Flower
Flower

Thursday, September 14, 2017

Jamii lugha na misigi yake


Ili kuweza kuifahamu zaidi dhana ya jamiilugha lazima tuchunguze misingi mikuu mitatu ifuatayo:-

(a)   Msingi wa kutumia Lugha
Katika mtazamo wa kiisimujamii, lugha ni msingi mmojawapo unaotumika kuitambulisha jamii. Katika sehemu nyingi duniani, jamii mbali mbali za watu hubainishwa kwa majina ya lugha zao. Kwa kufuata utaratibu huu tunaweza kupata majina ya lugha zao za jamii zao. Kwa mfano tuna lugha ya Kigogo (Wagogo), Kihehe (Wahehe),  Kihaya (Wahaya), Ciruuri (Waruuri), Kigweno  (Wagweno)n.k  Ieleweke kwamba si lazima pawe na uhusiano wa moja kwa moja baina ya jina la lugha na jamiilugha inayotumia lugha hiyo.  Nchi yenye jamiilugha moja, ndiyo huchukua jina la lugha hiyo.  Lakini nchi zenye jamiilugha nyingi huwa hazichukui majina ya lugha zao. Kwa mfano, hakuna lugha ya Kitanzania kutokana na jamii ya Watanzania, wala hakuna lugha ya Kikenya wala Kizambia kutokana na jamii za Wakenya na Wazambia. Hii ni kutokana na kuwa nchi zote zilizotajwa yaani Tanzania, Kenya na Zambia hazitokani na jamiilugha moja.
(b)   Msingi wa kutumia mahali
Huu ni msingi wa kisosiolojia. Wanasosiolojia  wanaona kuwa watu ndio huunda jamiilugha moja, kimsingi watu hao hukaa katika eneo moja lililo na mipaka ya kijiografia. Watu wote ambao hukaa katika eneo la jamii lugha moja huongozwa na kanuni na taratibu zilizokubaliwa na wanajamiilugha wenyewe. Kanuni na taratibu za jamii lugha hizo huzoeleka na hatimaye kuhalalishwa na wanajamii wenyewe kuwa mila na desturi za jamiilugha hizo. Jamii lugha hizi hutofautishwa na watu wa jamiilugha nyingine kwa kutumia mipaka ya kijiografia ambayo kwa kawaida huwa ni mito mikubwa, milima nakadhalika. Mipaka hii ya kijiografia huwekwa na wanajamii wenyewe na huheshimiwa na vizazi vyote kwa kurithishana mipaka hiyo baina ya jamiilugha moja na jamiilugha nyingine.


(c)    Misingi ya Makubaliano ya Kimazoea

Msingi huu unahusu jamiilugha ndogondogo ndani ya jamiilugha kubwa katika eneo husika. Jamiilugha  ndogondogo zaweza kuundwa na wafanyakazi wa kampuni, shirika, wanafunzi, wanachuo, vijana wenye mtazamo unaofanana wa kimaisha, kielimu, kibiashara n.k Kutokana na maelezo ya Gumperz (1972:219) akifafanua jamiilugha za aina hii ni kwamba kuwepo kwa jamiilugha hizi ndogondogo kunatokana na mazoea ya muda mrefu ya wanajamiilugha  hao  kuishi na kushirikiana pamoja, sifa ambayo huwawezesha kuwa na makubaliano yasiyo rasmi lakini yenye nguvu ya mazoea ya kutamka tofauti baadhi ya fonimu au maneno katika lugha ambayo ndiyo hutumika kutambulisha jamiilugha hizo kutoka jamiilugha nyingine. Kwa mfano, wafanyakazi wa bandarini toka asubuhi hadi jioni wanashinda pamoja na kujulikana kama jamiilugha ya wafanyakazi wa bandari ambao hujibainisha kwa utamkaji wa maneno uliotofauti na jamiilugha nyingine. Aidha wafanyakazi huwa wanaporudi kwenye makazi yao ya kuishi  ya majirani ambayo nayo hujibainisha kwa usemaji tofauti. Wafanyakazi hao hao wa bandari wakienda msikitini au kanisani kusali hujikuta pia wamo katika jamiilugha nyingine ya waumini n.k.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny