TUKI (1990) wanasema urejeshaji ni tendo la kuweka kiwakilishi ambacho huweza kutumiwa kupatanisha kishazi kinachojirejea na kukivumisha kikundi nomino hicho. Yaani kishazi rejeshi kinafanya kazi ya kuvumisha Nomino katika kikundi nomino hicho.
Tungo rejeshi ni tungo tegemezi ambayo hutegemezwa kwenye kundi nomino. Wengine wanasema ni uhusianishaji wa maneno kisarufi ambapo tungo rejeshi hurejelea kwenye neno kuu (kisabiki) la kifungu chote. Kuna uhusisano wa moja kwa moja kati ya kile kinachoelezwa katika tungo rejeshi na kile kisabiki kinachorejelewa.
Ili kuwa na kishazi bebwa katika sentensi moja inayotokana na sentensi mbili, kishazi kimoja hakina budi kupachikwa ndani ya kishazi kingine yaani kubebwa na kishazi kingine. Hii ni sawa na kusema kuwa kishazi kimoja kinashushwa hadhi na kukipachika ndani ya sentensi nyingine baada ya KN cha sentensi husika.
Kishazi rejeshi ni sentensi iliyoshushwa hadhi na kufanya kazi ya KN (ndani ya KN).
Mwalimu anaasoma kitabu
Kitabu ni kizuri
Tungo rejeshi ni aina mojawapo ya tungo tegemezi, na tungo tegemezi ni sentensi iliyoshushwa hadhi na kutegemezwa katika sentensi nyingine. Tungo tegemezi haitokei peke yake bali hutokea kama sehemu ya sentensi, na kimuundo tungo tegemezi huwa kiambajengo ama cha sentensi kuu au kiambajengo kingine cha sentensi hiyo (Mekacha, 1987). Sentensi hiyo au kishazi hicho kina kiima na kiarifu ndani yake licha ya kutegemezwa katika sentensi nyingine.
Mtoto meondoka.
Mtoto aliyekuja jana ameondoka.
Mtoto alikuja jana. kiima kiarifu
Massamba (2009) anafafanua kishazi rejeshi kuwa ni kishazi ambacho kina uamilifu wa kurejea kwenye kirai nomino ambacho kinakibeba. Kwa upande wa dhana ya kishazi bebwa anafafanua kuwa ni kishazi ambacho hakiwezi kujitegemea chenyewe na ambacho kimechopekwa ndani ya kishazi kingine kikuu. Kwa mfano; Watoto watakaofaulu mitihani yao vizuri watapata zawadi. Katika sentensi hii maneno yaliyopigiwa mstari ndio yajulikanayo kama kishazi bebwa.
Ukunjiano wa sentensi unahusu sentensi moja au zaidi kukunjiwa ndani ya sentensi nyingine na ukunjiaji huu huegemezwa katika kirai nomino. Hii ina maana kuwa kunakuwa na sentensi mbili zenye kutimiza kanuni za ukunjiano kisha sentensi moja hukunjiwa ndani ya kirai nomino cha sentensi nyingine na kufanya kazi kama kiambajengo cha kirai nomino hicho na sentensi kuu. Mathalani mfano ufuatao unashadidia maelezo hayo.
Mtoto ameondoka.
Mtoto alikuja jana
Katika sentensi hizi ambazo ni sentensi sahili, sentensi ya pili inakunjiwa ndani ya sentensi ya kwanza na kuwa kama kiambajengo cha sentensi hiyo. Kwa hali hiyo sentensi hiyo itakuwa;
[Mtoto [Mtoto alikuja jana] ameondoka] Mtoto aliyekuja jana ameondoka
Hivyo sentensi ya pili sasa inafanya kazi kama kijenzi au kiambajengo cha KN cha sentensi kuu. Kinafanya kazi ya kukumusha KN kilichotangulia. Kikumushi ni kusema kitu juu ya kitu kingine. Kikumushi chaweza kuwa kivumishi cha kawaida, kirai/kishazi rejeshi, kielezi katika analia sana. Huu ni urejeshi ambao kwa hakika haufanyiki kiholela bali kuna masharti ambayo hufuatwa ili kukamilisha dhana ya ukunjiaji wa sentensi sambamba na masharti ya utokeaji wa muunganiko huo wa vishazi viwili.
Kuna michakato/mikakati mitatu ya urejeshi au inayofanya uwepo wa ukunjiano. Mikakati hiyo ni;
Mkakati wa urejeshi wa umbo amba- (Kutumia amba- Umbo kamili) ambao kirejeshi huambikwa mwishoni na kuwa na muundo Amba + REJ. Kwa mfano; Mtoto ambaye alipotea amepatikana. Urejeshi huu hautumiki ikiwa njeo ziko katika hali moja yaani mofimu ya wakati katika kirejeshi inafanya kazi sawa na mofimu ya sentensi kuu.
Aina ya urejeshi ambayo kirejeshi kinaambikwa katikati ya viambishi awali. (Kutumia kiambishi cha urejeshi-umbo lisokamili), hali timilifu haihusishwi. Yaani nyakati, muda wa tendo huondolewa. Muundo wake huwa ni wa; VIAMBISHI AWALI + REJ + SHINA (T). Mfano wa sentensi; Mtoto aliyekuja jana ameondoka leo.
Kirejeshi kinachoambikwa mwishoni mwa kitenzi. Kitenzi au kirejeshi hicho nacho huwa na muundo wa KITENZI + REJ#. Muundo huu hutumika kuonyesha hali ya mazoea, hivyo kitenzi kinachoambikwa mwishoni katu hakiambishwi mofimu ya wakati na ikiwa kinyume chake, sentensi itakuwa haikubaliki
Kutokana na mikakati hiyo ya urejeshi, mkakati wowote ule husababisha sentensi moja kukunjiwa ndani ya sentensi nyingine na kufanya kazi kama kijenzi cha sentensi kuu.
Masharti ya kutokea kwa muunganiko wa vishazi viwili (masharti ya urejeshi)
Kama tulivyokwisha kueleza kuwa muunganiko wa vishazi viwili kuwa sentensi moja hautokei kwa bahati na wala si kila kishazi kinaweza kuunganishwa na kishazi kingine. Ili kuweza kufanikiwa kwa usahihi kuunganisha vishazi viwili au kubebesha vishazi viwili, ni dhahiri kuna masharti yanayostahili kutimizwa. Baadhi ya Masharti yanayofafanuliwa pia na Mekacha (1987) ni pamoja na;
Sharti pawepo na sentensi mbili sahili ambazo sentensi moja itakunjiwa ndani ya sentensi nyingine. Kwa mfano;
(a) Mtoto anacheza mpira .
(b) Mtoto ameumia mguu.
Nomino zinazotajwa katika sentensi zote mbili ni lazima ziwe ni zile zile au zinarejerea kitu kilekile. Yaani kuwe na sentensi mbili zenye nomino yenye kurejelea kitu kile kile. Huku kurejelea kitu kilekile ndiko kunakotoa mwanya wa kugeuza nomino mojawapo kuwa kiwakilishi rejeshi badala ya kiwakilishi kamili. Katika mfano wa hapo juu (katika i) nomino Mtoto katika sentensi ya kwanza na ya pili inamrejerea Mtoto yule yule anayecheza mpira na aliyeumia. Ikiwa sentensi zina nomino mbili tofauti au ambazo hazirejelei kitu kilekile ni dhahiri urejeshi hauwezi kufanyika. Mfano ufuatao unadhihirisha maelezo haya.
(a) Mwalimu anafundisha.
(b) Askari analinda.
Katika sentensi hizo nomino Mwalimu na Askari hazirejelei kitu kilekile kwa hiyo ni vigumu kwa kishazi kimoja kubebwa na kishazi kingine.
MUHIMU: Hakikisha kirejeshi kinakuwa karibu na kisabiki chake. Nomino ya kishazi bebwa ambayo imegeuzwa kuwa kirejeshi ni sharti kikae karibu na kirejelewa chake. Kwa mfano;
(a) Mtoto anacheza mpira.
(b) Mpira ni mzuri.
Katika ukunjiaji wa kishazi cha pili sentensi itakuwa;
[Mpira [Mtoto anacheza mpira] ni mzuri] [Mpira [mtoto anacheza ambao] ni mzuri]
Katika sentensi hiyo iliyopigiwa mstari kirejeshi kiko mbali na kisabiki chake hivyo sentensi haiwezi kuleta maana kwa hiyo kirejeshi kitatakiwa kuletwa karibu na kisabiki chake ambacho ni Mpira. Kibadala au kirejeshi kinawekwa kimoja na sharti kiendane na nomino husika na huakisi ngeli husika.
Kiwakilishi rejeshi kinafungashwa kwenye umbo linalokubali kulibeba
Kiwakilishi rejeshi si mofimu huru bali ni kiambishi na pia umbo lake hubadilika kwa kufuatana na ngeli ya nomino husika.
JEDWALI LA KUONYESHA MOFIMU REJESHI/VIWAKILISHI REJESHI ZINAZOTUMIKA KATIKA UREJESHI
Namba
Aina ya Ngeli
Viambishi awali vya kitenzi
Mofimu za urejeshi
1
A Wa
A
Wa
-o-
-ye-
2
U I
U
I
-o-
-yo-
3
Li Ya
Li
Ya
-lo-
-yo-
4
Ki Vi
KI
Vi
-cho-
-vyo-
5
I Zi
I
Zi
-yo-
-zo-
6
U Zi
U
Zi
-o-
-zo-
7
U Ya
U
Ya
-o-
-yo-
8
Ku-
Ku-
-ko-
9
Pa - Mu – Ku
Pa
Mu
Ku
-po-
-mo-
-ko-
SWALI: Katika lugha ya Kiswahili, kirejeshi huchukua maumbo tofauti kutokana na ngeli husika. Thibitisha kwa mifano madhubuti.
Chanzo cha jedwali: Samson, 2016
Sharti lingine la ukunjiaji wa kishazi ni kuwa, sentensi hizo mbili zisiwe za ukanushi wala za ulinganisho. Hii ina maana kuwa sentensi za ukanushi na ulinganishi haziwezi kugeuzwa kuwa urejeshi au kiambajengo cha sentensi nyingine. Kwa mfano;
(a) Mwanafunzi hasomi kitabu
(b) Kitabu hakisomwi.
(c) Juma ni mrefu kuliko Asha
(d) Asha ni mfupi kuliko Juma
Katika mifano hiyo hata kama nomino zinarejelea kitu kilekile lakini kwa sababu ya uwepo wa ukanushi na ulinganisho katika sentesnsi hizo, urejeshi hauwezi kufanyika.
Hatua za kupitia katika kukamilisha mchakato wa urejeshi
Zipo hatua kadhaa za kupitia katika mchakato wa ukunjiaji wa kishazi kimoja ndani ya kishazi kingine.
(a) Shati ni zuri.
(b) Mwanafunzi alinunua shati.
Hatua ya kwanza: Upachikaji wa sentensi ya pili ndani ya KN cha sentensi ya kwanza
. Katika makala haya sentensi ya (b) Mwanafunzi alinunua shati inapachikwa ndani ya sentensi ya kwanza baada ya KN ambacho ni Shati. Maelezo haya yanaonyehwa hapa chini.
(a) Shati ni zuri
[Shati [Mwanafunzi alinunua shati] ni zuri]
(b) Mwanafunzi alinunua shati
Hatua ya pili: Udondoshaji wa KN kinachojirudia
Katika hatua hii, KN ambacho kinajirudia katika sentensi hiyo hakina budi kudondoshwa ili kuondoa uradidi. KN kinachodondoshwa ni kile cha kishazi bebwa au cha sentensi pachikwa kisha kupachika umbo husika kulingana na nomino husika mfano lo- hivyo umbo hilo huwekwa sehemu iliyodondoshwa nomino. Mfano wa sentensi hiyo ni;
[Shati [Mwanafunzi alinunua shati] ni zuri] [Shati [Mwanafunzi alinunua ] ni zuri]
Upachikaji wa umbo rejeshi la nomino uko wa aina tatu au ni wa mikakati mitatu.
Kuna wa kupachika kirejeshi
kabla ya mzizi (huonyesha ubainifu/huweka ubayana)
baada ya mzizi (haionyeshi njeo na huwa kama msemo)
baada ya umbo amba (huongeza taarifa ya ziada)
(a) [Shati [Mwanafunzi alinunua -lo-] ni zuri] (upachikaji wa umbo la nomino husika)
(b) [Shati [Mwanafunzi alinunua amba-lo] ni zuri]
Uhamishaji wa umbo rejeshi la nomino (uchopekaji wa umbo rejeshi ndani ya kitenzi)
(a) Shati [Mwanafunzi alinunua -lo-] ni zuri] [Shati [Mwanafunzi alilonunua] ni zuri]
(b) [Shati [Mwanafunzi alinunua lo] ni zuri] [Shati [Mwanafunzi alinunualo] ni zuri]
(c) [Shati [Mwanafunzi alinunua amba-lo] ni zuri] [Shati [Mwanafunzi alinunua amba-lo] ni zuri
Katika hatua hii, umbo rejeshi limewekwa katika mikakati yote.
Hatua ya nne: Kuhamisha vipashio au kupangua vipashio (ubadilishanaji nafasi vipashio)
Uhamishaji huo unahusu sentensi bebwa tu. Uhamishaji unahitajika hasa kwa kuwa kirejeshi ni sharti kiwe karibu na kisabiki chake na nomino mbili haziwezi kufuatana bila kiunganishi. Kisabiki cha kirejeshi kilichowekwa ni shati, hivyo mikakati yote hiyo ya urejeshi lazima ihamishwe kuelekea palipo na kisabiki chake. Mageuzi haya yanafanyika kwa kishazi bebwa tu.
(a) Shati [Mwanafunzi alilonunua] ni zuri] [Shati [alilonunua Mwanafunzi] ni zuri]
(b) [Shati [Mwanafunzi alinunualo] ni zuri] [Shati [alinunualo Mwanafunzi] ni zuri]
(c) [Shati [ Mwanafunzi alinunua ambalo] ni zuri] [Shati [ambalo Mwanafunzi alinunua] ni zuri]
Hatua ya tano: Kudondosha njeo
(i) Kudondosha Njeo
Mkakati wa urejeshi mwishoni mwa kitenzi kuwa hauhitaji kuwa na njeo ndani ya kitenzi, hivyo njeo ya wakati uliopita haina budi kudondoshwa.
(b) [Shati [alinunualo Mwanafunzi] ni zuri] [Shati [anunualo Mwanafunzi] ni zuri]
Hatua ya Sita: Kuondoa mabano
Katika hatua hii mabano ambayo yalikuwa yametumika kuunganisha vipashio sasa yanaondolewa ili kuona umbo la nje lilivyo kwa mikakati yote mitatu.
(a) [Shati [alilonunua Mwanafunzi] ni zuri] Shati alilonunua mwanafunzi ni zuri.
(b) [Shati [anunualo Mwanafunzi] ni zuri] Shati anunualo Mwanafunzi ni zuri.
(c) [Shati [ambalo Mwanafunzi amenunua] ni zuri] Shati ambalo mwanafunzi amenunua ni zuri
Vishazi rejeshi vinaweza kuwa bainifu au visiwe bainifu
Kishazi rejeshi bainifu ni vile ambavyo vinatoa taarifa zenye kulenga ubayana zaidi kama katika sentensi ifuatayo [Mwalimu [aliyefukuzwa kazi juzi] amefariki] katika mfano huo, aliyefukuzwa kazi juzi ni kishazi rejeshi bainifu kwa sababu kinaonyesha ubayana wa mwalimu hasa kwa kuwa kuna walimu wengi ila aliyefariki ni yule aliyefukuzwa kazi juzi. Urejeshi wa mwisho au mwanzo wa kitenzi huonyesha ubainifu.
Mfano Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania una theluji nyingi. Hapa inaonekana kuna milima mingi hivyo matumizi ya neno ulioko unaonyesha ubayana wa mlima kuwa uko Tanzania.
Urejeshi shadidifu ni ule unaobainisha kisabiki (neno kuu) kwa kukitofautisha (kutoa sifa za pekee) na vingine; huu ni ule ambao unatumia viambishi vya urejeshi. Zaidi huonyesha ubayana wa kisabiki. Hasa kama kuna kurejelea visabiki vingi. Mfano Mlima Kilimanjaro ulioko Tanzania una theluj nyingi.
Mke wangu aliyekuja jana anaumwa. Hapa ana wake wengi na urejeshi huo unalengo la kuonyesha ubayana wa kisabiki.
Kwa upande wa kishazi rejeshi ambacho si bainifu zaidi hutoa taarifa ya ziada. Sentensi ifuatayo inaonyesha mfano wa kishazi rejeshi mbacho si bainifu. Mlima Kilimanjaro ambao uko Tanzania una theluji nyingi. Matumizi ya umbo amba katika sentensi hiyo yanaonyesha taarifa ya uziada ya mlima kuwa uko Tanzania na si sehemu yoyote duniani.
Jambo la kuzingatia ni kuwa urejeshi unaowekwa kabla na baada ya mzizi wa neno huwa ni bainifu na ule unaotumia amba- huwa si bainifu bali hulenga kutoa taarifa za ziada.
urejeshaji usioshadidifu ni ule unaotoa taarifa zaidi kuhusu kisabiki lakini hautofautishi kisabiki hicho na kingine; huu ni ule unaotumia amba- na aghalabu huwa na mkato kabla na baada ya tungo rejeshi. Kishazi rejeshi kisicho bainifu na hasa hutumia amba.. mlima kilimanjaro ambao uko Tanzania una theluji nyingi. Hapa kuna taarifa za ziada kuhusu mlima Kilimanjaro.
Tabia za tungo rejeshi
i)
Huwa jirani na kisabiki
ii)
Hufungamana moja kwa moja na kisabiki. Kwa mfano ukibadilisha ngeli ya kisabiki na kiambishi cha urejeshi hubadilika
iii)
Huweza pia kufanya kazi au kushika nafasi ya mtenda, mtendwa au mtendewa
iv)
Katika lugha ya Kiswahili tungo rejeshi huweza kurejelea mtenda, mtendwa, yambiwa, mahali, hali (hali ilivyo), nk. Pia unaweza kubaini kile kinachoelezwa na kirejeshi kwa kungalia aina ya kirejeshi kilichotumika.
v)
Huweza kutumika hata kama kisabiki hakiko wazi
Mfano: Lisemwalo lipo
Dhima za tungo rejeshi
i)
Hutumika kufafanua zaidi kisabiki
ii)
Hutumika katika kutunga sentensi zenye uchamko (zisizo na kikomo)
Changamoto za ushushaji hadhi kipashio (kishazi rejeshi) kwa ujumla
Katika mchakato wa ushushaji hadhi kipashio ili kibebwe na kipashio kingine au kifanye kazi kama kiambajengo kingine, kuna changamoto kadha wa kadha zinazojitokeza. Changamoto hizi pia zinaelezwa vizuri na Mkude (2010). Baadhi ya changamoto mbalimbali za ushushaji hadhi kipashio ni pamoja na;
Vilevile changamoto nyingine inayojitokeza wakati wa kushusha hadi kipashio ni kusababisha utata wa tungo. Kwa mfano; Msichana aliyempiga kijana huyu ni yule. (nani anapigana?) hii ni sentensi tata iliyotokana na ukunjiaji wa kishazi kingine ndani ya kishazi kimoja. Sentensi hii kabla ya ukunjiano zilikuwa ni sentensi sahili ambazo hazina utata kama; Msichana alimpiga kijana yule na Msichana ni yule.
Baadhi ya virejeshi havionyeshi muda dhahiri na husababisha sentensi ya umbo la nje kuwa kama msemo. Hali hii zaidi hujitokeza kwa mkakati wa urejeshi wa baada ya mzizi au mwisho wa kitenzi. Hii imejionyesha kupitia sentensi tuliyoitumia ya Shati anunualo Mwanafunzi ni zuri. Sentensi hii haionyeshi ni wakati gani ambapo tendo la ununuaji linatendeka.
Ukunjiano unafanyika zaidi kwa sentensi sahili ambazo ni
Marejeo
Mekacha, R. (1987). Tungo Rejeshi katika Kiswahili katika Mulika Na. 10. Dar es Salaam: TUKI,
Uk. 83-91
Mkude, D. J. (2010). Uchambuzi wa Sentensi za Kiswahili Katika Makala ya Semina ya Kimataifa
ya Waandishi wa Kiswahili, 1/2010, 219-244.
___________(2010). Sentensi kama Kifaa cha Mwandishi Katika Makala ya Semina ya Kimataifa
ya Waandishi wa Kiswahili, 1/2010, 273-288.
Rubanza, Y. I. (2003). Sarufi: Mtazamo wa Kimuundo. Dar es Salaam: Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania
Samson, E. (2016). Muundo wa Vishazi Tegemezi Bebwa katika Kiswahili. Tasnifu ya Umahiri.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
. Mekacha, 1987: 83 katika Mulika Na. 19;
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com