Anayetia sahihi hapa chini anathibitisha kuwa amesoma
Tasnifu hii iitwayo Ulinganishi wa
Nafasi ya Mwanaume na Mwanamke katika Fasihi: Mfano kutoka Riwaya ya Janga Sugu la Wazawa, na kupendekeza
ikubaliwe na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha Digrii ya
B.A Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
……………………………………
Mwl.
Neema Sway
( Msimamizi )
…………………………………..
Mwl.
George Kitundu
( msimamizi )
Tarehe…………………………………
IKIRARI
Mimi Manyama
Sylivery, ninathibitisha kuwa Tasnifu hii ni kazi yangu halisi na haijawahi
kuwasilishwa na haitawasilishwa katika Chuo Kikuu kingine chochote kwa minajili
ya kutunukiwa Digrii hii au nyingine yoyote ile.
Sahihi…………………………………..
SHUKURANI
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu
mwingi wa rehema kwa kukamilisha kazi hii ya Utafiti pamoja naa changamoto
mbalimbali zilizokuwepo. Pia napenda kuwashukuru wazazi na walezi wangu kwa kuweza kunilea na kunisomesha kuanzia elimu ya msingi hadi
kufikia elimu ya chuo kikuu Mungu awazidishie Baraka na neema tele katika
maisha yao.
Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipo washukuru walimu wangu
walionisaidia katika kufanikisha utafiti huu ambao ni Mwalimu Neema Sway na
George Kitundu ambao wamekuwa msaada mkubwa kwangu kwa ushauri na mawazo ili kuweza kufanikisha
utafiti huu. Mawazo na ushauri wao yamesababisha kuweza kujua na kufahamu mambo
mengi yanayohusu utafiti.
Nawashukuru pia wanafunzi wenzangu wa B.A
in Kiswahili kwani wamekuwa na mchango mkubwa kwangu katika mchakato mzima wa utafiti, tumekuwa
pamoja tukishauriana jinsi ya kuweza kufanikisha utafiti na kwa ufanisi
Mwisho napenda kutoa shukrani zangu za
dhati kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuweza kunichagua kuwa moja ya
wanafunzi wake.
Kazi hii ninaitabaruku kwa wanafunzi wote wanaosoma Lugha ya
Kiswahili kwani kupitia kazi hii itasaidia kupata elimu kuhusu mambo mbalimbali
yaliyomo kwenye kazi hii. Pia napenda kuitabaruku kazi hii wanajamii wote kwani
kwa kiasi kikubwa kazi hii imeangazia mambo yaliyopo kwenye jamii.,
Utafiti huu unahusu Ulinganishi kati ya nafasi ya mwanaume
na mwanamke katika fasihi: Mfano kutoka riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Katika utafiti huu mtafiti alitumia
usampulishaji lengwa na kutumia sampuli lengwa ambayo ni kitabu. Mtafiti
alichunguza ufanano na utofauti kati ya nafasi ya mwanaume na mwanamke katika
fasihi, katika uchunguzi huu mtafiti alitumia mbinu ya maktabani katika
ukusanyaji wa data na kutumia njia ya maelezo katika uchambuzi wa data. Utafiti
huu una malengo mahususi mawili ambayo ni kubainisha ufanano kati ya nafasi ya
mwanaume na mwanamke katika fasihi na kubainisha utofauti kati ya nafasi ya
mwanaume na mwanamke katika fasihi. Malengo hayo yalisaidia kujibu maswali ya
utafiti katika utafiti huu.
Utafiti huu ulibaini kuwa kuna ufanano
mkubwa kati ya nafasi ya mwanamke na mwanaume kuliko utofauti wao, na uwepo wa
usawa kati ya jinsi hizi mbili husaidia kuleta maendeleo kwenye jamii.
Mwisho utafiti huu unapendekeza
watafiti wengine wa tafiti zijazo wajikite pia katika kuangalia nafasi ya
mwanaume katika fasihi na jamii kwa ujumla kwani watafiti waliowengi wamejikita
kwa mwanamke tu.
Utafiti huu unahusu ulinganishi wa nafasi ya mwanaume na
mwanamke katika fasihi kupitia riwaya ya Janga
Sugu la Wazawa. Nafasi ya mwanamke na mwanaume katika fasihi imeoongelewa
kwa marefu na mapana na wataalamu mbalimbali, mathalani kwenye jamii zetu majukumu
mbalimbali hugawanywa kutokana na jinsia. Utafiti huu umegawanywa katika sehemu
mbalimbali ambazo ni utangulizi wa jumla, mapitio ya maandiko, mbinu za
utafiti, uchambuzi wa data, mapendekezo na hitimisho.
Ruhumbika (2002) anaelezea kuhusu maswala mbalimbali
yanayoikumba jamii kupitia riwaya yake ya Janga
Sugu la Wazawa ambapo wahusika wanawake na wanaume wamehusika kuiwakilisha
jamii kuhusu mambo mbalimbali. Ameangazia nafasi ya mwanamke katika jamii na
kumpa mwanamke nafasi kubwa katika riwaya hii na kusahau nafasi ya mwanaume.
Senkoro (2011) anafafanua kuwa riwaya ilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi
ya kiutamaduni, uchangamano wa maisha ya kijamii, kisiasa na kiuchumi yaliyopelekea
haja ya kimaudhui zaidi ya ngano na hadithi fupi. Anaendelea kusema kuwa riwaya
za kwanza zilitafsiriwa toka riwaya za kizungu mpaka za Kiswahili na riwaya
mojawapo ni ile ya James Mbotela ya Uhuru
wa Watumwa. Pia anaeleza kuwa riwaya ni utanzu uliozuka kutokana na hali
mahususi za kijamii, ilizuka kutokana na maendeleo na mageuzi ya kiutamaaduni
na viwanda. Suala la ukoloni na uvumbuzi pia liliumba hali ambazo zilihitaji
kuelezwa kwa mawanda mapana zaidi.
Kupanuka kwa usomaji hasa wakati wa vipindi vya mapinduzi ya
viwanda huko ndipo walipoibuka wasomaji hasa wanawake waliobaki majumbani
wakati waume zao walipokwenda viwandani kufanya kazi. Kupitia historia hiyo
inasaidia kujua mambo mbalimbali ambayo huweza kuzungumziwa na riwaya ambayo
kwa kiasi kikubwa yanaihusu jamii.
Kwa mujibu wa Nyerere (2009) anaeleza kuwa wanaume na
wanawake wana utofauti kuwa wao ni wanawake na wanaume ni wanaume. Wanawake
wana sauti ndogo zaidi, kuwa na maziwa makubwa zaidi, kutokuwa na ndevu na mara
nyingi huwa ni wazuri zaidi, udogo wao na hukua upesi zaidi kuliko wanaume na
kwa kawaida huanza kuonesha maisha ya utu uzima kuliko wanaume wenye umri
uleule. Kumekuwa na fikra mbalimbali kwenye jamii kuhusu wanawake na wanaume
mfano wanaume wanaona kuwa wanawake wakiruhusiwa kuhukumu katika mahakama
wataharibika na wanaume hawatapata haki zao kutokana na wanawake kuongoza.
Anafafanua kuwa tabia hii haiwezi kuwepo iwapo mwanamke na mwanaume ni wamoja
na wana umoja na ili wanawake na wanaume kuwa na umoja wapewe elimu sawa bila
ya kubagua jinsia. Wanawake na wanaume katika jamii huwa na majukumu tofauti,
mfano mume hutoa amri na wanawake hutii lakini mwanamke kutoa ushauri kwa mwanaume
ni jambo la aibu kwenye jamii nyingi.
Victoria (1999) anaeleza kuwa ubinafsi kati ya wanaume na
wanawake ni tatizo kubwa kwenye jamii ubinafsi unaosahau kwamba maendeleo ya
jamii nzima yanatokana na ushirikiano wa kikamilifu baina ya wanaume na
wanawake. Katika nyanja mbalimbali wanaume ndio hutawala lakini wanawake
wanaotawala ni wale wanaotoka kwenye familia au koo za watawala, japokuwa
wanawake wanaweza kutimiza kazi kubwa kwa ufundi wa maarifa mengi kazi ambayo
mwanaume mwenye akili angeweza kutimiza.
Lakini wanaume hujiona kuwa ndio wenye uwezo mkubwa kuliko
wanawake na katika jamii nyingi wanaume husadikika kuwa ndio wenye akili nyingi
kuliko wanawake. Senkoro (1982) anaeleza historia ya mwanamke na mwanaume
katika jamii kuwa jamii imegawanyika katika matabaka mbalimbali, mgawanyiko huo
umeleta matabaka kwenye jamii na kupelekea wanawake kuwa tegemezi kwa wanaume
ingawa kuna wanaume ambao pia ni tegemezi kwa wanawake.
Kutokana na mifumo
mbalimbali kwenye jamii nafasi ya mwanamke na mwanaume inatofautiana sana
kutokana na mila na desturi zilizopo kwenye jamii mbalimbali. Tafiti nyingi
kuhusu masuala ya nafasi ya mwanaume na mwanamke katika jamii zimeangaziwa au
kuegemea upande mmoja. Watafiti wengi wameegemea katika kuangalia nafasi ya
mwanamke tu kwenye jamii bila ya kuangalia nafasi ya mwanaume kwenye jamii
jambo ambalo sio sahihi kwa kuangalia upande mmoja tu, mathalani wataalamu walioangalia
upande mmoja wa mwanamke tu ni Victoria (1999), Senkoro (1982). Kwa hali hiyo
iko haja ya kuangazia pande zote mbili, utafiti huu utaangazia pande zote mbili
kwa kuchunguza ulinganishi wa nafasi ya mwanaume na mwanamke katika fasihi
kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa.
Kumekuwa na harakati nyingi zinazoendelea kuhusu mwanaume na
mwanamke katika jamii. Hata hivyo harakati hizo zinaonekana kutozaa matunda
kutokana na dhana zilizopo kutoka enzi na enzi kuhusu majukumu na nafasi ya
mwanaume na mwanamke kwenye jamii mbalimbali. Katika jamii nyingi wanaume
huonekana kuwa ndio kila kitu kwenye familia huku mwanamke kama ua au pambo
katika familia. Harakati hizo zinaonekana kujitokeza hata kwa waandishi
mbalimbali wa vitabu ambao nao ni sehemu ya jamii. Waandishi na watafiti wengi
wamezungumzia sana upande wa mwanamke na kusahau upande wa mwanaume. Tafiti
zilizokwishafanywa hazijakamilika kikamilifu juu ya ulinganishi wa nafasi ya mwanamke
na mwanaume katika fasihi. Hivyo utafiti huu unalenga kuchunguza ulinganishi
kati ya nafasi ya mwanaume na mwanamke katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Hivyo
Katika utafiti huu Mtafiti ameyagawa malengo katika sehemu
mbili, lengo kuu na malengo mahususi.
Lengo kuu la utafiti ni kuchunguza ulinganishi wa nafasi ya
mwanaume na mwanamke katika fasihi
Utafiti huu una malengo mahususi matatu ambayo ni;
i. Kubainisha nafasi ya mwanaume na mwanamke inayojitokeza
katika fasihi kupitia riwaya ya Janga
Sugu la Wazawa.
ii. Kubainisha ufanano wa nafasi ya mwanaume na mwanamke
inayojitokeza katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa.
iii. Kubainisha utofauti kati ya nafasi ya mwanaume na
mwanamke inayojitokeza katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa.
1.5 Maswali ya Utafiti
i. Je mwanaume na mwanamke wana nafasi gani zinazojitokeza
katika fasihi kupitia riwaya ya Janga
Sugu la Wazawa?
ii. Je kuna ufanano gani kati ya nafasi ya mwanamke na
mwanaume unaojitokeza katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa?
iii. Je kuna utofauti gani kati ya nafasi ya mwanaume na
mwanamke unaojitokeza katika fasihi kupiti riwaya ya Janga Sugu la Wazawa?
Utafiti huu utasaidia kuielimisha jamii kuhusu masuala ya
kinjinsia kati ya nafasi ya mwanamke na mwanaume kwenye jamii bila kuegemea
upande wowote, kuonesha ufanano na
tofauti kati ya nafasi ya mwanaume na mwanamke kwenye jamii. Utafiti huu utasaidia
kuondoa dhana ya mila na desturi zilizopo ambazo huegemea upande moja kati ya
mwanamke na mwanaume kwenye jamii kupitia Riwaya ya Janga Sugu la wazawa.
Utafiti huu umejikita kuchunguza ulinganishi uliopo kati ya
nafasi ya mwanamke na mwanaume katika fasihi kupitia riwaya ya Janga
Sugu La Wazawa. Nafasi ya mwanaume na mwanamke imezungumiwa katika
machapisho mbalimbali lakini utafiti huu utajikita zaidi kwenye riwaya tu, hii
ni kutoka na mda wa utafiti kuwa mdogo hivyo mda huu hautoshi kuangazia katika
aina nyingine za fasihi andishi.
1.8 Hitimisho
Sura hii imeeleza utangulizi wa jumla kuhusu Utafiti, Tatizo
la Utafiti, Usuli wa Tatizo, Malengo ya Utafiti, Umuhimu wa Utafiti, Mawanda ya
Utafiti na Maswali ya Utafiti. Sura ya pili inajadili kwa kina Mapitio ya
Vitabu mbalimbali na Machapisho mbalimbali.
SURA
YA PILI
2.1
Utangulizi
Katika sura hii Maandiko mbalimbali yamepitiwa yanayohusu
mwanaume na mwanamke kuhusu nafasi zao
na majukumu yao kwenye jamii. Utafiti huu unachunguza ulinganishi wa nafasi ya
mwanaume na mwanamke kwenye jamii kwa kutumia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Sura hii imepitia maandiko mbalimbali yaliyoandikwa
na wataalamu mbalimbali katika tafiti zao. Yafuatayo ni mapitio mbalimbali.
Nkwera (1978) anasema riwaya ni hadithi iliyo ndefu kuweza
kutosha kufanya kitabu kimoja au zaidi. Ni hadithi ya kubuniwa iliyojengwa juu ya
tukio la kihistoria na kuandikwa kwa kwa mtindo wa ushairi iendayo mfululizo
kwa kinaganaga katika kuelezea maisha ya mtu au watu na hata taifa, anaendelea
kusema kuwa riwaya ina muhusika mmoja au hata wawili.
Mulokozi (1996) anaeleza kuwa chimbuko la riwaya ya
Kiswahili lipo katika mambo makuu mawili ambayo ni fani za kijadi na fasihi
pamoja mazingira ya kijamii. Mulokozi anaeleza kuwa riwaya haizuki hivihivi
bali ilitokana na fani za masimulizi yaani hadithi na ndipo zikapatwa kuigwa na
watunzi wa riwaya wa mwanzo. Fani hizo zilizopata kuchipuza riwaya za mwanzo ni
kama vile riwaya za kingano. Hivyo inaonesha kuwa ili kujua maana ya riwaya ni
vyema kuzingatia mambo kadhaa ambayo ndiyo ya msingi na mambo hayo ni; lazima riwaya
iwe na lugha ya kinathari, isawiri maisha ya jamii, iwe na masimulizi ya kubuni
na visa virefu, wahusika zaidi ya mmoja, iwe na mpangilio wa msuko na matukio
na ifungamane na wakati yaani visa na matukio lazima viendane na matukio.
Riwaya ya Kiswahili
ni ile inafungamana na utamaduni wa jamii ya Waswahili katika lugha ya
Kiswahili ambao hupatikana katika nchi ya Afrika mashariki na huwahusu Waswahili
wenyewe. Muhando na Balisidya (1997) wanasema riwaya ni kazi ya kubuni, ni
hadithi ambayo hutungwa kufuatana na
uwezo wa fanani kuibusha mambo kutokana na mazoea au mazingira yake,
wanaendelea kusema kuwa riwaya yaweza kuanzia maneno 35000 na kuendelea.
Ruhumbika, (2002) ndiye mwandishi wa Riwaya ya Janga Sugu la Wazawa, ni riwaya ambayo imeandikwa na inahusu mambo mbalimbali
yaliyoko kwenye jamii. Mwandishi amewatumia wahusika wa kiume na wahusika wa
kike kufikisha ujumbe kwenye jamii. Katika riwaya hii mwandishi kaonesha jinsi
wanaume na wanawake wanavyotimiza majukumu mbalimbali. Wamitila (2003) anasema
riwaya ni kazi ya kinathari au kibunilizi ambayo huwa na urefu wa kutosha,
msuko uliojengeka vizuri, wahusika wengi walioendelezwa kwa kina yenye kuchukua
muda mwingi katika mandalizi na kuhusisha mandhari maalumu.
Madumulla (2009) anaeleza kuwa riwaya ilitokana na nathari
bunifu simulizi kama vile hadithi, hekaya na ngano inayosimuliwa kwa mdomo.
Anaendelea kusema kuwa fasihi ilitokana na mazumgumzo ya fanani ya ushairi na
tendi za Kiswahili katika hati za kiarabu kwa sababu ndio maandishi yaliyotamba
katika pwani ya afrika mashariki. Kwa ujumla riwaya ni kazi ya fasihi andishi
ambayo kwa kawaida ni ndefu kuliko hadithi fupi yenye wahusika wengi na msuko
wa matukio mengi na msuko huo umejengeka vizuri na mada zake ni nzito na pana
kiasi.
2.3 Nafasi ya Mwanamke na Mwanaume
Victoria (1997) anafafanu kuwa nafasi ya mwanaume na
mwanamke imegawanyika kutokana na mambo kama vile ubinafsi, na mila na desturi.
Anaeleza na kutoa pendekezo kuwa kikwazo kikubwa katika matatizo ya kijamii ni
ubinafsi baina ya wanawake na wanaume, ubinafsi huo sio mzuri kwani katika
kuleta maendeleo ya jamii nzima mwanamke na mwanaume wanatakiwa kuwa na umoja
na ushirikiano mzuri. Hali ya kuwepo kwa ubinafsi na utengano kati ya mwanaume
na mwanamke hurudisha maendeleo nyuma. Mtaalamu huyu amejikita katika kuangazia
mgawanyiko uliuopo kati ya nafasi ya mwanamke na mwanaume na kusahau kuangazia
ufanano wao na tofauti zao, hivyo utafiti huu utaangazia ulinganishi wa nafasi
ya mwanaume na mwanamke kwani mtaalamu huyu kajikita katika kuangalia sababu
zinazopelekea utengano kati ya mwanaume na mwanamke na kusahau jinsi
wanavyofanana na kutofautiana.
Chaligha (2011) alitafiti kuhusu mgawanyo wa majukumu katika
Fasihi ya picha ya katuni mnato za Kiswahili na kuona kuwa mgawanyo wa majukumu
kwenye jamii mbalimbali kati ya mwanamke na mwanaume hauko sawa kwani wanawake
kwa kiasi kikubwa ndio hupewa majukumu mengi na mazito kwenye jamii zao.
Mtaalam huyu alijikita zaidi kuangazia mgawanyo wa majukumu kati ya mwanaume na
mwanamke kwenye jamii na hajaangazia ufanano na tofauti zilizopo kati ya
mwanaume na mwanamke katika kutimiza majukumu mbalimbali. Utafiti huu
utaangazia ulinganishi wa nafasi ya mwanaume na mwanamke katika jamii.
Biblia hufundisha kikamilifu usawa kati ya mwanaume na
mwanamke wakati wa uumbaji na ukombozi. Biblia inafundisha kwamba mwanamke na
mwanaume wote waliumbwa kwa mfano na sura ya mungu walikuwa na ushirika na
walishirikiana pamoja katika majukumu ya uzazi na malezi ya watoto na kutawala
dunia na vyote vilivyoumbwa. Inafundisha kuwa mwanamke na mwanaume waliumbwa
katika utimilifu na usawa, katika kushirikiana na kuumbwa kwa mwanamke
kunatokana na mwanaume na hii ni ishara inayoonesha umoja na usawa wa binadamu
wote. Inafundisha pia wanaume na wanawake wote ni warithi wa neema ya uzima na
wameunganishwa katika uhusiano kwa kuonesha unyenyekevu na uwaibikaji pamoja,
pia baba na mama kwa pamoja wanatakiwa kuongoza au kounesha njia katika malezi,
nidhamu na mafundisho ya watoto wao. Mwanaume na mwanamke wanatakiwa kuridhiana
kutafuta, kutimiza matamanio na matarajio na malengo ya kila mmoja.
Mwanaume au mwanamke hawatakiwi kutafuta kumtawala mwenzake
bali kila mmoja awe kama mtumwa kwa mwenzake, wakati wa msuguano wa kimaamuzi
wanatakiwa kutafuta suluhisho kwa kufuata utaratibu maalumu. Utambulisho kwa
wanawake na wanaume wanaotoa huduma na uongozi ufanyike kwa wote bila kutoa
upendeleo wa kinjinsia. Kupanuka kwa usomaji hasa wakati wa vipindi vya
mapinduzi ya viwanda huko ndipo walipoibuka wasomaji hasa wanawake waliobaki
majumbani wakati waume zao walipokwenda viwandani kufanya kazi.
Katika mapitio ya machapisho mbalimbali kuhusu nafasi ya
mwanaume na mwanamke katika fasihi, wataalamu wengi wamejikita katika
kumuelezea mwanamke zaidi na kumsahau mwanaume. Kazi nyingi za fasihi huusisha
wahusika wanaume na wanawake lakini kwenye suala la nafasi zao katika jamii
waandishi waliowengi wameonesha nafasi ya mwanamke tu. Pia hata katika jamii
zetu nafasi ya mwanamke ndio inayopewa kipaumbele zaidi mfano kuna siku ya
wanawake inayoadhimishwa kila mwaka lakini hakuna siku ya wanaume
inayoadhimishwa kila mwaka. Machapisho machache mno yameangalia nafasi ya
mwanaume na mwanamke hivyo utafiti huu utaangalia ulinganishi kati ya nafasi ya
mwanaume na mwanamke katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa
Katika sura hii tafiti na mapitio mbalimbali yaliyoandikwa
kuhusu masuala ya nafasi ya mwanaume na mwanamke kwenye jamii zimeegemea upande
mmoja kwa kuelezea nafasi ya mwanamke na kuonesha jinsi gani mwanamke
anavyogandamizwa, lakini tafiti hizo hazikuangazia nafasi ya mwanaume kwenye
jamii na hazikuonesha ulinganifu uliopo kati ya mwanaume na mwanamke kwenye
jamii na imebainika kuwa ulinganifu wa nafasi ya mwanaume na mwanamke
haujazungumziwa vya kutosha. Hivyo utafiti huu utaangazia ulinganishi wa nafasi
ya mwanaume na mwanamke kwenye jamii.
Sura hii inazungumzia mbinu mbalimbali zitakazotumika katika
utafiti huu. Mambo yatakayo jadiliwa katika sura hii ni eneo la utafiti,
sampuli na usampulishaji, njia au mbinu za kukusanya data, vifaa vya kukusanya
data na mkabala wa kukusanya data.
Eneo la utafiti huu ni katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam katika maktaba ya Taasisi ya Taaluma ya Kiswahili.
Maktaba hii imesaidia upatikanaji wa riwaya ya Janga Sugu la Wazawa, pia imesaidia upatikanaji wa data mbalimbali
kuhusu mambo mabalimbali yanayohusu wanaume na wanawake kama vile vitabu,
machapisho na tasnifu mbalimbali.
Usampulishaji ni
tendo linalofanywa kwa kuchagua washiriki wawakilishi wanaotoka katika kundi
kubwa. Pia Sampuli hurejelea sehemu ya idadi ya watu au vitu ambavyo mtafiti
anatumia kukusanya data ambazo zitamsaidia katika utafiti wake. Mtafiti
ametumia sampuli na usampulishaji kama ifuatavyo;
Kuna mbinu kadhaa zinazotumika katika usampulishaji. Katika
utafiti huu mtafiti ametumia usampulishaji lengwa. Mtafiti kawatumia muhusika
mwanaume na mwanamke katika riwaya ya Janga
Sugu la Wazawa kama wawakilishi wa kundi kubwa la watu.
3.3.2 Sampuli
Katika utafiti huu aina ya sampuli iliyotumika ni sampuli
lengwa ambayo ni kitabu cha Janga Sugu la
Wazawa. Sababu ya kuchagua sampuli lengwa ni kuwakilisha kundi kubwa. Utafiti huu umetumia
riwaya ya Janga Sugu la Wazawa kama sampuli lengwa na sababu ya
kutumia riwaya hii ni kutokana na kuwa na wahusika wanaume na wanawake
wanaotimiza majukumu mbalimbali kwenye jamii.
Katika utafiti huu njia iliyotumika katika kukusanya data ni
njia ya maktabani. Mbinu hii ilitumika katika kusoma na kupitia machapisho
yanayohusiana na mada ili kuweza kupata data za msingi. Sababu iliyochangia
kutumia mbinu hii ni kutokana na data nyingi kupatikana kwenye maktaba kama
vile vitabu, tasnifu na makala
mbalimbali.
Katika utafiti huu vifaa mbalimbali vimetumika kwa ajili ya
kukusanya data. Vifaa vilivyotumika ni kama vile daftari, kalamu, Kinyonyi na
kompyuta. Vifaa hivi vimetumika kama ifuatavyo;
Katika utafiti huu mtafiti ametumia daftari katika kunuu
data nbalimbali. Daftari limesaidia katika kuhifadhi data za awali za mtafiti.
3.5.2 Kinyonyi
Hiki ni kifaa kitumikacho kuchukua na kuweka vitu mbalimbali
kwenye komputa pia huwa na uwezo wa kuhifadhi baadhi ya vitu kulingana na uwezo
wake. Mtafiti ametumia kifaa hiki katika kuweka data zake kwenye komputa. Kifaa
hiki kimesaidia kuhifadhi pia data za mtafiti
Ni kifaa chenye wino kinachotumika katika uandishi. Mtafiti
ametumia kalamu katika kuandikia data kwenye daftari alipokuwa maktabani
akikusanya data. Kalamu imemsaidia mtafiti katika uandishi wa data.
Mtafiti ametumia komputa katika kuandika kazi yake ya
utafiti na pia komputa imetumika kama kifaa cha kuhifadhi kadhi ya mtafiti.
Hivyo kompyuta imesaidia kuandika kazi ya utafiti na kuhifadhi kazi ya mtafiti.
Katika utafiti huu data zimechambuliwa kwa kutumia mkabala
wa maelezo. Mkabala wa maelezo huusisha data zilizo katika mfumo wa maelezo.
Mkabala huu umesaidia kunukuu data zilizo maktabani kwani data zilizo maktabani
ni data za kimaelezo. Mkabala wa maelezo umesaidia kupitia na kunukuu maelezo
mbalimbali yaliyoandikwa na wataalamu mbalimbali kuhusu ulinganishi wa nafasi
ya mwanamke na mwanaume kwenye jamii.
3.7 Hitimisho
Katika sura hii ya mbinu za utafiti mambo mbalimbali
yamejadiliwa kama vile kujua eneo la utafiti, Sampuli na Usampulishaji, mbinu
za kukusanya data, vifaa vya utafiti na mbinu za uchambuzi wa data.
SURA
YA NNE
Sura hii inahusu uwasilishaji wa data na uchambuzi wake kwa
ujumla. Sura hii inawakilisha matokeo ya data kuhusu ulinganishi wa nafasi ya
mwanaume na mwanamke katika fasihi. Uwasilishaji wa data na uchambuzi wake
umeongozwa na malengo ya utafiti na maswali ya utafiti na uchambuzi wa
data umefanywa kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Riwaya hii
inaongelea mambo mbalimbali ikitumia wahusika wanaume na wanawake katika
kufikisha ujumbe. Riwaya hii imegusa mambo mbalimbali kama vile uongozi, mila
na desturi, matabaka, na malezi.
Riwaya ya Janga Sugu
la Wazawa ilichapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2002 na kampuni ya E& D
limited, Dar es Salaam. Riwaya hii imegawanywa katika sehemu kuu kumi ambazo zinaelezea matukio mbalimbali.
Riwaya hii iliandikwa na Gabriel Ruhumbika na imejikita katika kuelezea maisha
ya familia ya mzee Ninwalo ambaye ni moja ya muhusika mkuu.
Katika riwaya hii mwandishi ameonesha jinsi matatizo
yanavyoikumba familia ya mzee Ninwalo na wanae na jinsi wanavyojitahidi
kutafuta suluhisho la matatizo hayo. Mwandishi amegusa Nyanja mbalimbali katika
riwaya hii kama vile kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Mwandishi amemtumia pia
muhusika Bugonoka kama muhusika mkuu na kuonesha jinsi anavyokabiriana na
changamoto mbalimbali. Mwandishi kawatumia wahusika wanawake na wanaume katika
kufikisha ujumbe kwa jamii.
Lengo la kwanza la utafiti huu ni kubainisha nafasi ya
nwanaume na mwanmke inayojitokeza katika fasihi. Hivyo kwa kutumia mbinu ya
maktabani na kuweza kusoma riwaya hiyo teule data mbalimbali zilipatikana
kuhusu nafasi ya mwanaume na mwanamke inayojitokeza katika fasihi na kuweza
kuchambuliwa kama ifuatavyo;
Katika riwaya hii mwandishi anamuonesha Mzee Ninwalo kama
mwanaume mwenye mapenzi ya dhati kwa watoto wake. Mzee Ninwalo alikuwa
akiwapenda watoto wake na kuwalea kwa usawa, pia kutokana na upendo wake
aliwafundisha wanae kazi mbalimbali kama vile kuvua samaki. Mwandishi anasema;
“Ninwalo alikuwa anawapenda
sana watoto wake wote, wakubwa kwa wadogo.
Hapo nyumbani kwake
watoto wote, wale wa kuwazaa pamoja na wajuu zake na
watoto wa ndugu zake na
wale wa ndugu za mke wake na ndugu za wake wa
wanawe, ambao wa nyumbani
wote walikuwa ni wanawe. Ulikuwa wajibu wake
kuonesha kwamba
aliwapenda na kuwatendea wote sawa” ( Uk 6 )
Hivyo katika jamii zetu kuna wanaume ambao wana mapenzi ya
dhati kwenye familia zao kwa kuwapenda watoto wao na ndugu zao kwa ujumla.
Wanaume wengi wamekuwa na mchango mkubwa kwenye familia zao.
4.3.2 Mwanaume Anaoneshwa kama Mtu Msomi
Riwaya hii inamuonesha Mazula kama mwanaume msomi mwenye
elimu ya juu. Mazula alikuwa analelewa na Bugonoka baada ya mama yake mzazi
kufariki, hivyo baada ya kuamia nchi mpya mlezi wake aliamua kumpeleka shule na
ndiye mtoto wa kwanza kwenye ukoo wa mzee Ninwalo kwenda shule. Mwandishi
anasema;
“Mabula alipomaliza masomo yake Makelele, Nchi ilikuwa ikingojea kwa
hamu
Wananchi wachache waliohitimu masomo yao
Makerere ili iwagawie kazi katika
juhudi zake za kupata watalamu wazalendo.
Mabula na shahada yake katika
Hisabati akachagua kufanya kazi katika idara
ya uhasibu ya serikali” ( Uk 106 )
Hivyo mwandishi anatuonesha kuwa katika jamii zetu kuna
wanaume ambao ni wasomi. Katika jamii mbalimbali wanaume ndio wamekuwa mstari
wa mbele kwenye elimu ukilinganisha na wanawake.
Mwandishi amemuonesha Padre John kama mwanaume mwenye tama ya ngono. Alitaka kulala Bugonoka
lakini akakataliwa. Mwandishi anaonesha jinsi maisha ya Padre John yalivyokuwa
pale anaposema;
“ Padre John alikuwa
anaishi kwenye nyumba kubwa ya ghorofa kwenye milima
Iganzo
ukingoni mwa Ziwa Victoria, nje kidogo y mji wa Mwanz. Humo
ndimo alimokuwa akiishi na wake zake wanne,
ambao alikuwa akiwatliki na
kuoa na kubadili
vionjo. Aliwaambi wasaidizi wake hata vitamu kiasi gani
ukila kila siku vitakukinai” ( Uk 121 )
Katika jamii wanaume wamekuwa na tamaa ambazo sio za msingi,
wanaume wengi walio oa wamekuwa wakitamani wanawake wa nje ya ndoa zao na
kupelekea familia nyingi kuvunjika. Pai Mapdri wamekuwa wakikiuka sheria za
kanisa za kutojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na wanawake, wengi wamekuwa
na wanawake na wengine kuoa na kuzaa watoto kitu ambacho ni kinyume na sheria
za kanisa.
Katika riwaya hii mwandishi anamuonesha maimuna kama
mwanamke tajiri na anayemiliki mali nyingi. Maimuna alikuwa mtoto wa pekee wa
mfanyabiashara mashuhuri wa sehemu ya Medina hapo jijini Dakar, mwandishi
anasema;
“Maimuna
alirithi mali ya baba yake yote ikiwa ni pamoja na maduka manne
makubwa hapo medina,
alikuwa na magari hapo kwake, pickup na malori
ya biashara zake
pamoja na gari ndogo za kutembelea. Alipo zeeka aliamua kula
mali yake hasa akawa
anapika couscous na pilau na ubwabwa kwa samaki
mkavu na mbichi” ( Uk 131 )
Mwandishi anatuonesha kuwa katika jamii zetu kuna wanawake
ambao ni matajiri na wanamiliki vitu vingi vyenye thamani. Baadhi ya wanawake
katika jamii zetu wamekuwa chachu ya maendeleo kutokana na shughuli
wanazozifanya.
Mwandishi amemuonesha Bugonoka kama mwanamke mwenye msimamo baada
ya kukataa kufanya mapenzi na Padre John. Bugonoka alikataa kulala na Padri
John hata pale alipolazimishwa kwa nguvu. Katika maisha ya Bugonoka hakuna
mwanaume aliyewahi kujaribu kumchezea tangu azaliwe na aliamua kutoolewa baada
ya kuanza kumlea Mazula. Hivyo Bugonoka hakutaka kabisa kuwa na mahusiano na
mwanaume yoyote yule. Hii inadhihirika mwandishi anaposema;
“ Alipotaka
kupita pale alipokuwa amekaa ilia toke njee, Padre John akamdaka
mkono na kumvuta
hadi kwenye mlango na kufunga mlango. Kwa mikono
miwili akamshika
huyo mwanamke mbichi aliyekuwa anamtia wazimu na
kumbania kifuani
kwake na kusikia joto huku mkia wake uliokwisha vimbiana
kama kifutu
anayetaka kuuma mtu unatafuta mapaja laini ya huyo kigoli mtoka
mbali. Bugonoka akashikwa na
ghadhabu kweli na kuamua kumalizana na
huyo mshenzi
mkubwa, na akamsukuma kwa nguvu zake zote ili aweze
kumuachia” ( Uk 95
)
Hivyo tunaona kuwa katika jamii zetu pia kuna wanawake ambao
wana misimamo na ambao hawataki kuyumbishwa na mtu yeyote. Kuwa na msimamo ni
kitu cha muhimu katika jamii na kwenye maisha. Watu wengi hasa wanawake hukosa
maamuzi kutokana na kutokuwa na msimamo.
Katika riwaya hii mwandishi amewaonesha wanawake kama chombo
cha starehe kwa kumstarehesha mwanaume. Wanawake hao walikuwa wanatumiwa na
Padre John kama starehe yake. Mwandishi
anasema;
“Hao mahawara zake walikuwa
tisa na pia akiwa anawabadilisha mmoja kwa kuleta
mpya mmoja kila mwezi
unapoandama. Yeye mwenyewe alikuwa
anaishi
kwenye nyumba ambapo wake zake na vimada wake pamoja na
wanawake
wengine chungu nzima wa kutoka nje walipelekwa
kumstarehesha kadri alivyo
hitaji. Nyumba ya hao
mahawara zake tisa na wake zake wanne
wanaobadilishwa
kama
shati ilikuwa uani” ( Uk 122 )
Pia tunaona kuwa katika jamii zetu wanawake wengi hutumiwa
kama chombo cha stsrehe na viburudisho kwa wanaume kitu ambacho kinashusha
thamani ya mwanamke kwenye jamii na familia yake.Wanawake wengine huamua
kujiuza kutokana na sababu mbalimbali hasa sababu za kiuchumi na ugumu wa
maisha.
Lengo la pili la utafiti huu ni kubainisha kufanana kati ya
nafasi ya mwanaume na mwanamke katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Hivyo kwa kutumia
mbinu ya maktabani na kuweza kusoma riwaya hiyo teule data mbalimbali
zilipatikana kuhusu kufanana kati ya mwanaume na mwanamke katika fasihi na
kuweza kuchambuliwa kama ifuatavyo.
Katika riwaya hii tunaona jinsi mwanaume na mwanamke
wakitimiza majukumu yao kwa kufanya kazi mbalimbali kwenye jamii zao. Mwandishi
anawaonesha wanaume ambao ni watoto wa mzee Ninwalo kama vile Magayane, na
wengine walivyokuwa wavuvi hodari wa kazi hiyo. Walifundishwa na baba yao, pia
walikuwa mafundi wa kutengeneza mitubwi, mafundi hao ni Magayane na Nagabona
mdogo. Mwandishi anasema
“Mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulikuwa mpya, uliotengenezwa na Magayane
akisaidiwa na mdogo
wake Nagabona” ( Uk 62 )
Halikadhalika kwa upande wa mwanamke naye hayuko nyuma
kwenye kufanya kazi mbalimbali kama mwanaume afanyavyo. Hii inadhihirika pale
mwandishi anapomuonesha Bugonoka akiwa anafanya kazi mbalimbali kama vile
kulima. Pia mwandishi anamuonesha mwanamke mwingine ambaye ni Maimuna ambaye
alikuwa ni mwanamke mchapakazi pamoja na kuwa na wasaidizi lakini alikuwa
akifanya kazi zake mwenyewe. Hii inadhihirika pale mwandishi anaposema
“Miaka yote kabla ya
hapo, Maimuna alikuwa ni mwanamke tajiri lakini
anayependa kufanya
kazi badala ya kufanyiwa kila kitu yeye amekaa tu na
kustarehe. Pamoja na
kwamba alikuwa na wafanyakazi watatu hapo nyumbani
kwake, kufua na
kupiga pasi nguo zake na za mumewe, hadi kupika, ado naye
alizifanya na hao wafanyakazi wake. Alidai
kwamba anapofanyiwa kazi huwa
haiendi sawa, hata
huko kwenye maduka yake pia alikuwa anafanya kazi zote za
huko” ( Uk 130 )
Hivyo tunaona jinsi mwanaume na mwanamke wanavyoweza kufanya
kazi mbalimbali katika jamii zao, pia katika jamii mbalimbali wanawake na
wanaume wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii ili kuweza kujipatia kipato na kuleta
maendeleo kwenye jamii zao.
Mwanaume na mwanamke katika riwaya hii wameonekana wote kwa
pamoja kushirikiana katika kuyakabili matatizo mbalimbali yanayotokea kwenye
jamii zao. Mwandishi anaonesha jinsi matatizo ya vifo yaliyo ikumba familia ya
mzee Ninwalo. Mwandishi anaonesha jinsi
wanaume na wanawake walivyoguswa na matukio hayo ya vifo pamoja na kutafuta utatuzi
wa matatizo hayo. Mwandishi anonesha ushirikiano huo pale anapoionesha familia
ya Mkaya na mumuwe pamoja na wanawe wa kike na wakiume wanapoamua kuvuka mto
usiku kwenda kwenye msiba wa mdogo wake Nakazenze mdogo. Mwandishi anasema;
“Kutoka pwani ya wavuvi
ya Kisolya kwenda pwni ya wavuvi ya Ngoma ni
mwendo kiasi
ukilinganisha na kivuko kifupi cha hapo Lugezi ya siku hizo. Siyo
mbali sana lakini kuna
mwendo wa hata wapiga makasia vijana na hodari kama
hao waliokuwa
wanavusha jirani zao wafiwa kuchukua kiasi cha nusu sa nzima,
na kwa mwendo wa
kukazana. Mkaya na wanawe na mumewe
wakaona
wamekishafika kwenye
msiba wao, na kilichobaki ni kutua tu alafu mkaya na
wanawe wote wa kike
wataanza kulilia marehemu wao kwa sauti za kuomboleza
na huenda hata Mazula
akawaunga mkono na kulia naye pia kwa sauti kubwa kwa
jinsi moyo wake
ulivyokuwa umejaa huzuni licha ya kwamba wanume walitakiwa
kuomboleza kimya
kimya ili waweze kutuliza waombolezaji
wenzao wa kike
wasizidiwe na majonzi” (
Uk 30 )
Katika jamii mbalimbali pia tunaona wanawake na wanaume
jinsi wanavyoshirikiana katika kuyakabili matatizo mbalimbali yanayojitokeza
kwenye jamii. Wote wamekuwa wakifarijiana hasa pale wanapopoteza wapendwa wao.
