SARUFI
FINYIZI
Maana ya sarufi finyizi
Sarufi finyizi ni nadharia ya
kisarufi ambayo inaangazia utaratibu wa kuchunguza lugha ulio na unyumbufu wa
mielekeo tofauti inayowezeshwa na ufinyizi wake. Sarufi finyizi imekuwa ikikua
ndani ya nadharia ya hapo awali ya sarufi zalishi tangu miaka ya tisini. Hasa
hujikita katika kueleza sifa za kijumla ambazo lugha ya mwanadamu huwa nazo.
Nadharia hii ilianzishwa na
mwanaisimu wa Kimarekani na mwenye asili ya Uyahudi Noam Chomsky. Katika sarufi
finyizi, Chomsky anaiwasilisha sio hasa kama nadharia bali kama utaratibu wa
uchunguzi wa lugha. Nadharia hii ilijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka wa 1993
kupitia kazi yake Chomsky "A
minimalist program for linguistic theory."
Hata hivyo, nadharia hii aliiweka wazi mwaka wa 1995 katika
chapisho lake "The Minimalist Program." Baadhi ya watu
waliowahi kuirejelea na kuizungumzia nadharia hii ni kama vile Webelhuth (Tah) (1995), Brody (1995), Cook na
Newson (1996), Radford (1997) miongoni mwa wengine.
Sarufi finyizi ni maendelezo na uboreshaji wa nadharia ya
sarufi zalishi iliyoanzishwa na Chomsky mwenyewe alipoizungumzia kwa mara ya
kwanza mwaka wa 1957 katika chapisho lake “Syntactic
Structures.’
Sarufi zalishi ilianza hasa kwa kutofautisha dhana mbili kuu
ambazo ni umilisi lugha na utendaji lugha. Pia ilitambulisha muundo nje na
muundo ndani. Muundo ndani uliwakilisha umilisi nao muundo nje ukawakilsha
utendaji.
Kufuatia sarufi finyizi, dhana ya muundo ndani iliondolewa
ikabaki ile ya muundo nje pekee. Aidha vinadharia vilivyoongoza uchanganuzi wa
sentensi viliondolewa na vikageuzwa kuwa kanuni za kisintaksia katika sarufi
finyizi. Jambo hili linaangaliwa kuwa na umuhimu wa kuifanya nadharia ya lugha
kuwa na uwekevu zaidi na urahisi kuliko sarufi panuzi ya awali.
Sarufi finyizi inajikita katika kuendeleza malengo ya sarufi
zalishi ambayo yanahusisha kuandaa sintaksia bia ya lugha. Hii ina maana ya
sarufi ambayo inajumlisha kanuni zinazoweza kudhihirika katika lugha yoyote ya
mwanadamu. Hivyo basi, sarufi ya kijumla inayoeleza sifa zinazopatikana katika
lugha zote za mwanadamu inazingatia maongozi maalum. Haya ni pamoja na sifa ya
kuwa na ufafanuzi toshelevu, uasilia wa lugha inayochunguzwa, upekee wa lugha
ya mwanadamu na ujumla wa tanzu zote za lugha. Pia utumiaji wa vipengee
vichache vyenye utoshelevu (ufinyizi) na urahisi au wepesi wa kueleweka.
Aidha, sarufi finyizi inalenga kutafuta uhusiano kati ya
nadharia ya isimu na tanzu nyinginezo za lugha kama vile miundo ya fasihi na
falsafa ya lugha.
Nadharia ya sarufi finyizi inajikita katika imani kuwa
kunayo idadi maalum ya sheria ambazo hufanya kazi kwa lugha zote za mwanadamu.
Pia inashikilia kwamba kuna mseto wa sifa unaoweka msingi wa mfumo anaopata
mtoto mzawa wa lugha fulani na ambao unamwezesha kuipata lugha kwa urahisi.
Chomsky (1995) anahoji kwamba yapo maswali yazuliwayo na
sarufi finyizi tu ila majibu yake yanaweza kufafanuliwa katika nadharia yoyote.
Kwake, swali muhimu zaidi kati ya yote ni lile linaloulizia sababu za lugha ya
mwanadamu kuwa na sifa inazodhihirika kuwa nazo. Hivyo basi, sarufi finyizi
inaandaa mtazamo mahsusi wa misingi ya sintaksia katika sarufi ya lugha. Katika
hali hii, sarufi finyizi inapolinganishwa na mifumo mingineyo inatazamika kama
nadharia.
Mhimili mwingine muhimu wa sarufi finyizi ni kuwa utendaji
wa lugha miongoni mwa watu ni ishara tosha inyothibitisha mfumo komavu ulio na
mpangilio maalum. Suala hili linaelekeza kwamba mfumo wa lugha umeingiliana na
kurandana na kanuni nyepesi ya matumizi yake au kuhimiliwa ama na kiungo au
kitivo fulani maalum katika ubongo wa binadamu.
Hii ni kumaanisha kwamba sarufi finyizi inajiegemeza katika dai eti
sarufi bia inajumlisha muundo toshelevu unaofanikisha mahitaji ya ufahamu na
yale ya kimatamshi.
Katika mtazamo wa
kinadharia na muktadha wa sarufi zalishi, sarufi finyizi inaainishwa kama
mtazamo wa kanuni na sheria unaoangaliwa kuwa kielelezo cha upeo wa nadharia
ambayo imekuwa ikikuzwa na kuendelezwa na isimu zalishi tangu miaka ya
themanini. Mtazamo huu unachokieleza ni kuwepo kwa mseto maalum wa sheria
zinazotumika katika lugha zote. Sheria hizi zikishirikishwa kwa miundo fulani
ya kanuni zenye idadi mahsusi hueleza sifa za mfumo wa lugha ambao mtoto mzawa
wa lugha hiyo huja kupata.
Sarufi finyizi inatambulisha jumla ya kategoria nane za
maneno ambazo zinagawika katika matapo mawili. Tapo la kwanza ni lile la
kileksia na la pili ni lile la kisarufi
Tapo la kileksia linahusisha kategoria za maneno ambazo
zinawakilisha maana msingi au maana za kileksia. Kategoria hizi ni tano kama
ifuatavyo:
i)
Nomino
ii)
Kitenzi
iii)
kivumishi
iv)
kielezi
v)
Kielezi
Tapo la kisarufi huwa na kategoria
za maneno ambayo hayawakilishi maana ya kimsingi. Maneno haya huwa na umuhimu
wa kuendeleza maana ya maneno ya kileksia. Kategoria hizi za kisarufi ni tatu:
i)
Kibainishi
ii)
Kishamirishi
iii)
Kipatanishi
.
Kutokana
na maelezo haya, ni wazi kuwa sarufi finyizi inatumika
kufafanua na kuchanganua sentensi za Kiswahili. Sarufi finyizi inatambulisha
sentensi sahili kama kishazi huru na kuchukulia utanzu wa sintaksia kuwa msingi
zaidi.
Urahisishaji wa jinsi ya kuchanganua
sentensi kwa kuondoa muundo ndani na muundo nje huenda una manufaa lakini
itachukua muda kujenga uzoevu wa hatua zilizopendekezwa. Pia kuondolewa kwa
vile vinadharia na kupunguzwa kumeondoa utata pamoja na kutupilia mbali dhana
ya x-baa na ile nadharia ya utawala na ufungamanisho.
Japo sarufi finyizi ilipata uungwaji mkono na wasomi
wanaisimu, kunao waliipinga mwishoni mwa miaka ya tisini. Kwa mfano, David E. Johnson na Shalom
Lappin
katika jarida la Natural Language and Linguistic Theory wanadai kuwa
sarufi finyizi haikutokana na mtazamo wa kisayansi na hivyo haikuwa na
malengo yoyote ya kiusomi bali ni dhana
iliyotokana na Chomsky kutaka tu kujidai na kunadhifisha nadharia ya awali ya
lugha.
Wanadai kuwa kukubalika kwa sarufi finyizi hakukuwa na
manufaa au ishara zozote za mapinduzi ya kisayansi katika isimu ila ni kutokana
na nafasi na mchango wa hapo awali wa Chomsky katika taaluma ya isimu.
Kutokana na hali ya nadharia hii kuendeleza sarufi bia, ni
wazi kwamba sarufi finyizi hutumika kueleza vipengee vya lugha yoyote ya
mwanadamu.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com