Isimujamii ina
malengo makubwa matatu yafuatayo:-
(a) Kuchunguza
tofauti za wazungumzaji wa lugha katika jamii.
Wanaisimujamii
hufanya uchunguzi na kufafanua tofauti zilizopo za watumiaji wa lugha katika
jamii na kueleza tofauti hizo za wazungumzaji husababishwa na nini. Kuelewa
lugha ya jamii kunaendana na kuielewa jamii yenyewe ikiwa ni pamoja na
kuyaelewa matabaka na makundi mbalimbali yaliyomo ndani ya jamii hiyo. Jamii
imeundwa na matabaka na makundi mbalimbali ya watu. Kuna matabaka ya watawala
na watawaliwa, wakulima na wasiowakulima, wafanyakazi wa kuajiriwa na
wasiowakuajiriwa, waliosoma na wasiosoma, wafanyabiashara na wasio
wafanyabiashara n.k. Pia kuna makundi ya vijana, wazee, wanawake, wanaume,
wanafunzi, wanachuo, wanamichezo n.k. Ukichunguza kwa makini utabaini kuwa kila
tabaka au kundi la watu katika jamii hutumia lugha inayotambulisha tabaka au
kundi hilo. Kuchunguza na kufafanua tofauti za wazungumzaji wa lugha katika
jamii kunasaidia watumiaji wa lugha kufahamu watumie lugha ipi katika mazingira
rasmi na yasiyo rasmi miongoni mwa wanajamii wenyewe. Lugha rasmi ni ile lugha
iliyokubalika na kutangazwa na chombo chenye mamlaka ili lugha hiyo itumike
katika shughuli za serikali, bunge, mahakama, elimu nakadhalika. Pia umuhimu
mwingine wa kuchunguza tofauti za wazungumzaji wa lugha ni kusaidia
wazungumzaji kufahamu namna bora ya kutumia lugha katika mawasiliano ya jamii
baina ya wazungumzaji na msikilizaji.
(b) Kufanya uchunguzi na kufafanua uhusiano uliopo
baina ya lugha na wazungumzaji wake. Lengo hili pia linalenga kuifahamu jamii
kwa kuchambua lugha ya wazungumzaji wanayoitumia. Kwa kuchambua lugha wanayoitumia
wazungumzaji, tunaweza kuitambua jamii inayohusika kama ina dini ua imani ipi,
iko maeneo gani ya nchi (pwani, bara, kusini/kaskazini n.k), watu wake
wanafanya kazi gani, wanaume au wanawake, vijana au wazee, wasomi au
wasiowasomi n.k
(c) Kuangalia
uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine
Mwanaisimujamii
anapaswa kuchunguza na kutolea ufafanuzi uhusiano uliopo baina ya lugha moja na
lugha nyingine zinazotumika. Katika jamii au taifa kuna lugha zaidi ya moja
zinazotumiwa na watu. Nchini Tanzania, kwa mfano, kuna lugha zaidi ya 120
zinazotumiwa na watu mbalimbali. Kidhima lugha hizi zimegawanywa katika makundi
matatu. Lugha ya Kiingereza, lugha ya Kiswahili na lugha za kijamii. Ni kazi ya
mwanaisimu kufanya uchunguzi na ufafanuzi wa mambo ya msingi yanayohusu
uhusiano wa lugha hizi na wazungumzaji wake kwa kuzingatia mahitaji ya jamii ya
wakati huo.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com