Mfano kwenye msiba wanaume na wanawake wamekuwa mstari wa mbele wote kwa pamoja
katika kuomboleza na kufarijiana pia kwenye
misiba wanawake wamekuwa wakijushughurisha na kupika chakula huku
wanaume wakichimba kaburi na kusomba maji kama maji yanapatikana mbali.
Katika riwaya hii mwandishi anamuonesha mzee Ninwalo na bi
Nakazenze kama wazazi na walezi wa familia yao. Walikuwa wakiishi katika kijiji
cha ukelewe na huko ndipo walipoweza kuzaa na kulea watoto wao. Tunaona kuwa
baada ya matatizo kuikumba familia yao na kupoteza watoto wao wote na kubaki
mtoto mmoja ambaye ni Bugonoka bado waliendelea kumlea mtoto wao huyo na kuamua
kumtafutia makazi mengine katika nchi ya usukumani. Hii inadhihirika pale
mwandishi anaposema
“Huko mzee Ninwalo alipaona huenda
pakamfaa kujaribu kumtaftia binti yake
Bugonoka na mjukuu wake
huyo mchanga Mazula dunia mpya, nchi itakayo
salimisha uhai wao,
Mungu akipenda na mahali watakapo weza kuishi maisha
yanayotamanika. Mkewe
Bibi Nakazenze akakubaliana na uwamuzi wake na pia
chaguo lake hilo”( Uk 62
)
Tunaona pia katika jamii mbalimbali baba na mama wamekuwa ni
nguzo kubwa katika familia zao. Pale baba au mama anapo kosekana kwenye
familia, familia huweza kuyumba na kuweza kupoteza mwelekeo. Hivyo ushirikiano
katika malezi kwenye familia.
Mwandishi anaonesha jinsi mwanaume na mwanamke wote kwa
pamoja wanavyoshirikiana katika kutoa mawazo. Hii inadhihirika pale Bugonoka
anapotoa wazo la kutaka kumlea Mazula ambaye alikuwa mtoto wa dada yake
Nakazenze mdogo. Wazo hilo linaonekana kuwashituwa wazazi wake hasa mzee
Ninwalo lakini mwisho anaruhusiwa kumlea mtoto huyo. Hii inadhihirika pale
mwandishi anaposema
“Ninwalo umemsikia binti yako!” Mkewe, Bibi Nakazenze, mshauri wake
mkuu
duniani akang’atuka
kwenye mshangao wake. Mzee Ninwalo akakubaliana na
mkewe kuhusu Bugonoka
kumlea Mazula kama mwanaye wa kumzaa na
kuongezea kuwa binti yetu mwenyewe anayeomba kuwa mama
ya huyu mtoto
mbona bado naye ni mtoto
mdogo. Mkewe akamjibu, huyu binti yetu kwanza ni
mama hasa wa huyu mtoto,
ni mama yake mdogo mdogo wa mama yake mzazi wa
baba mmoja na mama mmoja” ( Uk 45
)
Pia sehemu nyingine inayoonesha mwanaume na mwanamke
kushirikiana katika mawazo ni pale Mkaya na mwanae wa kiume Mazula
waliposhirikiana katika kutoa wazo la kutoa kafara baada ya mtumbwi wao kutaka
kuzama kwenye mji wakiwa wanavuka kwenda kwenye msiba wa ndugu yao Nakazenze
mdogo .Mwandishi anasema
“Mama labda nitoe sadaka!” Mazula alimuuliza mama yake. Alikuwa
amerithishwa jadi ya
kutambikia Mungu wa Ziwa Victoria, Nyanza na majii yote
ulimwenguni” ( Uk 31 )
Hivyo tunaona kuwa mwanaume na mwanamke wanafikra mbalimbali
ambazo fikra hizo zikiwekwa pamoja zinaweza kuwa chachu ya maendeleo kwenye
jamii. Kwa kawaida kunapokuwa na watu wengi kila mtu huwaza tofauti kutokana na
alivyoelewa.
Lengo la tatu katika utafiti huu ni kubainisha utofauti kati
ya nafasi ya mwanaume na mwanamke katika fasihi. Mwanaume na mwanamke katika
riwaya hii wanatofautiana katika mambo mbalimbali mathalani mwanaume anaonekana
kuwa na umuhimu na nafasi kubwa katika jamii kuliko mwanamke. Tofauti hizi kati
ya mwanaume na mwanamke zinaonekana kumuathiri mwanamke kwa kiasi kikubwa huku
mwanaume akionekana shujaa.
Katika riwaya hii mila na desturi ni moja ya kipengele
kinachobainisha utofauti kati ya mwanaume na mwanamke, kwani mila nyingi
zimekuwa zikimgandamiza mwanamke na kumkweza mwanaume. Mwandishi anaeleza kuwa
katika familia ya Mzee Ninwalo wanawake hawakupaswa kula na wanaume sehemu
moja, wanawake walikula kivyao na wanaume kivyao. Mwandishi anasema;
“ “Siku hizo wanaume wa Kikerewe wenye miji iliyojengwa na kujengeka,
kama
huo wa Mzee Ninwalo
walikuwa wanapikiwa ugali na kitoweo cha kufaa, na
hicho chakula walikila na watoto wao wa kike
na wakiume. Watoto wa kike
walikuwa
wanakula chakula na wanawake wenzao hawali chakula na
wanaume”.
(Uk 7)
Kwa kawaida wanaume hula chakula katika mazingira mazuri
kamavile mezani lakini wanawake hula chakula wakiwa wamekaa chini au jikoni hivyo
kudhihirisha utofauti kati ya mwanaume na mwanaamke. Utofauti huu husababisha
matabaka kwenye familia.
Mwandishi amemuonesha Mwanaume kama ndiye kiongozi mkuu
katika mambo mbalimbali huku mwanamke kuonekana kama mtekelezaji tu. Mwandishi
anasema katika kijiji cha ukerewe Watemi walikuwa ni wanaume na ndio viongozi
wa kijiji hicho na wala haijawahi kutokea mwanamke kuwa ntemi. Mwandishi
anasema;
“Mwakaa uliopita mtemi wa
Ukerewe wa zamani aliyekuwa ametawala nchi yake
kwa miaka mingi zaidi
ya kizazi kizima, alifariki. Mwaka huo, mwanawe wa
kiume kwanza kuzaliwa
alikuwa ametawazwa kama omukama, mtemi wa watu
wake” (Uk 70)
Tunaona katika riwaya hii hakuna sehemu inayomwonesha
mwanamke kama mtawala au kiongozi bali ni wanaume ndio watemi na viongozi
katika vijiji vyao, hivyo kuonesha utofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Hata
katika sehemu mbalimbali wanaume ndio wamekuwa wakipewa madaraka ya juu kuliko
wanawake hii ni kutokana na mazoea kuwa mwanamke hawezi kumuongoza mwanaume.
Sura ya nne inaonesha nafasi, tofauti na ufanano kati ya
nafasi ya mwanaume na mwanamke katika riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Matokeo yanaonesha kwamba pamoja na kuwepo
kwa ufanano na tofauti kati ya mwanamke na mwanaume, bado mwanaume anaonekana
kama nguzo muhimu katika jamii huku mwanamke akionekana kama mfuasi au mtumwa
wa mwanaume.
Madhumuni ya sura hii ni kutoa matokeo ya utafiti, matatizo
yaliyojitokeza wakati wa utafiti huu, mapendekezo kwa tafiti zijazo na
hitimisho
5.2 Matokeo ya
Utafiti
Mtafiti amechunguza ulinganishi wa nafasi ya mwanaume na
mwanamke katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa, ambapo ameonesha
nafasi za mwanaume na mwanamke katika fasihi, ufanano na utofauti wao. Sura ya
kwanza, inaelezea kuhusu utangulizi, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti,
umuhimu wa utafiti, mawanda ya utafiti na tatizo la utafiti. Sura tatu
inaelezea kuhusu mbinu zilizotumika katika ukusanyaji wa data, uwasilishaji wa
data pamoja na uchambuzi. Pia kuna eneo la utafiti, vifaa vya utafiti, mbinu za
kukusanya data na uchambuzi wa data pamoja na sampuli na usampulishaji. Sura ya
nne inaelezea kuhusu uchambuzi na uwasilishaji wa data. Katika sura hii mtafiti
aliweza kuwasilisha na kuchanganua data za utafiti. Sura ya tano inaelezea
kuhusu matokeo ya utafiti, muhutasari pamoja na mapendekezo.
Utafiti huu ulilenga kuchunguza ulinganishi wa nafasi ya
mwanamke na mwanaume katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Ili kutimiza hilo utafiti huu ulikuwa na
malengo mahususi yafuatayo; Kubainisha nafasi ya mwanaume na mwanamke
inayojitokeza katika fasihi, kubainisha ufanano kati ya nafasi ya mwanaume na
mwanamke katika fasihi na kubainisha utofauti kati ya nafasi ya mwanaume na
mwanamke katika fasihi kupiti riwaya ya Janga
Sugu la Wazawa. Malengo haya yalikusudia kujibu maswali yafuatayo; Je
mwanaume na mwanamke wana nafasi gani katika fasihi? Je kuna ufanano gani kati
ya nafasi ya mwanaume na mwanamke katika fasihi? na je kuna utofauti gani kati
ya nafasi ya mwanaume na mwanamke katika
fasihi?
Katika swali la kwanza mtafiti ameonesha nafasi mbalimbali
za mwanamke na mwanaume zinazojitokeza katika fasihi kama vile mwanaume ni mtu
mwenye upendo wa dhati, mtu msomi, na mtu mwenye tama ya ngono, pia mwanamke
anaoneshwa kama chombo cha starehe, mtu tajiri, na mtu mwenye msimamo. Katika
swali pili tumeonesha jinsi ufanano kati ya mwanaume na mwanamke ulivyo.
Wanafanana katika suala la malezi kwa kulea familia, wanafanana katika
kushirikiana katika kutoa mawazo, kushirikiana katika matatizo mbambali, wote
hufanya kazi mbalimbali kwenye jamii zao. Katika swali la tatu mtafiti
ameonesha utofauti kati ya mwanamke na mwanaume kwa kuonesha jinsi
wanavyotofautiana. Utofauti wa kwanza ni utofauti uliopo kwenye mila na desturi
nyingi humgandamiza mwanamke na kumkweza mwanaume, pia tofauti nyingine ni
tofauti katika uongozi na mgawanyo wa madaraka ambapo mwanaume ndio anapewa
nafasi kubwa kuliko mwanamke.
Katika utafiti huu mtafiti amegundua kuwa nafasi ya mwanaume
na mwanamke katika jamii ni muhimu kwani wote huweza kutimiza majukumu
mbalimbali. Mwanaume na mwanamke hawapaswi kubaguliwa na kupewa majukumu kwa
kuangalia jinsia zao, kwani majukumu yanayotekelezwa na mwanaume yanaweza
kufanywa na mwanamke. Pia mtafiti amebaini kuwa watu wanapaswa kuacha na
kutupilia mbali mila na desturi potofu zilizopitwa na wakati kwani hurudisha
nyuma maendeleo katika jamii zetu, mfano baadhi ya mila za makabila mbalimbali
mwanaume hapaswi kula na mwanamke, mwanaume huwa na sehemu yake ya kulia
chakula na mwanamke huwa na sehemu yake. Pia jamii zingine mwanamke asipopigwa
na mumewe hudai kuwa mume wake hana upendo wa dhati kwake kitu ambacho sio
sahihi. Hivyo mtafiti anaona kuwa mila na desturi anbazo zinamgandamiza
mwanaume au mwanamke hazifai na inabidi kuondolewa.
5.4
Mapendekezo ya Utafiti
Katika utafiti huu mtafiti amejikita katika kuangalia
ulinganishi wa nafasi ya mwanaume na mwanamke katika fasihi kupitia riwaya ya Janga Sugu la Wazawa. Tafiti nyingi za
watafiti zimejikita katika kuangalia nafasi ya mwanamke katika jamii. Hivyo
mtafiti anapendekeza kuwa itakuwa ni jambo la muhimu iwapo tafiti zijazo
zitaangazia na kuchunguza nafasi ya mwanaume katika fasihi na umuhimu kwani
tafiti nyingi zimejikita katika kumwangalia mwanamke tu na kumsahau mwanaume.
Mtafiti katumia riwaya katika kuangalia ulinganishi huo hivyo tafiti zijazo
zinaweza kuangalia kwa upana zaidi kwa kutumia ushairi, tamthilia na nyimbo.
Utafiti huu umegawanywa katika sura tano ambapo sura ya
kwanza inahusu utangulizi wa jumla, sura ya pili inahusu mapitio ya maandiko,
sura ya tatu inahusu mbinu za utafiti, sura ya nne inaelezea kuhusu
uwasilishaji na uchambuzi wa data na sura ya mwisho ni muhutasari, mapendekezo
na hitimisho.
Chaligha, E. N. (2011). “Usawiri wa
Mwanamke na Mgawanyo wa Majukumu Kinjinsia katika
Fasihi Picha ya Katuni Mnato za
Kiswahili” Tasnifu ya M . A Kiswahili, Chuo Kikuu
Cha Dar es Salaam.
Madumulla, J. S. (2009). Riwaya ya Kiswahili, Historia na Misingi
ya Uchambuzi. Nairobi:
Sitima Printer and Station Ltd.
Muhando, P., & Balisidya. (1976). Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Dar es
Salaam: Tanzania
Publishing House.
Mulokozi, M, M. (1996). Fasihi ya Kiswahili. Dar es salaam:
The Open University of Tanzania.
Nkwera, F. (1978). Sarufi na Fasihi Sekondari na vyuo. Dar es salaam: Tanzania Publis House.
Ruhumbika, G. (2002). Janga Sugu la Wazawa. Dar es salaam: E
& D Limited.
Senkoro, F. E. M. K. (1982). The Prostitute in Africa Literature.
Dar es salaam: University press.
Wamitila, K. Y. (2003). Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia.
Nairobi: Focus Publication Ltd.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com