zilizo yakinifu na zinazojaribika (mfano utamkaji, usikiaji na usafirishaji wa mawimbisauti). Vitu hivi hupimika na kuthibitika katika maabara za lugha.
  8. Fonetiki huchunguza tabia za sauti za kiutamkaji, kiusafirishi na kimasikizi wakati fonolojia huangalia jinsi sauti zinavyohusiana na zinavyotumika katika lugha maalumu ili kuleta maana. Kwa hiyo, fonolojia inahusu muundo wa vipande sauti hivyo katika neno na uamilifu wake.
  9. Nk.

1.3.2 Kukamilishana na kuhusiana kwa Fonetiki na Fonolojia

  1. Kuna vipengele na dhana za kifonetiki vinavyotumika kuelezea fonolojia; kwa mfano sifa za sauti
  2. Huwezi pia kupata fonetiki pasipo kujifunza fonolojia za lugha mbalimbali. Bohari kuu la sauti limechangiwa pia na utafiti uliofanywa wa fonolojia za lugha mbalimbali. Ili uijue sauti fulani ni lazima uende katika fonolojia ya lugha yenye sauti hiyo
  3. Taaluma zote mbili zinahusu sauti za lugha
  4. Fonetiki pia huweza kutumika katika lugha moja maalumu bila kuchukulia fonetiki kimajumui. Lakini pia fonolojia huweza kuangalia vipengele vya kifonolojia vya kimajumui katika lugha zote asilia na ikiwa hivyo si tena lugha moja maalumu.
  5. Nk.

Kwa hiyo, fonolojia na fonetiki ni taaluma zinazokaribiana sana. Kuna vipengele vya kifonetiki vinavyotumika kuelezea fonolojia. Hivyo fonetiki ni msingi wa fonolojia lakini fonolojia vilevile ni msingi wa fonetiki, ili kuijua sauti lazima uende kwanza kwenye fonolojia. Aidha, kila lugha ina fonetiki yake pia kama ambavyo ina fonolojia yake.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny