5.1 Malengo ya
isimujamii
Isimujamii ina
malengo makubwa matatu yafuatayo:-
(a) Kuchunguza
tofauti za wazungumzaji wa lugha katika jamii.
Wanaisimujamii
hufanya uchunguzi na kufafanua tofauti zilizopo za watumiaji wa lugha katika
jamii na kueleza tofauti hizo za wazungumzaji husababishwa na nini. Kuelewa
lugha ya jamii kunaendana na kuielewa jamii yenyewe ikiwa ni pamoja na
kuyaelewa matabaka na makundi mbalimbali yaliyomo ndani ya jamii hiyo. Jamii
imeundwa na matabaka na makundi mbalimbali ya watu. Kuna matabaka ya watawala
na watawaliwa, wakulima na wasiowakulima, wafanyakazi wa kuajiriwa na
wasiowakuajiriwa, waliosoma na wasiosoma, wafanyabiashara na wasio
wafanyabiashara n.k. Pia kuna makundi ya vijana, wazee, wanawake, wanaume,
wanafunzi, wanachuo, wanamichezo n.k. Ukichunguza kwa makini utabaini kuwa kila
tabaka au kundi la watu katika jamii hutumia lugha inayotambulisha tabaka au
kundi hilo. Kuchunguza na kufafanua tofauti za wazungumzaji wa lugha katika
jamii kunasaidia watumiaji wa lugha kufahamu watumie lugha ipi katika mazingira
rasmi na yasiyo rasmi miongoni mwa wanajamii wenyewe. Lugha rasmi ni ile lugha
iliyokubalika na kutangazwa na chombo chenye mamlaka ili lugha hiyo itumike
katika shughuli za serikali, bunge, mahakama, elimu nakadhalika. Pia umuhimu
mwingine wa kuchunguza tofauti za wazungumzaji wa lugha ni kusaidia
wazungumzaji kufahamu namna bora ya kutumia lugha katika mawasiliano ya jamii
baina ya wazungumzaji na msikilizaji.
(b) Kufanya uchunguzi na kufafanua uhusiano uliopo
baina ya lugha na wazungumzaji wake. Lengo hili pia linalenga kuifahamu jamii
kwa kuchambua lugha ya wazungumzaji wanayoitumia. Kwa kuchambua lugha wanayoitumia
wazungumzaji, tunaweza kuitambua jamii inayohusika kama ina dini ua imani ipi,
iko maeneo gani ya nchi (pwani, bara, kusini/kaskazini n.k), watu wake
wanafanya kazi gani, wanaume au wanawake, vijana au wazee, wasomi au
wasiowasomi n.k
(c) Kuangalia
uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine
Mwanaisimujamii
anapaswa kuchunguza na kutolea ufafanuzi uhusiano uliopo baina ya lugha moja na
lugha nyingine zinazotumika. Katika jamii au taifa kuna lugha zaidi ya moja
zinazotumiwa na watu. Nchini Tanzania, kwa mfano, kuna lugha zaidi ya 120
zinazotumiwa na watu mbalimbali. Kidhima lugha hizi zimegawanywa katika makundi
matatu. Lugha ya Kiingereza, lugha ya Kiswahili na lugha za kijamii. Ni kazi ya
mwanaisimu kufanya uchunguzi na ufafanuzi wa mambo ya msingi yanayohusu
uhusiano wa lugha hizi na wazungumzaji wake kwa kuzingatia mahitaji ya jamii ya
wakati huo.
5.3 Isimujamii ya mawandafinyu
Huu
ni makabala wa kiisimu unaozingatia lengo la kwanza na la pili la isimujamii
katika uchunguzi na uchanganuzi wake. Ni makabala unaochunguza uhusiano wa
tofauti za wazungumzaji wa lugha na kubainisha vitambulisho vya usemaji au
utamkaji wa wazungumzaji au wazungumzaji ili kuhusisha na kundi la aina ya watu
au matabaka ndani ya jamii. Mwanaisimu Labov (1972) katika utafiti wake
alioufanya katika jiji la New York, Marekani ameonyesha kuwa, watu wa tabaka la
chini hutamka sauti [r] kwa mkwaruzo zaidi katika maneno yenye fonimu /r/
kuliko watu wa matabaka mengine (tabaka la juu). Trughdill (1874), katika
uchunguzi alioufanya nchini Uingereza, ameonyesha kuwa mbali na kuwepo kwa
lahaja la kijiografia, pia kuna lahaja za kijamii yaani zinazoonyesha hadhi
mbalimbali za watumiaji wa lugha ya Kiingereza. Kwa maneno mengine Trudgill
anaeleza kwamba unaweza kupata lahaja za wazungumzaji wa hadhi ya juu na lahaja
za wazungumzaji wa hadhi ya chini.
5.4 Isimujamii ya mawandamapana
Huu
ni mkabala unaozingatia lengo la tatu la isimujamii ambalo linachunguza na
kufafanua uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine zinazotumika katika jamii.
Kwa mujibuwa mkabala huu, mambo yanayozingatiwa ni yale yote yanahohusu
utumiaji wa lugha kwa jumla. Kujua lugha zilizopo katika jamii na uhusiano wake
kidhima na lugha nyingine ni moja ya mambo ya msingi ya mkabala huu. Kwa mfano
mwanaisimujamii katika mkabala huu, hupenda kujua sababu za msingi zinazofanya
lugha moja iteuliwe kuwa lugha ya taifa, lugha rasmi au lugha ya kufundis hia
katika mfumo wa elimu. Sababu zinazotumika kuteua lugha kuwa na dhima kitaifa
mara nyingi huwa hazina budi zitokane na sababu za msingi za kiisimu na
kijamii. Kimsingi, hata zile lugha ambazo haziteuliwi kuchukua dhima yoyote
kitaifa bado kwa mujibu wa mkabala huu, ni muhimu lugha hizo kufanyiwa
uchunguzi ili kuona hali halisi ilivyo, kwa lengo la kutaka kujua hatma ya
lugha hizo, hasa kule zinakotumika na pia kutaka kujua maendeleo ya lugha hizo
ili kuweza kutoa mapendekezo ya nini kifanyike. Uhusiano huu wa lugha
mbalimbali katika jamii hutegemea sana sera ya lugha ya nchi husika. Mkabala
huu huhusisha watu wengi kijiografia. Mathalani, mkabala huu unaweza kuhusisha
wazungumzaji wa nchi moja, nchi zilizoungana, jumuia ya nchi kadhaa, kanda za
nchi mbalimbali na hata huweza kuhusisha wazungumzaji wa bara zima. Kimsingi,
mkabala huu wa mawanda mapana ni mkabala ambao kusema ukweli, uchunguzi wake
unalenga kutatua matatizo mbambali yahusuyo utumiaji wa lugha kitaifa na
kimataifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment
syliverymanyama@gmail.com