Flower
Flower

Tuesday, September 12, 2017

Dhana ya lugha na lahaja


Lugha ni mfumo wa sauti nasibu ambazo zimebuniwa na jamii kwa madhumuni ya mawasiliano kati yao (Massamba 2004:45).  Jambo la msingi la kuzingatia katika fasili hii ni kuelewa kwamba dhima kuu ya lugha katika jamii ni kuwezesha mawasiliano miongoni mwa jamii yaweze kufanyika na kufanikiwa. Kwa kutumia lugha inayofahamika na jamii mbalimbali, jamii moja inaweza kuwasiliana na jamii nyingine ya mbali. Kufanikiwa kwa mawasiliano hupimwa na mzungumzaji pale anapoona kuwa msikilizaji wake ameitikia na ametenda kama anavyotarajiwa. Inapotokea msikilizaji akashindwa kuelewa au kutenda sawasawa na makusudio ya mzungumzaji wake, mambo kadhaa yanaweza kuwa yamechangia. Yawezekana mzungumzaji ametumia lahaja, lafudhi tofautitofauti, misimu au hata ametumia lugha za kigeni ambazo hazifahamiki kwa wasikilizaji wake.

Wazungumzaji wa lugha moja wanapoongezeka na kuwa wengi husababisha wakazi wake kutafuta maeneo mengine mapya ya kuishi na kufanya maeneno ya wazungumzaji wake kupanuka. Inapotokea wazungumzaji wa lugha hiyo watokao sehemu moja wanatamka baadhi ya maneno tofauti na wazungumzaji wa lugha hiyohiyo watokao sehemu nyingine na bado wazungumzaji hao wote wakaelewana, basi hatusemi kuwa watu hao wanazungumza lugha tofauti, bali tunasema wanazungumza lahaja mbili tofauti.


Lahaja ni aina za lugha ambazo kimsingi huchukuliwa kama lugha moja isipokuwa hutofautiana katika baadhi ya vipengele fulani fulani kama lafudhi, fonolojia, na msamiati usiokuwa wa msingi (Massamba 2001:190). Kwa mfano lugha ya Kiswahili ina lahaja nyingi kama Kiunguja, Kimtang’ata, Kipemba, Kitumbatu, Chichifundi, Kivumba, Kingazija, Kisiu na kadhalika,

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny