Flower
Flower

Friday, November 24, 2017

FONETIKI




1.1       Fonetiki ni nini?
Ni taaluma ya sauti za lugha ya mwanadamu (Kindija,2012). Tawi hili la isimu limegawanywa katika matawi madogo matatu:

1. Fonetiki Matamshi: Ni tawi ambalo lonajishughulisha na utamkaji wa sauti za lugha ya mwanadamu. Tawi hili linajumuisha mahali pa matamshi, jinsi sauti zinavyotamkwa, mkao wa glota na mkao wa mdomo.

2. Fonetiki Safirishi/Akustika: Ni tawi la fonetiki linaloshughulikia na kuchunguza jinsi sauti zinavyosafiri kutoka kwa msemaji hadi kumfikia msikilizaji. Huhusisha misikiko na mawimbi ya sauti na jinsi yanavyosafirishwa kutoka kwa msemaji hadi kwa msikilizaji. Huchunguzwa maabara kwa Spektrogramu. Hutazama pia vijenzi vya sauti kwa kutumia vifaa vya mmabara.

3. Fonetiki masikizi: Ni tawi linalohusu uchunguzi na uchanganuzi wa jinsi sauti za lugha zinavyokamatwa na sikio na kusafirishwa kwenda kwenye ubongo kupitia neva zinazohusika na usikiaji.

Lugha ya mwanadamu imejengwa na sauti na uzalishaji wa sauti hizi hutokana na muungano wa mambo yafutayo:
Mfumo wa Mkondohewa, mkondosauti na ala za sauti

Mkondohewa: Ni funda la hewa inayosafiri kuingia ndani au nje ya mapafu katika uzalishaji wa sauti. Mkondohewa umegawanyika katika aina tatu ambazo ni:
(a)                Mkondohewa wa mapafuni (pulmonic)  ambapo hewa hutoka mapafuni kwenda nje
(b)               Mkondohewa wa glota ambapo hewa ya kwenye koromeo husukumwa na mwendo juu au chini wa glotisi liyofunga. (mfano baadhi ya sauti za kiarabu
(c)                Mkondohewa wa kaakaa laini (velaric) ambao huhusu mzunguko wa hewa ya mdomoni. (mfano: vidoko = > kidoko cha midomo)

Mkondohewa huu pia upo wa ndani na wa nje. Mkondohewa ndani huhusu mtiririko wa hewa kuelekea ndani ya mapafu (sauti kama [º] - Kimatumbi) na mkondohewa nje huhusu mtiririko wa hewa kuelekea nje ya mapafu.
Mkondosauti ni njia ambamo hewa hupita. Hujumisha chemba ya kinywa au chemba ya pua. Mkondosauti huu huwa na ala za sauti ambazo hutumika kuzalishia sauti. Ala sauti ni viungo vitumikavyo  kutamkia sauti ingawa huwa na kazi nyingine pia za kibaiolojia. Ala hizi ni:

  1. Midomo ya juu 2. Meno 3. kakakaa gumu 4. kakakaa laini 5. kidaka tonge 6. midomo 7 ulimi 8. Kongomeo (glota na nyuzi sauti 9. Ufizi .
                                                                                          
Sauti zinaundwa kwa kutumia mambo haya yote ili kuunda bohari la sauti ambalo husaidia lugha asilia kuchukua sauti chache tu zinazotumika na kuunda orodha ya  kifonetiki ya sauti ya kila lugha ambazo mjifunza lugha wa lugha hiyo hana budi kuzijua na kujua jinsi zinavyotumika katika mfumo wa mfuatano wa sauti wa lugha hiyo. Kwa hiyo, ujifunzaji wa uzalishaji wa sauti kwa ujumla ndiyo fonetiki na ujifunzaji wa mfumo wa sauti katika lugha maalumu ndiyo fonolojia.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny