SWALI: Huku ukionesha ubora
na udhaifu wa kila mtazamo. Hakiki mitazamo mbalimbali ya fonimu kama
inavyopendekezwa na wataalamu wa isimu
Wataalamu mbalimbali
wamejadili maana ya fonimu, Trubertzkoy (1939) kama anavyonukuliwa na Massamba
anasema fonimu ni jumla ya sifa za sauti zilizona umuhimu wa kifonolojia. Yaani
upambanuzi wake wa kutofautisha maana katika lugha au mfumo husika. Mfano:
maneno Pia-Nia sauti /p/ na /n/ ni fonimu kwani zinauwezo wakubadili maana.
De Courtney (1952)
akinukuliwa na Mgullu (1952:53) anasema fonimu ni kipande sauti ambacho picha
yake huwa akilini mwa mtu ambayo hukusudia aitoe wakati anaongea.
Massamba (2004) fonimu
ni kipande kidogo kabisa katika mfumo wa sauti za lugha ambacho kina sifa
pambanuzi kuweza kutofautisha na vipande vingine vya aina yake.
TUKI (2013) Fonimu
sarufi tamshi katika neno ambalo likibadilishwa na tamshi jingine maana ya neno
hilo hubadilika au hupotoka katika lugha hiyo. Mfano: neno sabuni na zabuni
hapa fonimu zinazotofautisha maana ni /s/ na /z/.
Dhana ya fonimu
imewashughulisha wanaisimu wengi na imeelezwa kwa namna mbalimbali. Wataalamu
wanakinzana na mara nyingine kukubaliana juu ya mitazamo yao kuhusu dhana ya
fonimu. Hyman (1975) anatoa mitazamo mikuu mitatu inayoelezea dhana ya fonimu.
Mitazamo hiyo ni fonimu kama tukio au uhalisia wa kifonetiki, fonimu kama tukio
la kisaikolojia na fonimu kama tukio la kifonolojia. Mitazamo hiyo ina ubora na
udhaifu wake kama ifuatavyo:
Fonimu kama tukio la
kifonetiki; Mtazamo huu unaongozwa na Daniel Jones(1975) ambao kwao wanasema
fonimu ni kundi la sauti muhimu na sauti
zinazohusiano nazo na ambazo hutumiwa
mahali pake na miktadha maalumu. Fonimu inatazamwa kuwa ni umbo halisi la
kifonetiki na linalodhihirishwa kwa sifa za kifonetiki yaani kimatamshi na
kimasikizi. Kwa mtazamo huu wanaona pia fonimu ni kundi la sauti zinazofanana
sana kifonetiki. Hivyo kama sauti mbili zinztofautiana sana kifonetiki haziwezi kuwa fonimu au kundi moja la fonimu.
Mathalani katika mfano ufuatao:
[kata] na
[pata]
Sauti [k] [kikwamizi,
si sghuna cha kaakaa laini] na sauti [p][kipasua si ghuna cha midomo] sauti
hizo ni tofauti sana kifonetik yaani mahali pa matamshi na utamkaji wake hivyo
ni fonimu mbili tofauti.
Ubora wa kigezo hiki
cha fonimu kama tukio la kifonetiki ni kuwa ni kigezo dhahiri kinachoweza
kuthibitishwa kwani sifa za kifonetiki ni za wazi na zinaweza kuchunguzika. Kwa
mfano kujua mpumuo wa sauti pale mtu anapotamka sauti ya mpumuo.
Lakini pia kigezo hiki
kimeonesha mbinu mbalimbali za utambuzi wa fonimu mbalimbali za lugha. Mbinu
hizo ni kama zifuatazo
Kigezo cha jozi
mlinganyuo finyu: Samweli akimnukuu Fischer (1957) anaeleza kuwa, jozi
mlinganyuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya kifonolojia iliyopo baina ya maneno
fulani. Maneno hayo yanatakiwa yawe namambo matatu ambayo ni;
a) Idadi
sawa ya fonimu
b) Fonimu
zinazofanana isipokuwa moja
c) Mpangilio
sawa wa fonimu
Kwa
mfano katika lugha ya Kiswahili maneno kama: /taa/, /saa/ na /baa/ ni jozi ya
mlinganyuo finyu kwasababu zina idadi sawa za fonimu yaani zote zina fonimu
tatu. Aina za fonimu zilizoponi sawa isipokuwa moja, yaani [t], [s] na [b]
sauti hizi ni tofauti kwasababu zina sifa tofauti za kifonetiki zinazoathiri
pia maana.
Kigezo cha pili nikigezo
cha mgawanyo wa kimtoano/ mtawanyo mkamilishano: Samweli akimunukuu Hyman
(1975) anaeleza kuwa, utoano ni dhana ambayo hutumiwa kuelezea uhusiano uliopo
baina ya sauti mbili au zaidi za fonimu moja ambazo haziwezi kutokea katika
mazingira sawa. Hivyo kila sauti huwa na mahala/ mazingira yake maalumu ambayo
hayawezi kukaliwa na sauti nyingine. Kwa mfano, kutoka katika lugha ya
kiingereza sauti [p], na [p] hutokea katika mazingira tofauti. Ambapo [p]
hutokea mahali popote pale na [ph]hutokea mwanzoni mwa neno tu mfano katika
maneno kama vile [pin], [pay] na [pan]. Sauti [p] na sauti [ph] ni sauti za
kundi moja kwasababu zinafanana sana kifonetiki na tofauti pekee ni mpumuo
ambayo hubadilisha mazingira ya utokeaji wake.
