KI 110: UTANGULIZI WA
ISIMUJAMII KATIKA KISWAHILI
1.1
Dhana
ya lugha
Lugha ni mfumo wa sauti
nasibu ambazo zimebuniwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao
(Massamba 2004:45). Jambo la msingi la
kuzingatia katika fasili hii ni kuelewa kwamba dhima kuu ya lugha katika jamii
ni kuwezesha mawasiliano miongoni mwa jamii yaweze kufanyika na kufanikiwa. Kwa
kutumia lugha inayofahamika na jamii mbalimbali, jamii moja inaweza kuwasiliana
na jamii nyingine ya mbali. Kufanikiwa kwa mawasiliano hupimwa na mzungumzaji
pale anapoona kuwa msikilizaji wake ameitikia na ametenda kama anavyotarajiwa.
Inapotokea msikilizaji akashindwa kuelewa au kutenda sawasawa na makusudio ya
mzungumzaji wake, mambo kadhaa yanaweza kuwa yamechangia. Yawezekana
mzungumzaji ametumia lahaja, lafudhi tofautitofauti, misimu au hata ametumia
lugha za kigeni ambazo hazifahamiki kwa wasikilizaji wake.
Wazungumzaji wa lugha
moja wanapoongezeka na kuwa wengi husababisha wakazi wake kutafuta maeneo
mengine mapya ya kuishi na kufanya maeneno ya wazungumzaji wake kupanuka. Inapotokea
wazungumzaji wa lugha hiyo watokao sehemu moja wanatamka baadhi ya maneno
tofauti na wazungumzaji wa lugha hiyohiyo watokao sehemu nyingine na bado
wazungumzaji hao wote wakaelewana, basi hatusemi kuwa watu hao wanazungumza
lugha tofauti, bali tunasema wanazungumza lahaja mbili tofauti.
Lahaja ni aina za lugha
ambazo kimsingi huchukuliwa kama lugha moja isipokuwa hutofautiana katika
baadhi ya vipengele fulani fulani kama lafudhi, fonolojia, na msamiati usiokuwa
wa msingi (Massamba 2001:190). Kwa mfano lugha ya Kiswahili ina lahaja nyingi kama
Kiunguja, Kimtang’ata, Kipemba, Kitumbatu, Chichifundi, Kivumba, Kingazija,
Kisiu na kadhalika,
1.2
Dhana
ya jamii na taifa
Jamii ni jumla ya mtu
mmoja mmoja ambao kwa pamoja huunda jamii yenye matabaka na makundi ya watu
mbalimbali (Mekacha 2000).
Matabaka na makundi ya
watu katika jamii hutokana na vigezo anuwai kama umri, jinsia, kipato, aina ya
kazi, viwango vya elimu, maeneo ya kuishi na kadhalika. Mekacha (2000) anaeleza
kuwa jamii ni dhana changamano.
1.3
Uhusiano
baina ya lugha na jamii
Lengo
la mwanaisimujamii ni kuchunguza na kufafanua uhusiano uliopo baina ya lugha na
wazunguzaji wake. Lengo hili linalenga kuifahamu jamii kwa kuchambua lugha ya
wazungumzaji wanayotumia. Kwa kuchambua lugha wanayotumia wazungumzaji,
tunawezakutambua yafuatayo:-
ü Kama
jamii ina dini au imani ipi?
ü Kujua
jamii inayotumia lugha fulani iko maeneo gani ya nchi?
ü Watu
wanaotumia lugha fulani wapo maeneo gani ya nchi?
ü Ni
wanaume au wanawake, vijana au wazee, wasomi au wasiowasomi? n.k
Kwa
kusikiliza mazungumzo ya watu mbalimbali utagundua kuwa kuna vibainishi vya
lugha vinavyoonesha aina ya watu wanaozungumza. Vibainishi hivyo vyaweza kuwa
vya kimofolojia, kifonolojia, kileksika n,k
Mfano
mzungumzaji akisema
1.
Umenunua wapi samaki nchanga?
2.
Mtoto amefika apa sa ngapi?
Kwa
kusikiliza matamshi katika sentensi ya kwanza utagundua kwamba mzungumzaji, ama
kutokana na athari za kifonolojia zitokanazo na lugha yake ya asili au kwa
sababu nyinginezo, ana mazoea ya kutamka baadhi ya maneno sanifu ya Kiswahili kulingana
na matamshi ya lugha yake ya kwanza. Badala
ya kutamka mchanga anatamka nchanga. Kwa mujibu wa jamii za
Tanzania, watu watu watamkao [nchanga] badala ya [mchanga] ni Wamakonde kutoka
mkoa wa Mtwara.
Tunaweza
pia kutambua aina ya wazunguzaji wenye imani au dini mbalimbali kwa kuchunguza
lugha ya mazungumzo inayotumika na wahusika wakuu.
3.
(a) Nataka mtoto wangu abatizwe jumapili ijayo, je inawezekana?
(b) Huyu mzee hakufunga Ramadhani kwa sababu alikuwa mgonjwa.
(c) Kila
mwaka baba huwa anakwenda kutambika
kwenye milima yao.
Kwa
kuzingatia mifano yetu katika (3), unaweza kugundua kuwa katika mfano wa 3
(a) mzungumzaji ni wa dini ya kikristo, wakati mzee
anayeongelewa katika 3 (b) ni wa dini ya
kiislamu. Katika mfano 3(c), baba
anayezungumziwa anaweza kuwa ni imani ya dini ya
jadi. Uteuzi ya maneno batiza, hakufunga ramadhani na tambika ni vibainishi ya kileskika.
MODULI YA
PILI
JAMIILUGHA
MBALIMBALI
2.1 Dhana ya jamiilugha mbalimbali
Wataalamu
mbalimbali wa isimujamii kama vile (Hymes, 1996, Gampez, 1972, Labov, 1972, na
Mekacha, 2000) wanakiri kwamba kufasili dhana ya jamiilugha siyo kazi rahisi
kutokana na ugumu wa kuweka mipaka ya maeneo ya matumizi ya lugha ya watumiaji
wake.
Wataalamu
wa isimujamii, hasa hao waliotajwaja wanakubaliana kuwa jamiilugha ni watumiaji
wa lugha wanaoishi katika eneo moja ambao hubainishwa na mahusiano yao ya
kuendelea kutumia aina fulani ya lugha tofauti na watumiaji wengine wa lugha
hiyohiyo.
