1.1 Dhana ya matumizi ya lugha kwa
ujumla
ü Hii
ni dhana inayohusu muktadha halisi wa kijamii wa matumizi ya lugha. Muktadha
huo unatokana na kuhusisha shughuli zinazofanywa na jamii inayohusika, mada za
mazungumzo, mahusiano miongoni mwa wanaowasiliana na mahali yanapofanyika
mawasiliano hayo.
ü Mambo
hayo yanahusishwa kwa namna ambayo inawezekana kubainisha, kutofautisha na
kuhusisha mwenendo wa mtu binafsi wa matumizi ya lugha na utaratibu wa
jamiilugha wa matumizi ya lugha.
ü Kutokana
na mahusiano hayo inawezekana kusema kwa uhakika mkubwa kwamba katika jamiilugha
husika, lugha fulani kwa kawaida ndio hutumika katika mazungumzo ya eneo
fulani.
ü Kufahamu
ni lugha ipi inatazamiwa kutumika katika eneo gani la matumizi ya lugha ni kufahamu
mojawapo ya kanuni muhimu za kiisimujamii katika jamiilugha husika. Kuacha
kutumia lugha inayotazamiwa kutumika katika eneo fulani la matumizi ya lugha
katika mazungumzo kunadhaniwa na wanajamii kwamba ama kutokana na kutofahamu
kanuni za isimujamii za jamiilugha husika, au kuna ashiria mabadiliko katika
kanuni hizo au kutokana na msemaji kutaka kufikia malengo mahususi ya
kimawasiliano na kimahusiano.
Maeneo
hayo yanatofautiana kutoka jamiilugha moja hadi nyingine, lakini upo ufanano
katika jamiilugha nyingi katika baadhi ya maeneo hayo kama vile familia (ambapo
watu wanaoishi kwa pamoja katika familia moja wanawasiliana wakiwa nyumbani)
mtaani, kazini, serikalini,mashuleni, sokoni na kwenye shughuli za utamaduni.
Maeneo
ya matumizi ya lugha yanaweza kugawanywa katika makundi makubwa mawili
kutegemeana na jinsi yanavyohusiana na shughuli za kidola. Kuna maeneo rasmi na
maeneo yasiyo rasmi ya matumizi ya lugha. Maeneo rasmi ni yale ambayo matumizi
yake ya lugha kwa namna moja au nyingine yanaratibiwa au kuathiriwa moja kwa
moja na taratibu za dola. Miongoni mwa maeneo hayo ni kazini, elimu na mafunzo
na mahakamani. Maeneo yasiyorasmi ni yale ambayo hayaratibiwi au kuathiriwa
moja kwa moja na taratibu za kidola. Miongoni mwa maeneo hayo ni nyumbani na
miongoni mwa wanafamilia na maeneo ya makazi na miongoni mwa majirani. Haya ni
maeneo ambamo kwa kawaida hutumika lugha za kijamii. Kwa kawaida, maeneo rasmi
ya matumizi ya lugha huwa yenye hadhi na fahari kubwa zaidi ya maeneo
yasiyorasmi na matumizi ya lugha katika maeneo hayo hatimaye huchochea mabadiliko katika maeneo
yasiyorasmi ya matumizi ya lugha na kusababisha hatari ya lugha au vilugha
kutolewa.
1.2 Maeneo ya matumizi ya Kiswahili
Lugha ya Kiswahili ina
hadhi miongoni mwa Watanzania wa ngazi zote katika jamii. Watanzania takriban
wote wanahitaji na kuhitajika kutumia lugha hii katika maeneo yote yaliyo rasmi
isipokuwa mawasiliano ya kimataifa, elimu ya juu, kutunga sheria na mahakama za
juu. Maeneo mengine yoye ya matumizi ya lugha humuhusu na kumuhusisha karibu
kila mtu. Kwa kiasi fulani matumizi ya lugha ya Kiswahili yanawatambulisha
Watanzania wengi na jamii pana ya kitaifa. Hata hivyo, tathmini ya lugha hii
kuwa yenye ufahari ni kwa watu wa ngazi za chini. Watu wa ngazi hizo huiona
lugha hii kama kigezo cha kushiriki katika jamii pana na kama kigezo cha
kujiendeleza kijamii. Watu wa ngazi za juu wanaitambua lugha hii kama kigezo
cha kushiriki katika jamii pana na kama kigezo cha kushiriki katika maeneo
rasmi inamotumika. Lakini si wengi wao wenye kuithamini kuwa lugha yenye
ufahari mkubwa.
Lugha
nyingine zote za kijamii, ikiwa ni pamoja na vilugha vya Kiswahili vilivyo
lugha za kijamii, zina hadhi miongoni mwa watu wengi sana katika jamii. Watu
wengi wanazitumia lugha hizi katika mawasiliano yao mengi katika maeneo yasiyo
rasmi ya matumizi ya lugha, hasa vijijini na majumbani mwao katika familia zao.
Pia ni lugha ambazo matumizi yake yanawatambulisha watu wa jamii zao za
kikabila na fasihi na utamaduni unaoambatana na jamii zao.
Lugha ya Kiswahili inaweza kutumika katika
maeneo mbalimbali kama haya yafuatayo:-
(a)
Majumbani na
miongoni mwa wanafamilia
Hili
ni eneo lisilo rasmi la matumizii ya lugha. Katika eneo hili taratibu za
matumizi ya lugha haziamuliwi moja kwa moja na matumizi ya lugha, bali mfumo wa
mahusiano ya kijamii. Watafiti wengi wameripoti kwamba kwa jumla na kwa kawaida
mawasiliano yanayofanyika majumbani miongoni mwa wanafamilia moja, ndugu na
marafiki wa karibu hufanyika kwa lugha za kijamii (Abdulazizi Mkilifi, 1972;
Brauner na wenzake, 1978, Rubagumya 1991, Mekacha 1993, Ngonyani, 1994 na
wengineo). Takwimu zinaonesha kwamba hadi hivi sasa bado asilimia kati ya 75 na
80 ya Watanzania wote wanaishi vijijini na wanategemea ukulima wa kujikimu. Kwa
hiyo, kwa Watanzania wengi, lugha za kijamii ndiyo kwa kawaida zinatazamiwa
kutumika majumbani na katika familia. Kutawala kwa matumizi ya lugha hizo
katika eneo hilo kutokana na siyo tu mahitaji ya kimawasiliano, yana haja ya
watu kuwasiliana kwa lugha wanayoifahamu vyema zaidi, bali pia ukweli kwamba
lugha za kijamii zimefungamana na utamaduni na maisha ya jamii hizo na ni
kigezo kimojawapo cha kuzitambulisha.
Katika
ripoti za utafiti za hivi karibuni, inaoneshwa kwamba hata huko vijijini kuna
matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mazungumzo ya watu wa familia moja
majumbani, hasa kwa watu wenye umri mdogo. Kwa hiyo, ingawa majumbani na
miongoni mwa watu wa familia moja, matumizi ya lugha za kijamii ndiyo
yanatawala, huko vijijini kuna ushahidi kwamba matumizi ya lugha ya Kiswahili,
hasa miongoni mwa watu wenye umri mdogo, yanaanza kubadilika kuwa ya kawaida (Mekacha,
1993; Ngonyani, 1994, Yoneda, katika Hino 1996; Msanjila, 1996). Hata hivyo
matumizi ya lugha ya Kiswahili majumbani na miongoni mwa wanafamilia ni makubwa
zaidi mijini kuliko vijijini. Hii inatokana hasa na ukweli kwamba mijini
familia za watu wa kutoka jamii tofauti huishi karibu karibu. Hali hiyo hufanya
matumizi ya lugha ya Kiswahili kutawala kote isipokuwa baina ya wanafamilia
ndani ya nyumba yao tu.
(b)
Katika maeneo ya
makazi miongoni mwa majirani
Katika
maeneo ya makazi miongoni mwa majirani, matumizi ya lugha si tofauti sana na
kama ilivyo majumbani na miongoni mwa wanafamilia katika maeneo ya vijijini.
Ingawa kuna ushahidi kwamba kuna matumizi kidogo ya Kiswahili, vijijini
matumizi yanayotawala katika maeneo ya makazi na mingoni mwa majirani ni lugha
za kijamii. Hii ni kwa sababu hasa kwamba wengi wa majirani huwa ni watu wa
jamii ileile na ambao pia wanazungumza lugha hiyo hiyo ya kijamii. Kadhalika,
ingawa hutokea yakasikika matumizi kidogo ya lugha za kijamii miongoni mwa
majirani walio wasomi, mijini maongezi yanayotawala katika maeneo ya makazi na
miongoni mwa majirani ni Kiswahili. Hii inatikokana hasa na ukwel kwamba mijini
watu wa kutoka jamii tofauti huishi wakiwa majirani na hivyo kuhitaji lugha ya
mawasiliano mapana kuwasiliana, lugha ambayo kwa Tanzania ni Kiswahili. Pia
inatokana na hadhi na ufahari wa lugha ya Kiswahili ikilinganishwa na lugha za
kijamii ambapo matumizi ya lugha za kijamii yanafungamanishwa na ukabila wakati
matumizi ya Kiswahili yanafungamanishwa na maendeleo, usasa na hisia za utaifa.
(c)
Katika masoko na
biashara za ndani ya nchi
Kadhalika,
katika masoko na biashara za ndani ya nchi, tofauti kubwa katika matumizi ya
lugha ni baina ya mjini na vijijini. Mijini matumizi ya lugha ya Kiswahili
yanatawala karibu kwa namna ile ile yanavyotawala katika maeneo ya makazi na
miongoni mwa majirani, hata hivyo katika masoko na biashara za ndani mijini
hakuna matumizi ya lugha za kijamii, na kama yapo ni kidogo mno kiasi kwamba
hayatazamiwi na si ya kawaida. Vijijini, katika masoko na biashara za ndani
matumizi ya lugha za kijamii ni makubwa zaidi na ambavyo kwa kiasi fulani
yanatazamiwa. Hata hivyo kuna matumizi makubwa pia ya lugha ya Kiswahili katika
masoko na biashara za ndani kuliko ilivyo majumbani na miongoni mwa wanafamilia
na katika makazi na miongoni mwa majirani.
(d)
Sehemu za kazi
Wengi
wa watu vijijini hujishughulisha na kazi za ukulima, ufugaji na uvuvi wakati
wengi wa watu wa mijini hujishughulisha na kazi za maofisini, viwandani, huduma
na biashara. Kazi za watu wa vijijini hufanywa katika familia au kwa
ushirikiano na majirani, lakini nyingi za kazi za mijini hufanywa kwa
ushirikisha watu wasio na familia wala
majirani. Huku vijijini watu wanaoshirikiana aghalabu huwa wa jamii moja na
huwa wazungumzaji wa lugha moja ya kijamii wakati mijini watu wanaoshirikiana katika
kazi aghalabu huwa kutoka jamii tofauti. Kazi nyingi vijijini ni eneo lisilo
rasmi la matumizi ya lugha wakati kazi nyingi mijini ni eneo rasmi la matumizi
ya lugha. Kwa sababu hiyo, kwa jumla
matumizi ya lugha katika meneo ya kazi hutofautiana baina ya miji na vijiji,
ambapo vijijini matumizi ya lugha za kijamii hutawala na mijini matumizi ya
lugha ya Kiswahili hutawala.
(e)
Katika
usafiri wa umma
Katika usafiri wa umma,
kwa kawaida hukutana na watu ambao hawafahamiani. Kadhalika usafiri wa umma ni
eneo la umma kwa maana kwamba watu wanahusiana kulingana na taratibu za umma na
wala sio kutokana na undugu, urafiki au ujirani. Kutokana na kuwa eneo la umma,
usafiri wa umma hufuata sana ratatibu za matumizi ya lugha sawa na maeneo
rasmi. Kwa sababu hizo, lugha inayotawala katika matumizi katika eneo hilo huwa
lugha ya umma, bila kujali kama ni vijijini au mijini. Katika Tanzania lugha ni
Kiswahili. Kwa hiyo, nchini Tanzania matumizi ya lugha ya Kiswahili ndiyo
yanayotawala katika usafiri wa umma.
(f)
Katika shughuli
za michezo na burudani
Shughuli
za michezo na burudani zinazofanywa ni nyingi na zinatofautiana kutoka mahali
pamoja hadi pengine na kutoka tabaka la watu hadi wengine. Baadhi ya shughuli
za michezo na burudani ambazo hufanywa katika mukatdha usio rasmi. Hata hivyo
tofauti muhimu ya matumizi ya lugha katika eneo hili ni baina ya vijiji na
miji. Mijini shughuli za michezo na burudani hutawaliwa na matumizi ya
Kiswahili wakati vijijini shughuli hizo hutawaliwa na matumizi ya lugha za
kijamii.
(g)
Katika
mfumo wa elimu na mafunzo
Matumizi ya lugha
katika mfumo wa elimu na mafunzo ni eneo rasmi la matumizi ya lugha. Nchini
Tanzania, hili ni eneo ambalo limepata kutafitiwa na kujadiliwa kwa kina na kwa
mapana, pengine kuliko maeneo mengine yote ya matumizi ya lugha. Hii ni kwa
sababu sera ya lugha nchini Tanzania imeruhusu hasa matumizi ya lugha katika
mfumo wa elimu. Mfumo wa elimu na mafunzo nchini Tanzania una ngazi kuu tatu,
elimu na mafunzo ya msingi, elimu na mafunzo ya sekondari na elimu na mafunzo
ya juu. Kulingana na sera ya lugha inayoendelea kutekelezwa nchini hadi hivi
sasa elimu ya watu wazima, elimu ya msingi na mafunzo ya ngazi za chini (yaani yanayowalenga watu wa vijijini
na ambao elimu yao ni msingi) inapaswa kutolewa kwa lugha ya Kiswahili. Elimu ya
kuanzia ngazi ya sekondari na mafunzo mengine yanayotolewa kwa watu waliohitimu
masomo ya ngazi ya sekondari na kuendelea yanatakiwa kutolewa kwa Kiingereza.
(h)
Katika
utawala na siasa
Utawala na siasa ni
eneo rasmi la matumizi ya lugha kutokana na ukweli kwamba shughuli za utawala
ni za kiserikali na shughuli za kisiasa huambatana kwa karibu sana na zile za
kiserikali. Kwa sababu hiyo matumizi ya lugha katika eneo hilo kwa kiasi
kikubwa hutawaliwa na miongozo, kanuni na taratibu zinazoamuliwa na dola.
Shughuli za kiserikali za kiutawala na zile za kisiasa ni zenye mamlaka katika
jamii na hufanywa na watu wenye madaraka. Kwa sababu hiyo, lugha inayotakiwa
kutumika katika maeneo hayo inatakiwa kuwa lugha yenye mamlaka na ambayo
inapendwa na watu wenye madaraka na lugha ambayo ina ufahari katika jamii.
Katika eneo hili kinatawaliwa na matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza.
Lugha za kijamii hazina nafasi na kama zinatumika ni kwa kiwango kidogo sana katika
ngazi za chini kabisa za utawala, ambapo zikitumika ni kwa sababu maalumu.
Lugha ya Kiswahili ndiyo inatawala kwa kiasi kikubwa matumizi ya lugha katika
eneo hili katika ngazi zote. Matumizi ya lugha ya Kiingereza yanatawala katika
baadhi ya shughuli za ngazi za juu kabisa na siasa.
(i)
Katika
ibada na shughuli za kidini
Nchini Tanzania wapo
watu wanaofanya ibada kwa kufuata madhehebu mbalimbali ya dini ya kikristu,
wapo wanaofanya ibada kwa kufuata madhehebu mbalimbali ya dini ya kiislamu,
wapo wanaofanya ibada kwa mijibu wa dini za kiasili za jamii zao na pia wapo
watu ambaohawafanyi ibada zozote kwa kuwa hawaamini katika kuwapo kwa mungu.
Kuenea kwa dini za kigeni katika nchi ya Tanzania kulisaidia sana katika kuenea
kwa lugha ya Kiswahili kutokana na ukweli kwamba kwa jumla dini hizo zilienezwa
kwa lugha ya Kiswahili, ingawa taratibu za matumizi ya lugha zilitofautiana
kutoka dini moja hadi nyingine. Baada ya kupatikana kwa uhuru, hata hivyo na
hata baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha shughuli nyingi za dini hizo
zilitawaliwa na matumizi ya lugha ya Kiswahili. Hata hivi sasa matumizi ya
lugha ya Kiswahili ndiyo yanayotawala katika ibada ya shughuli nyingine za dini
hizo.
(j)
Katika
mfumo wa sheria na mahakama
Matumizi ya lugha
katika mahakama na mfumo wa sheria ni mojawapo ya mambo yanayoelezwa na sera ya
lugha nchini. Kulingana na sera hiyo, Kiswahili ndiyo lugha inayotakiwa
kutumika katika ngazi za chini za mahakama. Lugha ya Kiswahili ndio hutumika
katika kusikiliza mashauri katika mahakama za mwanzo na kumbukumbu za mashauri
hayo huandikwa kwa Kiswahili. Hata hivyo hapana shaka kwamba katika ngazi hii,
hasa huko vijijini kuna matumizi kidogo ya lugha za kijamii katika uendeshaji
wa mashauri. Sera ya lugha inazitaka mahakama za hakimu mkazi kuendesha mashauri
kwa lugha ya Kiingereza, ingawa matumizi ya lugha ya Kiswahili yanaruhusiwa
pia. Hata hivyo, mashauri mengi yanaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na lugha ya
Kiingereza hutumika tu pale panapokuwa na malumbano ya kisheria miongoni mwa
mawakili, waendesha mashtaka na mahakimu.
Maeneo mengine ambamo Kiswahili
hutumika ni kama vile katika mawasiliano na maandishi, katika uandishi na
usomaji wa kazi za fasihi na katika vyombo vya habari.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com