Kigezo cha tatu ni kigezo
cha mpishano huru: Mgullu (1999) anaeleza kuwa,ni uhusiano wa fonimu mbili
tofauti kubadilishana nafasi moja katika jozi maalumu ya maneno bila kubadili
maana ya maneno. Maneno hayo yanaweza kuwa na tofauti ya fonimu moja tu lakini
ni tofauti sana kifonetiki na haziwezi kuwa alofoni za fonimu moja. Mfano:
kichuguu na kisuguu, kheri na heri. Ubadilikaji wa sauti hizi unategemea hali ya
mtuna wazungumzaji wote wanaweza kutumia vibadala hivyo kulingana na tofauti za
kimazingira, kimtindo na tofauti za watu binafsi.
Kigezo cha nne ni
kigezo cha kubadilishana kwa sauti: Massamba (2012:78-79) anaeleza kuwa, sauti
fulani na sauti nyingine katika neno zinapobadilishwa na kuwekwa sauti nyingine
unaangalia kama kutatokea mkengeuko katika utamkaji au hautokea. Ambapo kuna
mkengeuko mkubwa na mkengeuko mdogo. Mkengeuko mkubwa unatokea pale
kunapokuwana fonimu mbili tofauti mfano: (uje), (eje) au (oje) sauti [u], [e]
na [o] zinapobadilishwa mkengeuko wake ni mkubwa sana unaweza kutambuliwa na
wasikilizaji na kama mkengeuko ni mdogo/si mkubwa sauti itachukuliwa kuwa ni
alofoni ya fonimu moja. Mfano: ‘Hiki ni changu’ na ‘iki ni changu’ sauti Hi na
I zinavyobadilishwa mkengeuko ni mdogo tu.
Kigezo cha tano ni
kigezo cha ulinganifu wa ruwaza: Massamba (2012:77) anasema wataalamu wa kigezo
hiki wanaeleza kwamba kuna namna ya kubaini fonimu na alofoni kwa kuangalia
ujitokezaji wa sauti fulani katika mfumo mzima wa fonolojia ya lugha husika.
Kama sauti fulani inajitokeza kwa namna fulani katika mazingira fulani basi iwe
hivyo hivyo katika mfumo mzima wa fonolojia husika. Mfano Kama katika Kiswahili
kuna sauti [c] basi isije kutokea kukawa na mfuatano wa [t] na [S] yaani [tS]na
ikawa [tSati] badala ya [cati]
Kigezo cha mwisho ni
mlandano wa kifonetiki: Hockett (1972) kama anavyonukuliwa na Hyman (1975)
anasema kuwa kama sauti ‘a’ na ‘b’ ni memba wa fonimu moja basi wanachangia
sifa moja au zaidi. Sauti za familia moja zina mlandano mkubwa wa kifonetiki.
Kwa mfano [p] na [ph] zote ni (+konso, +midomo, +ghuna, +kipasuo) tofauti yao
ni mpumuo tu. Hivyo basi hizi ni sauti za kundi moja kifonetiki.
Udhaifu wa mtazamo huu
ni kuwa hautoshi kuelezea dhana ya fonimu kwasababu sifa za kifonetiki hazina
maana kama hazitajikita katika mfumo wa lugha husika. Mfano katika kigezo cha
jozi mlinganuo finyu, ubadilishaji wa sauti ambazo kwazo waliona ni tofauti
kifonetiki unatokea katika maneno ya lugha husika na ambapo husababisha tofauti
ya maana.
Fonimu kama tukio au
uhalisia wa kisaikolojia: Mtazamo huu unapewa nguvu na wanasarufi kama vile
Noam Chomshy, Baudoun de Courtney na Morris Halle. Katika mtazamo huu wanaona
fonimu ni tukio la akilini. De Courtneykama anavyonukuliwa na Mgullu (1999) anasema
fonimu ni tukio la akilini ambapo huwa na nia ya mzungumzaji au jinsi
msikilizaji anavyomwelewa mzungumzaji au vyote viwili kwa pamoja. Kwa upande
wao wanaona wazungumzaji wa lugha wanazo sauti zote za lugha yao katika akili
na kile kinachotamkwa ni picha au taswira ya kile kilichopo ubongoni mwake.
Aidha katika kuelezea mtazamo huu Noam Chomsky (1957) kama anavyonukuliwa na
Mgullu (1999:52) anadai lugha ina mambo makuu mawili yaani umilisi na utendaji.
Umilisi ni ule ujuzi ambao wazawa wa lugha fulani huwa wanao unaowawezesha
kuelewa na kutunga sentesi sahili katika lugha zao na kupinga mitindo isiyo
sahihi. Anaendelea kusema kuwa umilisi wa wazawa wa lugha moja hufanana na
ndiyo maana huweza kuelewana.
Ubora wa mtazamo huu ni
kuwa watetezi wake wanadai kuwa wazawa wa lugha huelewa ni sauti zipi ni za
lugha yaona zina sifa zipi bainifu zinazoweza kuleta tofauti ya maana. Kwa
mfano: Wazungumzaji wa Kiswahili hutambua kuwa sifa ya mpumuo si ya msingi
katika lugha yao bila hata kujifunza isimu.
Pili mtazamo huu
unapewa nguvu na wanasaikolojia na wanabaiolojia ambao wanasema katika ubongo
wa msemaji au mwanadamu ipo sehemu inayojishughulisha na ujifunzaji na utumiaji
wa lugha na hii inathibitisha kuwa mwanadamu huwa na mfumo mzima na lugha yake
katika bongo lake. Lakini pia Massamba (2012:94) anaongeza kuwa wasemaji wazawa
wa lugha wanaweza kutambua ni sauti zipi zipo au hazipo katika lugha yao hata kama wao wenyewe si wanaisimu na hivyo
ni wazi kuwa msemaji wa lugha ameuhifadhi mfumo wa lugha akilini mwake.
Udhaifu wa mtazamo huu
kama unavyoelezwa na Twaddell(1935) akinukuliwa na Massamba (2012:94) anasema si
sahihi na anatilia mashaka kuihusisha fonimu na mambo ya akili au ubongo ambao
hauna uwezo wa kuuingiliwa na kuthibitisha na hivyo mtazamo huu ni wa kubahatisha
tu. Anaendelea kueleza kwa kimantiki si sawa kueleza kitu kisichoonekana au
hata kukifikia na kukipahadi jina na wakati hatuwezi kukithibitisha kisayansi
katika taaluma isimu.
Lakini pia Trubertzkoy
akinukuliwa na Massamba (2012) anasema si sahihi kuhusisha dhana ya kiisimu
yaani fonimu na saikolojia na hivyo fonimu haina budi kutazamwa kiisimu zaidi.
Fonimu kama tukio la kifonolojia:
Mtazamo huu unaongozwa na mtaalamuTrubertzkoy(1939) akinukuliwa na Mgullu
(1999) anafasili fonimu kuwa ni jumla ya sifa za sauti zenye umuhimu wa
kifonolojia, wanadai fonimu hufasiliwa kwa misingi ya ukinzani katika mfumo wa
fonolojia na kwamba hauwezi kufasili kwa kuishia katika misingi ya kisaikolojia
au uhusiano kifonetiki wa vibadala bali kwa misingi ya uamilifu wake katika
mfumo wa lugha tu. Anaendelea kusema kuwa ni lazima mtu achunguze uamilifu wa
fonimu hiyo katika mfumo mzima wa fonolojia inamotumika yaani katika kazi
mbalimbali ambazo hufanywa na fonimu fulani katika lugha maalumu.
Ubora wa kigezo hiki ni
kuwa kwanza fonimu ni kipashiocha kifonolojia hivyo haina mantiki yoyote
kuielezea fonimu bila kuihusisha na mfumo wa lugha mahususi. Vilevile hadhi ya fonimu
fulani katika lugha moja si sawa na lugha nyingine. Mathalani katika Kiswahili
/ph/ haina hadhi ya kifonimu lakini katika kimtang’ata sauti hiyo ni fonimu
halisi.
Lakini pia dhana ya
ukinzani inayoleta tofauti katika maana za maneno hutokea katika mfumo wa sauti
au lugha fulani. Hivyo ili sauti zilete athari ya maana ni lazima
zifungamanishwe katika lugha mahususi. Mfano /m/ na /n/ zikiwa pweke hazileti
maana yoyote lakini zikitumika katika maneno mfano mia na nia zinaleta maana
Udhaifu wa kigezo hiki,
baadhi ya wataalamu wanaoshadidia mtazamo huu wanachanganya mtazamo wa
kifonolojia na mtazamo wa kifonetiki. Mathalani Trubertzkoy anapoelezea suala
la ukinzani anahusisha na sifa za kifonetiki. Mfano: anapoainisha ukinzani
kimantiki angalabu ukinzani kiwili ambapo anasema ni ukinzani ambao memba
wawili wa ukinzani wanakuwa na sifa zinazopatikana kwa memba hao tu. Mfano:
/b/, /p/ sifa hizo zikiwa [+midomo,+kipasuo, -mpumuo]. Ukiangalia sifa hizo ni
za kifonetiki suala hili linazua mkanganyiko mkanganyiko kwa wanaisimu.
Kwa ujumla mitazamo
yote mitatu yaani mtazamo wa fonimu kama tukio lakifonolojia, kifonetiki na kisaikolojia
imesaidia sana kuielewa dhana ya fonimu. Hivyo hatuna budi kuichunguza mitazamo
yote kwani inakamilishana yaani fonimu inayodhihirika kifonetiki lazima iwepo
katika akili ya msemaji na itumike katika mfumo wa lugha husika ndio itofautishe
maana.
Nashukuru kwa kazi nzuri mliyofanya
ReplyDelete