Fasili
hii ya jamiilugha inaonekana ni rahisi kueleweka, kiutendaji fasili hii huzua
utata hasa katika kufanya uainishaji wa wazungumzaji na uchanganuzi wa data za
isimujamii. Wanaisimujamii wanachukulia
dhana ya jamiilugha kuwa inawakilisha eneo msingi la matumizi ya lugha. Kwa
maeneo mengine, jamiilugha ndio muktadha halisi wa kupatia taarifa zote muhimu
za wazungumzaji wa lugha ili zifanyiwe uchunguzi kwa lengo la kuzichanganua na
hatimaye kuzitolea ufafanuzi wa tofauti za matumizi na sababu zake.
Utata
wa maana ya jamiilugha unatokana na fasili yenyewe kutokuwa wazi hasa katika
mambo kadhaa yafuatayo:-
(a) Utata
unahusu eneo msingi la watumiaji wa lugha katika jamiilugha. Je, mipaka ya eneo
hili inaanzia wapi na kuishia wapi?
(b) Mipaka
ya eneo la jamiilugha inawekwaje bila ya kuingilia mipaka ya eneo jingine la
jamiilugha?
(c) Wazungumzaji
wa lugha waliomo ndani ya jamiilugha moja wanazungumza lugha ngapi? Wanatumia
lahaja, lugha sanifu, misimu, lafudhi au wanatumia lugha zote?
(d) Je,
tunatumia vigezo gani kuwatambua na kuwa ainisha watumiaji wa lugha waliomo
ndani ya jamiilugha moja kuwa hao ndio wanajamii wa jamiilugha hiyi? Kusema
kweli, maswali haya na mengine mengi ndiyo yanayofanya fasili ya jamiilugha
ionekane kuwa na utata zaidi hasa kinadharia na kiutendaji.
Ili
kuweza kuifahamu zaidi dhana ya jamiilugha lazima tuchunguze misingi mikuu
mitatu ifuatayo:-
(a)
Msingi
wa kutumia Lugha
Katika
mtazamo wa kiisimujamii, lugha ni msingi mmojawapo unaotumika kuitambulisha
jamii. Katika sehemu nyingi duniani, jamii mbali mbali za watu hubainishwa kwa
majina ya lugha zao. Kwa kufuata utaratibu huu tunaweza kupata majina ya lugha
zao za jamii zao. Kwa mfano tuna lugha ya Kigogo (Wagogo), Kihehe
(Wahehe), Kihaya (Wahaya), Ciruuri
(Waruuri), Kigweno (Wagweno)n.k Ieleweke kwamba si lazima pawe na uhusiano wa
moja kwa moja baina ya jina la lugha na jamiilugha inayotumia lugha hiyo. Nchi yenye jamiilugha moja, ndiyo huchukua
jina la lugha hiyo. Lakini nchi zenye
jamiilugha nyingi huwa hazichukui majina ya lugha zao. Kwa mfano, hakuna lugha
ya Kitanzania kutokana na jamii ya Watanzania, wala hakuna lugha ya Kikenya
wala Kizambia kutokana na jamii za Wakenya na Wazambia. Hii ni kutokana na kuwa
nchi zote zilizotajwa yaani Tanzania, Kenya na Zambia hazitokani na jamiilugha
moja.
(b)
Msingi wa
kutumia mahali
Huu
ni msingi wa kisosiolojia. Wanasosiolojia
wanaona kuwa watu ndio huunda jamiilugha moja, kimsingi watu hao hukaa
katika eneo moja lililo na mipaka ya kijiografia. Watu wote ambao hukaa katika
eneo la jamii lugha moja huongozwa na kanuni na taratibu zilizokubaliwa na
wanajamiilugha wenyewe. Kanuni na taratibu za jamii lugha hizo huzoeleka na
hatimaye kuhalalishwa na wanajamii wenyewe kuwa mila na desturi za jamiilugha
hizo. Jamii lugha hizi hutofautishwa na watu wa jamiilugha nyingine kwa kutumia
mipaka ya kijiografia ambayo kwa kawaida huwa ni mito mikubwa, milima
nakadhalika. Mipaka hii ya kijiografia huwekwa na wanajamii wenyewe na
huheshimiwa na vizazi vyote kwa kurithishana mipaka hiyo baina ya jamiilugha
moja na jamiilugha nyingine.
(c)
Misingi ya
Makubaliano ya Kimazoea
Msingi
huu unahusu jamiilugha ndogondogo ndani ya jamiilugha kubwa katika eneo husika.
Jamiilugha ndogondogo zaweza kuundwa na
wafanyakazi wa kampuni, shirika, wanafunzi, wanachuo, vijana wenye mtazamo
unaofanana wa kimaisha, kielimu, kibiashara n.k Kutokana na maelezo ya Gumperz
(1972:219) akifafanua jamiilugha za aina hii ni kwamba kuwepo kwa jamiilugha
hizi ndogondogo kunatokana na mazoea ya muda mrefu ya wanajamiilugha hao
kuishi na kushirikiana pamoja, sifa ambayo huwawezesha kuwa na
makubaliano yasiyo rasmi lakini yenye nguvu ya mazoea ya kutamka tofauti baadhi
ya fonimu au maneno katika lugha ambayo ndiyo hutumika kutambulisha jamiilugha
hizo kutoka jamiilugha nyingine. Kwa mfano, wafanyakazi wa bandarini toka
asubuhi hadi jioni wanashinda pamoja na kujulikana kama jamiilugha ya
wafanyakazi wa bandari ambao hujibainisha kwa utamkaji wa maneno uliotofauti na
jamiilugha nyingine. Aidha wafanyakazi huwa wanaporudi kwenye makazi yao ya
kuishi ya majirani ambayo nayo
hujibainisha kwa usemaji tofauti. Wafanyakazi hao hao wa bandari wakienda
msikitini au kanisani kusali hujikuta pia wamo katika jamiilugha nyingine ya
waumini n.k.
2.2 Jamiilugha zinazotumia lugha
moja
ü Jamiilugha
inayotumia lugha moja ni ile ile jamiilugha asilia ambayo haijawahi kutawaliwa
wala haijaingiliwa katika utawala wa kiserikali.
ü Katika
jamiilugha ya namna hiyo, lugha moja tu inayosemekana kuwa inatumika katika
maeneo yote ya matumizi ya lugha. Lugha hiyo inatumika katika maeneo rasmi ya
matumizi ya lugha kama vile katika shughuli za mahakama, elimu, utawala na
maeneo yasiyo rasmi ya matumizi ya lugha kama vile mawasiliano ya kawaida ya
ndani ya familia na miongoni mwa majirani.
ü Kadhalika,
wanajamiilugha wote wanadhaniwa kuwa wanaifahamu na kuitumia lugha hiyo katika
shughuli zao.
ü Katika
karne ya leo ya maingiliano na mawasiliano bora miongoni mwa jamii mbalimbali
duniani ni nadra sana kupata jamiilugha inayotumia lugha moja katika
mawasiliano yake. Hali hii inatokana na sababu mbalimbali kama vile uhamiaji,
biashara, utalii, elimu, dini, kuoleana na mawasiliano ya kimtandao.
ü Kwa
kutumia hasa mbinu ya mawasiliano ya kisasa ya Kiteknolojia ya Habari ya
Mawasiliano (TEHAMA), dunia iliyo na mataifa mengi yenye jamiilugha mbalimbali
sasa inaonekana kama kijiji. Dunia sasa imekuwa kama kijiji kwa sababu
mawasiliano baina ya jamiilugha ya taifa moja na jamiilugha za mataifa
mbalimbali yamerahisishwa kupitia radio, televisheni, simu za mikononi na hata
kwa njia za kielektroniki kupitia mifumo ya kompyuta.
ü Lugha
tofauti zinazotumiwa na jamiilugha mbalimbali katika mwasiliano miongoni mwao
wenyewe na nje ya mipaka ya matumizi ya jamiilugha hizo.
2.3 Jamiilugha uwili na Jamiilugha ulumbi
ü Jamiilugha
inayotumia lugha mbili huitwa jamiilugha uwili na jamiilugha inayotumia lugha
zaidi ya mbili huitwa jamiilugha ulumbi.
ü Jamii
hizi mbili yaani jamiilugha uwili na jamiilugha ulumbi zina sifa zinazofanana,
tofauti yake ni kwamba jamiilugha moja inatumia lugha mbili na nyingine
inatumia lugha zaidi ya mbili.
ü Jamiilugha
ulumbi ndizo jamiilugha zinazopatikana na kuenea sehemu nyingi katika nchi
mbalimbali. Kwa mfano Tanzania, Kenya, Uganda, Kanada na Zimbabwe. Kwa mfano
Tanzania hutumia lugha za jamii, Kiswahili, Kiingereza na lugha nyingine za
kigeni. Hii haina maana kwamba kila Mtanzania hutumia lugha hizo tatu au nne,
kinachosemwa hapa ni kwamba baadhi ya wanajamiilugha huzungumza lugha mbili,
tatu, nne n.k
Mambo yanayochangia kuwepo kwa jamiilugha Uwili na
jamiilugha Ulumbi
Wanaisimujamii
mbalimbali wakiwemo Coulmas (1997), Mekacha (2000), na wengineo wanataja sababu
kadhaa za msingi zinazichangia kuwepo kwa jamiilugha uwili na jamiilugha
ulumbi. Baadhi ya sababu walizotaja ni hizi zifuatazo:-
(a) Uhamiaji
(b) Ukoloni
(c) Biashara
(d) Dini
(e) Mipaka
ya kimataifa
(f) Elimu
(g) Lugha
kuenea kwa msaada wa dola
(h) Lugha
kuenea kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (kujifunza lugha ya
kigeni kupitia program ya kompyuta).
v Mambo
yanayochangia kuwepo kwa jamiilugha uwili na jamiilugha ulumbi hutofautiana
kutoka jamiilugha moja hadi jamiilugha nyingine. Ni kazi ya mwanaisimujamii kuchunguza
na kueleza sababu mahususi zinazochangia kuwepo kwa jamiilugha uwili na
jamiilugha ulumbi katika nchi mbalimbali.
v Katika
nchi yenye jamiilugha ulumbi wanajamii wake huwa hawana umahiri wa lugha yenye
repetwa inayofanana katika lugha wanayozungumza.
v Umahiri
ni uhodari wa mtu kuzungumza lugha vizuri kwa kiwango cha mzawa
wa lughahiyo.
v Repetwa
ni jumla ya usemaji wa mtu wa kuelewa lahaja, lafudhi na lugha mbalimbali kwa
kiwango cha kawaida cha kuelewana na mzungumzaji wa lugha hizo. Kwa mfano mtu
anaweza kuwa na repetwa ya kuzungumza lugha moja na lahaja zake, 77lugha mbili,
lugha tatu n.k. Tunasema mzungumzaji ana repetwa finyu kama mtu huyo
anazungumza lugha moja tu.
v Mtu
mwenye repetwa pana ni yule ambaye ana uwezo wa kuzungumza lugha nyingi na
wazungumzaji wa lugha hizo.
Matatizo ya jamiilugha ulumbi
v Ni
jambo la kawaida kwa taifa lenye jamiilugha ulumbi kuwa na matatizo mbalimbali yanayohusu lugha zinazotumiwa na wanajamii
lugha wake. Kimsingi yapo matatizo makuu mawili.
ü Tatizo
la kwanza linahusu uteuzi wa lugh ili kuchukua dhima mbalimbali za kitaifa.
Taifa lenye jamiilugha ulumbi hukabiliwa na tatizo la kuchagua lugha ya taifa,
lugha ya kufundishia katika mfumo wa elimu, lugha rasmi ya kuwasiliana na
mataifa ya nje nakadhalika.
·
Uamuzi wowote unaofanywa na serikali wa
kuchagua lugha fulani huchukua dhima ya kitaifa unapaswa uzingatie vigezo
muhimu ambavyo vitahakikisha kuwepo kwa
haki na fursa sawa kwa wanajamiilugha wote waliomo katika taifa hilo.
·
Pia serikali inapaswa kuzingatia
historia ya taifa husika, kuhakikisha kwamba umoja wa wanajamiilugha
unaimarishwa na kuepuka upendeleo wa aina yoyote na kuzingatia idadi kuwa ya
wazungumzaji wa lugha inayokusudiwa kuteuliwa.
·
Uteuzi wa lugha kuchukua dhima fulani
katika taifa unapaswa kufanywa kwa makini kwa kuhusisha wataalamu mbalimbali
wakiwemo wanasiasa, wanaelimu, wanahistoria, wanasosiolojia, wanaisimu na
makundi mengine muhimu katika jamii.
ü Tatizo
la pili ni kujenga umoja wa kitaifa. Jamiilugha zinazotumia lugha moja
ndizo kwa asili zina umoja,
mshikamano na utamaduni wenye nguvu.
·
Kujenga umoja wa kitaifa katika
jamiilugha siyo kazi rahisi kwa sababu kila jamiilugha ina umoja wake,
mshikamano na utamaduni wake unaokubalika na wanajamiiwake.
·
Tatizo la kujenga umoja wa kitaifa
linatokana na kuchanganywa kwa tamaduni tofauti za jamiilugha mbalimbali
zinazounda taifa hilo jipya.
·
Taifa jipya hukosa makubaliano ya pamoja
ya dhati kuhusu aina ya utamaduni unaofaa kufuatwa na lugha ipi itumike
kuziunganisha hizo jamiilugha ulumbi.
MODULI YA TATU
MATUMIZI YA LUGHA
3.1 Dhana ya matumizi ya lugha kwa
ujumla
ü Hii
ni dhana inayohusu muktadha halisi wa kijamii wa matumizi ya lugha. Muktadha
huo unatokana na kuhusisha shughuli zinazofanywa na jamii inayohusika, mada za
mazungumzo, mahusiano miongoni mwa wanaowasiliana na mahali yanapofanyika
mawasiliano hayo.
ü Mambo
hayo yanahusishwa kwa namna ambayo inawezekana kubainisha, kutofautisha na
kuhusisha mwenendo wa mtu binafsi wa matumizi ya lugha na utaratibu wa
jamiilugha wa matumizi ya lugha.
ü Kutokana
na mahusiano hayo inawezekana kusema kwa uhakika mkubwa kwamba katika jamiilugha
husika, lugha fulani kwa kawaida ndio hutumika katika mazungumzo ya eneo
fulani.
ü Kufahamu
ni lugha ipi inatazamiwa kutumika katika eneo gani la matumizi ya lugha ni kufahamu
mojawapo ya kanuni muhimu za kiisimujamii katika jamiilugha husika. Kuacha
kutumia lugha inayotazamiwa kutumika katika eneo fulani la matumizi ya lugha
katika mazungumzo kunadhaniwa na wanajamii kwamba ama kutokana na kutofahamu
kanuni za isimujamii za jamiilugha husika, au kuna ashiria mabadiliko katika
kanuni hizo au kutokana na msemaji kutaka kufikia malengo mahususi ya
kimawasiliano na kimahusiano.
Maeneo
hayo yanatofautiana kutoka jamiilugha moja hadi nyingine, lakini upo ufanano
katika jamiilugha nyingi katika baadhi ya maeneo hayo kama vile familia (ambapo
watu wanaoishi kwa pamoja katika familia moja wanawasiliana wakiwa nyumbani)
mtaani, kazini, serikalini,mashuleni, sokoni na kwenye shughuli za utamaduni.
Maeneo
ya matumizi ya lugha yanaweza kugawanywa katika makundi makubwa mawili
kutegemeana na jinsi yanavyohusiana na shughuli za kidola. Kuna maeneo rasmi na
maeneo yasiyo rasmi ya matumizi ya lugha. Maeneo rasmi ni yale ambayo matumizi
yake ya lugha kwa namna moja au nyingine yanaratibiwa au kuathiriwa moja kwa
moja na taratibu za dola. Miongoni mwa maeneo hayo ni kazini, elimu na mafunzo
na mahakamani. Maeneo yasiyorasmi ni yale ambayo hayaratibiwi au kuathiriwa
moja kwa moja na taratibu za kidola. Miongoni mwa maeneo hayo ni nyumbani na
miongoni mwa wanafamilia na maeneo ya makazi na miongoni mwa majirani. Haya ni
maeneo ambamo kwa kawaida hutumika lugha za kijamii. Kwa kawaida, maeneo rasmi
ya matumizi ya lugha huwa yenye hadhi na fahari kubwa zaidi ya maeneo
yasiyorasmi na matumizi ya lugha katika maeneo hayo hatimaye huchochea mabadiliko katika maeneo
yasiyorasmi ya matumizi ya lugha na kusababisha hatari ya lugha au vilugha
kutolewa.
3.2 Maeneo ya matumizi ya Kiswahili
Lugha ya Kiswahili ina
hadhi miongoni mwa Watanzania wa ngazi zote katika jamii. Watanzania takriban
wote wanahitaji na kuhitajika kutumia lugha hii katika maeneo yote yaliyo rasmi
isipokuwa mawasiliano ya kimataifa, elimu ya juu, kutunga sheria na mahakama za
juu. Maeneo mengine yoye ya matumizi ya lugha humuhusu na kumuhusisha karibu
kila mtu. Kwa kiasi fulani matumizi ya lugha ya Kiswahili yanawatambulisha
Watanzania wengi na jamii pana ya kitaifa. Hata hivyo, tathmini ya lugha hii
kuwa yenye ufahari ni kwa watu wa ngazi za chini. Watu wa ngazi hizo huiona
lugha hii kama kigezo cha kushiriki katika jamii pana na kama kigezo cha
kujiendeleza kijamii. Watu wa ngazi za juu wanaitambua lugha hii kama kigezo
cha kushiriki katika jamii pana na kama kigezo cha kushiriki katika maeneo
rasmi inamotumika. Lakini si wengi wao wenye kuithamini kuwa lugha yenye
ufahari mkubwa.
Lugha
nyingine zote za kijamii, ikiwa ni pamoja na vilugha vya Kiswahili vilivyo
lugha za kijamii, zina hadhi miongoni mwa watu wengi sana katika jamii. Watu
wengi wanazitumia lugha hizi katika mawasiliano yao mengi katika maeneo yasiyo
rasmi ya matumizi ya lugha, hasa vijijini na majumbani mwao katika familia zao.
Pia ni lugha ambazo matumizi yake yanawatambulisha watu wa jamii zao za
kikabila na fasihi na utamaduni unaoambatana na jamii zao.
Lugha ya Kiswahili inaweza kutumika katika
maeneo mbalimbali kama haya yafuatayo:-
(a)
Majumbani na
miongoni mwa wanafamilia
Hili
ni eneo lisilo rasmi la matumizii ya lugha. Katika eneo hili taratibu za
matumizi ya lugha haziamuliwi moja kwa moja na matumizi ya lugha, bali mfumo wa
mahusiano ya kijamii. Watafiti wengi wameripoti kwamba kwa jumla na kwa kawaida
mawasiliano yanayofanyika majumbani miongoni mwa wanafamilia moja, ndugu na
marafiki wa karibu hufanyika kwa lugha za kijamii (Abdulazizi Mkilifi, 1972;
Brauner na wenzake, 1978, Rubagumya 1991, Mekacha 1993, Ngonyani, 1994 na
wengineo). Takwimu zinaonesha kwamba hadi hivi sasa bado asilimia kati ya 75 na
80 ya Watanzania wote wanaishi vijijini na wanategemea ukulima wa kujikimu. Kwa
hiyo, kwa Watanzania wengi, lugha za kijamii ndiyo kwa kawaida zinatazamiwa
kutumika majumbani na katika familia. Kutawala kwa matumizi ya lugha hizo
katika eneo hilo kutokana na siyo tu mahitaji ya kimawasiliano, yana haja ya
watu kuwasiliana kwa lugha wanayoifahamu vyema zaidi, bali pia ukweli kwamba
lugha za kijamii zimefungamana na utamaduni na maisha ya jamii hizo na ni
kigezo kimojawapo cha kuzitambulisha.
Katika
ripoti za utafiti za hivi karibuni, inaoneshwa kwamba hata huko vijijini kuna
matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mazungumzo ya watu wa familia moja
majumbani, hasa kwa watu wenye umri mdogo. Kwa hiyo, ingawa majumbani na
miongoni mwa watu wa familia moja, matumizi ya lugha za kijamii ndiyo
yanatawala, huko vijijini kuna ushahidi kwamba matumizi ya lugha ya Kiswahili,
hasa miongoni mwa watu wenye umri mdogo, yanaanza kubadilika kuwa ya kawaida (Mekacha,
1993; Ngonyani, 1994, Yoneda, katika Hino 1996; Msanjila, 1996). Hata hivyo
matumizi ya lugha ya Kiswahili majumbani na miongoni mwa wanafamilia ni makubwa
zaidi mijini kuliko vijijini. Hii inatokana hasa na ukweli kwamba mijini
familia za watu wa kutoka jamii tofauti huishi karibu karibu. Hali hiyo hufanya
matumizi ya lugha ya Kiswahili kutawala kote isipokuwa baina ya wanafamilia
ndani ya nyumba yao tu.
(b)
Katika maeneo ya
makazi miongoni mwa majirani
Katika
maeneo ya makazi miongoni mwa majirani, matumizi ya lugha si tofauti sana na
kama ilivyo majumbani na miongoni mwa wanafamilia katika maeneo ya vijijini.
Ingawa kuna ushahidi kwamba kuna matumizi kidogo ya Kiswahili, vijijini
matumizi yanayotawala katika maeneo ya makazi na mingoni mwa majirani ni lugha
za kijamii. Hii ni kwa sababu hasa kwamba wengi wa majirani huwa ni watu wa
jamii ileile na ambao pia wanazungumza lugha hiyo hiyo ya kijamii. Kadhalika,
ingawa hutokea yakasikika matumizi kidogo ya lugha za kijamii miongoni mwa
majirani walio wasomi, mijini maongezi yanayotawala katika maeneo ya makazi na
miongoni mwa majirani ni Kiswahili. Hii inatikokana hasa na ukwel kwamba mijini
watu wa kutoka jamii tofauti huishi wakiwa majirani na hivyo kuhitaji lugha ya
mawasiliano mapana kuwasiliana, lugha ambayo kwa Tanzania ni Kiswahili. Pia
inatokana na hadhi na ufahari wa lugha ya Kiswahili ikilinganishwa na lugha za
kijamii ambapo matumizi ya lugha za kijamii yanafungamanishwa na ukabila wakati
matumizi ya Kiswahili yanafungamanishwa na maendeleo, usasa na hisia za utaifa.
(c)
Katika masoko na
biashara za ndani ya nchi
Kadhalika,
katika masoko na biashara za ndani ya nchi, tofauti kubwa katika matumizi ya
lugha ni baina ya mjini na vijijini. Mijini matumizi ya lugha ya Kiswahili
yanatawala karibu kwa namna ile ile yanavyotawala katika maeneo ya makazi na
miongoni mwa majirani, hata hivyo katika masoko na biashara za ndani mijini
hakuna matumizi ya lugha za kijamii, na kama yapo ni kidogo mno kiasi kwamba
hayatazamiwi na si ya kawaida. Vijijini, katika masoko na biashara za ndani
matumizi ya lugha za kijamii ni makubwa zaidi na ambavyo kwa kiasi fulani
yanatazamiwa. Hata hivyo kuna matumizi makubwa pia ya lugha ya Kiswahili katika
masoko na biashara za ndani kuliko ilivyo majumbani na miongoni mwa wanafamilia
na katika makazi na miongoni mwa majirani.
(d)
Sehemu za kazi
Wengi
wa watu vijijini hujishughulisha na kazi za ukulima, ufugaji na uvuvi wakati
wengi wa watu wa mijini hujishughulisha na kazi za maofisini, viwandani, huduma
na biashara. Kazi za watu wa vijijini hufanywa katika familia au kwa
ushirikiano na majirani, lakini nyingi za kazi za mijini hufanywa kwa
ushirikisha watu wasio na familia wala
majirani. Huku vijijini watu wanaoshirikiana aghalabu huwa wa jamii moja na
huwa wazungumzaji wa lugha moja ya kijamii wakati mijini watu wanaoshirikiana katika
kazi aghalabu huwa kutoka jamii tofauti. Kazi nyingi vijijini ni eneo lisilo
rasmi la matumizi ya lugha wakati kazi nyingi mijini ni eneo rasmi la matumizi
ya lugha. Kwa sababu hiyo, kwa jumla
matumizi ya lugha katika meneo ya kazi hutofautiana baina ya miji na vijiji,
ambapo vijijini matumizi ya lugha za kijamii hutawala na mijini matumizi ya
lugha ya Kiswahili hutawala.
(e)
Katika
usafiri wa umma
Katika usafiri wa umma,
kwa kawaida hukutana na watu ambao hawafahamiani. Kadhalika usafiri wa umma ni
eneo la umma kwa maana kwamba watu wanahusiana kulingana na taratibu za umma na
wala sio kutokana na undugu, urafiki au ujirani. Kutokana na kuwa eneo la umma,
usafiri wa umma hufuata sana ratatibu za matumizi ya lugha sawa na maeneo
rasmi. Kwa sababu hizo, lugha inayotawala katika matumizi katika eneo hilo huwa
lugha ya umma, bila kujali kama ni vijijini au mijini. Katika Tanzania lugha ni
Kiswahili. Kwa hiyo, nchini Tanzania matumizi ya lugha ya Kiswahili ndiyo
yanayotawala katika usafiri wa umma.
(f)
Katika shughuli
za michezo na burudani
Shughuli
za michezo na burudani zinazofanywa ni nyingi na zinatofautiana kutoka mahali
pamoja hadi pengine na kutoka tabaka la watu hadi wengine. Baadhi ya shughuli
za michezo na burudani ambazo hufanywa katika mukatdha usio rasmi. Hata hivyo
tofauti muhimu ya matumizi ya lugha katika eneo hili ni baina ya vijiji na
miji. Mijini shughuli za michezo na burudani hutawaliwa na matumizi ya
Kiswahili wakati vijijini shughuli hizo hutawaliwa na matumizi ya lugha za
kijamii.
(g)
Katika
mfumo wa elimu na mafunzo
Matumizi ya lugha
katika mfumo wa elimu na mafunzo ni eneo rasmi la matumizi ya lugha. Nchini
Tanzania, hili ni eneo ambalo limepata kutafitiwa na kujadiliwa kwa kina na kwa
mapana, pengine kuliko maeneo mengine yote ya matumizi ya lugha. Hii ni kwa
sababu sera ya lugha nchini Tanzania imeruhusu hasa matumizi ya lugha katika
mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu na mafunzo nchini Tanzania una ngazi kuu tatu,
elimu na mafunzo ya msingi, elimu na mafunzo ya sekondari na elimu na mafunzo
ya juu. Kulingana na sera ya lugha inayoendelea kutekelezwa nchini hadi hivi
sasa elimu ya watu wazima, elimu ya msingi na mafunzo ya ngazi za chini (yaani yanayowalenga watu wa vijijini
na ambao elimu yao ni msingi) inapaswa kutolewa kwa lugha ya Kiswahili. Elimu ya
kuanzia ngazi ya sekondari na mafunzo mengine yanayotolewa kwa watu waliohitimu
masomo ya ngazi ya sekondari na kuendelea yanatakiwa kutolewa kwa Kiingereza.
(h)
Katika
utawala na siasa
Utawala na siasa ni
eneo rasmi la matumizi ya lugha kutokana na ukweli kwamba shughuli za utawala
ni za kiserikali na shughuli za kisiasa huambatana kwa karibu sana na zile za
kiserikali. Kwa sababu hiyo matumizi ya lugha katika eneo hilo kwa kiasi
kikubwa hutawaliwa na miongozo, kanuni na taratibu zinazoamuliwa na dola.
Shughuli za kiserikali za kiutawala na zile za kisiasa ni zenye mamlaka katika
jamii na hufanywa na watu wenye madaraka. Kwa sababu hiyo, lugha inayotakiwa
kutumika katika maeneo hayo inatakiwa kuwa lugha yenye mamlaka na ambayo
inapendwa na watu wenye madaraka na lugha ambayo ina ufahari katika jamii.
Katika eneo hili kinatawaliwa na matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza.
Lugha za kijamii hazina nafasi na kama zinatumika ni kwa kiwango kidogo sana katika
ngazi za chini kabisa za utawala, ambapo zikitumika ni kwa sababu maalumu.
Lugha ya Kiswahili ndiyo inatawala kwa kiasi kikubwa matumizi ya lugha katika
eneo hili katika ngazi zote. Matumizi ya lugha ya Kiingereza yanatawala katika
baadhi ya shughuli za ngazi za juu kabisa na siasa.
(i)
Katika
ibada na shughuli za kidini
Nchini Tanzania wapo
watu wanaofanya ibada kwa kufuata madhehebu mbalimbali ya dini ya kikristu,
wapo wanaofanya ibada kwa kufuata madhehebu mbalimbali ya dini ya kiislamu,
wapo wanaofanya ibada kwa mijibu wa dini za kiasili za jamii zao na pia wapo
watu ambaohawafanyi ibada zozote kwa kuwa hawaamini katika kuwapo kwa mungu.
Kuenea kwa dini za kigeni katika nchi ya Tanzania kulisaidia sana katika kuenea
kwa lugha ya Kiswahili kutokana na ukweli kwamba kwa jumla dini hizo zilienezwa
kwa lugha ya Kiswahili, ingawa taratibu za matumizi ya lugha zilitofautiana
kutoka dini moja hadi nyingine. Baada ya kupatikana kwa uhuru, hata hivyo na
hata baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha shughuli nyingi za dini hizo
zilitawaliwa na matumizi ya lugha ya Kiswahili. Hata hivi sasa matumizi ya
lugha ya Kiswahili ndiyo yanayotawala katika ibada ya shughuli nyingine za dini
hizo.
(j)
Katika
mfumo wa sheria na mahakama
Matumizi ya lugha
katika mahakama na mfumo wa sheria ni mojawapo ya mambo yanayoelezwa na sera ya
lugha nchini. Kulingana na sera hiyo, Kiswahili ndiyo lugha inayotakiwa
kutumika katika ngazi za chini za mahakama. Lugha ya Kiswahili ndio hutumika
katika kusikiliza mashauri katika mahakama za mwanzo na kumbukumbu za mashauri
hayo huandikwa kwa Kiswahili. Hata hivyo hapana shaka kwamba katika ngazi hii,
hasa huko vijijini kuna matumizi kidogo ya lugha za kijamii katika uendeshaji
wa mashauri. Sera ya lugha inazitaka mahakama za hakimu mkazi kuendesha mashauri
kwa lugha ya Kiingereza, ingawa matumizi ya lugha ya Kiswahili yanaruhusiwa
pia. Hata hivyo, mashauri mengi yanaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na lugha ya
Kiingereza hutumika tu pale panapokuwa na malumbano ya kisheria miongoni mwa
mawakili, waendesha mashtaka na mahakimu.
Maeneo mengine ambamo
Kiswahili hutumika ni kama vile katika mawasiliano na maandishi, katika
uandishi na usomaji wa kazi za fasihi na katika vyombo vya habari.
3.3 Sosiolojia ya lugha
Sosiolojia
ni taaluma inayoshughulikia uchunguzi na uchanganuzi wa matabaka na makundi ya watu
katika jamii. Mifano ya matabaka na makundi ya watu katika jamii ni kama vile:-
(a) Matabaka
ya watu wa kipato cha juu, watu wa kipato cha kati, na watu wa kipato cha
chini, pina kuna matabaka ya watawala na watawaliwa.
(b) Kuna
makundi ya wafanyabiashara, wafanyakazi, wakulima, wasomi, wanafunzi, wazee,
vijana, wanawake n.k
Matabaka na makundi
haya ya watu, kwa kawaida huwa yanatumia aina ya lugha inayoelekea kufanana, na
inayotofautisha matabaka na makundi mengine ya watu katika jamii.
Sosiolojia ya lugha
inatakiwa ihusike na uchambuzi na ufafanuzi wa muundo wa jamii, hususani kama
unavyojidhihirisha kutokana na tofauti katika matumizi ya lugha. Lengo ni kujua
jamii na kuchambua lugha na ni kipengele kimojawapo miongoni mwa vipengele
vingi vya kusaidia kufikia lengo hilo. Kwa mtazamo huo sosiolojia ya lugha
inakuwa tawi la au mada ya sosiolojia na kila kipengele kinachochambuliwa
hufanywa hivyo kwa nia ya kuchangia katika kuielewa jamii au
Kwa nia ya kuboresha
nadharia za (sosiolojia) za kijamii. Vipengele hivyo, kwa maoni ya Trugdill
(1983) ni kama vile ulumbi, yaani
hali ya kutumika kwa lugha mbili au zaidi katika jamiilugha moja; diglosia, yaani hali ya lugha mbili
zinatumika katika jamiilugha moja kugawana uamilifu, hadhi na fahari; kubadili msimbo; yaani matumizi ya
lugha mbili tofauti katika mazungumzo hayo hayo; kupanga sera ya lugha;
mwelekeo kuhusu lugha, lugha katika elimu, na masuala mengine yote
yanayohusiana na kufafanua nani anasema lugha gani na nani.
MODULI YA NNE
TOFAUTI ZA MATUMIZI YA LUGHA
4.4
Tofauti za kiisimu na kilahaja
4.2
Tofauti za kijamii na kitamaduni
4.3 Tofauti za
lugha za Pijini, Krioli na lugha nyingine
Pijini
na Krioli ni dhana ambazo zinapaswa kufafanuliwa kwa pamoja kwa sababu kuwepo
kwa Krioli kunategemea kuwepo kwa Pijini.
Kwa mujibu wa De Camp (1971) na Hall (1972), Pijini ni lugha yenye mfumo
uliorahisishwa sana ambao hutumiwa na wazungumzaji wenye lugha tofauti katika
mazingira maalumu baina yao na kwamba Pijini siyo lugha mama kwa mzungumzaji
yeyote.
Mazingira
maalumu huwa ndio kichocheo cha kuzuka kwa lugha za pijini. Kihistoria,
mazingira maalumu ni kama vile:-
ü yale
yaliyotokea kwenye mashamba makubwa ya miwa, pamba n.k
ü katika
mazingira ya misafara ya watumwa iliyotokea zamani kwenye karne ya 15 na
kuendelea.
ü Mazingira
ya kwenye machimbo ya migodi mbalimbali
ü Mazingira ya kuwa ndani ya meli kubwa kwa siku
nyingi
ü Makambi
mbali mbali ya kijeshi, ya wakoloni yaliyokuwa na wanajeshi mchanganyiko kutoka
mataifa mbali mbali.
Mazingira
haya maalumu tuliyoyataja hapa ni matukio halisi ya kihistoria ambayo yalitokea
katika karne ya 15.
Kwa
mujibu wa De Camp (keshatajwa) na Hall (keshatajwa), Krioli ni lugha mama
zinazotumiwa na wazungumzaji wazawa ambao kihistoria wametokana na jamiilugha
ya pijini.
v Lugha
za Pijini na Krioli hutofautiana na lugha nyingine kutokana na sifa za msingi
zifuatazo:-
ü Kwa
asili ni lugha chotara.
Asili ya lugha za
Pijini na Krioli ni mazingira maalumu ya mchanganyiko au mwingiliano wa
jamiilugha mbalimbali zisizokuwa na uhusiano wa karibu na makundi ya lugha za
jamii hizo. Jamiilugha hizo hujikuta zikiishi pamoja kwa muda mrefu katika
mazingira maalumu ya kibiashara au ya kufanya kazi mbalimbali. Kuzuka kwa lugha
hizi za Pijini na Krioli, miongoni mwa wanajamiilugha hao ni matokeo ya kukosa
lugha nyingine inayofahamika kwa wanajamiilugha hao, ambayo ingeweza kutumika
kwa mawasiliano baina yao. Lugha nyingi za Pijini zina asili ya lugha za Ulaya
lakini pia kuna chache zilizo na asili ya lugha za Afrika na Asia. Hali hii
imetokana na nchi nyingi za Afrika na Asia kutawaliwa na wakoloni wa kutoka
ulaya. Ukichunguza kwa makini misamiati ya lugha za Pijini na Krioli utagundua
kuwa idadi kubwa ya misamiati hiyo imetokana na lugha ya Kiingereza, Kifaransa,
Kireno, Kihispania, Kijerumani n.k
Mbali na kuwepo kwa
Pijini na Krioli zenye asili ya lugha za ulaya, ziko pia zenye asili ya lugha
za Afrika na Asia. Kwa mfano, huko New Guinea, kwa mfano, kuna Pijini
inayojulikana kama Melanesian Pidgin
English (MPE) Hii ni Pijini yenye asili ya Afrika iliyotumiwa na watawala
wa Kijerumani katika karne ya 20 kama lugha ya kufundishia mafunzo ya polisi
kwa vijana wa New Guinea.
ü Zina
mfumo wa lugha sahili
Mfumo wa lugha ulio
sahili ni ule ambao sarufi yake ni sahili pia. Ni mfumo wa lugha unaotumia
maneno machache sana kwa madhumuni ya mawasiliano sahili ili kukidhi haja ya
wazungumzaji walioko katika mazingira maalumu. Kimsingi misamiati mingi ya
miundo ya lugha hizi huwa haitokani na lugha mama za wazungumzaji wa Pijini na
Krioli, bali kwa kiasi kikubwa, hutokana na lugha za kigeni zenye hadhi ya juu
na kiasi kidogo sana cha msamiati wa kutokana na lugha zao za asili. Hata
hivyo, jambo la msingi la kukumbuka hapa kuhusu msamiati wa lugha ni kwamba
maneno mengi ya Pijini na Krioli huwa yana maana nyingi za kikoa kimoja kutoka
lugha chasili au lugha nyingine ili kuweza kukidhi mahitaji ya mwasiliano ya
wazungumzaji wake. Mifano ifuatayo inadhihirisha hoja hiyo:-
4.
Neno spit kutoka Pijini ya Chinese Pidgin English CPE lina maana
ya:
(a) kutema
(b) kutapika
5.
Neno gras
kutoka Pijini ya MPE lina maana ya:
(a) Kitu chochote kinachoota
ardhini
(b) Kitu chochote kinachoota
mwilini n.k
6. Neno anner la Pijini
inayojulikana kama Russenorsk iliyokuwa
ikizungumzwa na jamii ya Wa- Norway na Warusi katika karne ya 19 lilikuwa na
maana ya
(a) – a pili
(b) – a kufuata
Kwa kuzingatia hoja ya neno kuwa na
maana nyingi za kikoa, neno gras lina maana za majani, mimea, nywele, ndevu, na manyoya.
ü Hutumika
zaidi katika mawasiliano yasiyo rasmi
Kihistoria, lugha za Pijini na
Krioli zinajulikana kuwa ni lugha
zinazotumikwa kwa mawasiliano
ambayo ni sahili na kwa sababu hii hutumika zaidi katika mawasiliano yasiyo
rasmi, lugha nyingi za Pijini na Krioli hazikusanifiwa. Mfano mwingine wa
Pijini yenye asili ya Afrika na Asia ni Pijini inayojulikana kama fanakalo inayotumika Afrika kusini.
MODULI YA TANO
MAWANDA
YA ISIMUJAMII
5.1 Malengo ya
isimujamii
Isimujamii ina
malengo makubwa matatu yafuatayo:-
(a) Kuchunguza
tofauti za wazungumzaji wa lugha katika jamii.
Wanaisimujamii
hufanya uchunguzi na kufafanua tofauti zilizopo za watumiaji wa lugha katika
jamii na kueleza tofauti hizo za wazungumzaji husababishwa na nini. Kuelewa
lugha ya jamii kunaendana na kuielewa jamii yenyewe ikiwa ni pamoja na
kuyaelewa matabaka na makundi mbalimbali yaliyomo ndani ya jamii hiyo. Jamii
imeundwa na matabaka na makundi mbalimbali ya watu. Kuna matabaka ya watawala
na watawaliwa, wakulima na wasiowakulima, wafanyakazi wa kuajiriwa na
wasiowakuajiriwa, waliosoma na wasiosoma, wafanyabiashara na wasio
wafanyabiashara n.k. Pia kuna makundi ya vijana, wazee, wanawake, wanaume,
wanafunzi, wanachuo, wanamichezo n.k. Ukichunguza kwa makini utabaini kuwa kila
tabaka au kundi la watu katika jamii hutumia lugha inayotambulisha tabaka au
kundi hilo. Kuchunguza na kufafanua tofauti za wazungumzaji wa lugha katika
jamii kunasaidia watumiaji wa lugha kufahamu watumie lugha ipi katika mazingira
rasmi na yasiyo rasmi miongoni mwa wanajamii wenyewe. Lugha rasmi ni ile lugha
iliyokubalika na kutangazwa na chombo chenye mamlaka ili lugha hiyo itumike
katika shughuli za serikali, bunge, mahakama, elimu nakadhalika. Pia umuhimu
mwingine wa kuchunguza tofauti za wazungumzaji wa lugha ni kusaidia
wazungumzaji kufahamu namna bora ya kutumia lugha katika mawasiliano ya jamii
baina ya wazungumzaji na msikilizaji.
(b) Kufanya uchunguzi na kufafanua uhusiano uliopo
baina ya lugha na wazungumzaji wake. Lengo hili pia linalenga kuifahamu jamii
kwa kuchambua lugha ya wazungumzaji wanayoitumia. Kwa kuchambua lugha wanayoitumia
wazungumzaji, tunaweza kuitambua jamii inayohusika kama ina dini ua imani ipi,
iko maeneo gani ya nchi (pwani, bara, kusini/kaskazini n.k), watu wake
wanafanya kazi gani, wanaume au wanawake, vijana au wazee, wasomi au
wasiowasomi n.k
(c) Kuangalia
uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine
Mwanaisimujamii
anapaswa kuchunguza na kutolea ufafanuzi uhusiano uliopo baina ya lugha moja na
lugha nyingine zinazotumika. Katika jamii au taifa kuna lugha zaidi ya moja
zinazotumiwa na watu. Nchini Tanzania, kwa mfano, kuna lugha zaidi ya 120
zinazotumiwa na watu mbalimbali. Kidhima lugha hizi zimegawanywa katika makundi
matatu. Lugha ya Kiingereza, lugha ya Kiswahili na lugha za kijamii. Ni kazi ya
mwanaisimu kufanya uchunguzi na ufafanuzi wa mambo ya msingi yanayohusu
uhusiano wa lugha hizi na wazungumzaji wake kwa kuzingatia mahitaji ya jamii ya
wakati huo.
5.3 Isimujamii ya mawandafinyu
Huu
ni makabala wa kiisimu unaozingatia lengo la kwanza na la pili la isimujamii
katika uchunguzi na uchanganuzi wake. Ni makabala unaochunguza uhusiano wa
tofauti za wazungumzaji wa lugha na kubainisha vitambulisho vya usemaji au
utamkaji wa wazungumzaji au wazungumzaji ili kuhusisha na kundi la aina ya watu
au matabaka ndani ya jamii. Mwanaisimu Labov (1972) katika utafiti wake
alioufanya katika jiji la New York, Marekani ameonyesha kuwa, watu wa tabaka la
chini hutamka sauti [r] kwa mkwaruzo zaidi katika maneno yenye fonimu /r/
kuliko watu wa matabaka mengine (tabaka la juu). Trughdill (1874), katika
uchunguzi alioufanya nchini Uingereza, ameonyesha kuwa mbali na kuwepo kwa
lahaja la kijiografia, pia kuna lahaja za kijamii yaani zinazoonyesha hadhi
mbalimbali za watumiaji wa lugha ya Kiingereza. Kwa maneno mengine Trudgill
anaeleza kwamba unaweza kupata lahaja za wazungumzaji wa hadhi ya juu na lahaja
za wazungumzaji wa hadhi ya chini.
5.4 Isimujamii ya mawandamapana
Huu
ni mkabala unaozingatia lengo la tatu la isimujamii ambalo linachunguza na
kufafanua uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine zinazotumika katika jamii.
Kwa mujibuwa mkabala huu, mambo yanayozingatiwa ni yale yote yanahohusu
utumiaji wa lugha kwa jumla. Kujua lugha zilizopo katika jamii na uhusiano wake
kidhima na lugha nyingine ni moja ya mambo ya msingi ya mkabala huu. Kwa mfano
mwanaisimujamii katika mkabala huu, hupenda kujua sababu za msingi zinazofanya
lugha moja iteuliwe kuwa lugha ya taifa, lugha rasmi au lugha ya kufundis hia
katika mfumo wa elimu. Sababu zinazotumika kuteua lugha kuwa na dhima kitaifa
mara nyingi huwa hazina budi zitokane na sababu za msingi za kiisimu na
kijamii. Kimsingi, hata zile lugha ambazo haziteuliwi kuchukua dhima yoyote
kitaifa bado kwa mujibu wa mkabala huu, ni muhimu lugha hizo kufanyiwa
uchunguzi ili kuona hali halisi ilivyo, kwa lengo la kutaka kujua hatma ya
lugha hizo, hasa kule zinakotumika na pia kutaka kujua maendeleo ya lugha hizo
ili kuweza kutoa mapendekezo ya nini kifanyike. Uhusiano huu wa lugha
mbalimbali katika jamii hutegemea sana sera ya lugha ya nchi husika. Mkabala
huu huhusisha watu wengi kijiografia. Mathalani, mkabala huu unaweza kuhusisha
wazungumzaji wa nchi moja, nchi zilizoungana, jumuia ya nchi kadhaa, kanda za
nchi mbalimbali na hata huweza kuhusisha wazungumzaji wa bara zima. Kimsingi,
mkabala huu wa mawanda mapana ni mkabala ambao kusema ukweli, uchunguzi wake
unalenga kutatua matatizo mbambali yahusuyo utumiaji wa lugha kitaifa na
kimataifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com