Flower
Flower

Tuesday, July 7, 2020

Wamitila (2003: 44), anaeleza kuwa fasihi simulizi ni dhana inayotumika kurejelea kazi ambazo kimsingi hupokezanwa kwa njia ya masimulizi au kwa mdomo. Anaendelea kueleza kuwa fasihi hii hutumiwa katika jamii kwa njia ya kupashana maarifa inayohusu utamaduni fulani, historia ya jamii, matamanio yao, mtazamo wao na historia yao.

Aidha, Njogu (2006: 2) anaeleza kuwa, fasihi simulizi ina ubunifu na uhai wa kipekee wenye kutoa fursa njema ya kuibua nadharia za kijamii, kiuchumi na kisiasa, pia aina hii ya fasihi ni uti wa mgongo wa maendeleo ya binadamu. Kwani ndani yake kuna masimulizi, maigizo, tathmini za mazingira na mahusiano ya kijamii. Kwa ujumla fasihi simulizi ni sanaa inayotumia lugha ya mazungumzo ya ana kwa ana kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa hadhira husika.

Lyimo (2014), anaeleza kuwa fasihi ya watoto ni fasihi iliyotungwa ama na watu wazima au watoto wenyewe yenye kutumia lugha na hukusudiwa kusomwa au kutendwa na watoto. Ingawa kwa ujumla fasihi hii ya watoto haitofautiani sana na ile ya watu wazima kwa dhana ya kutumia sanaa ya lugha. Fasihi ya watoto ni mpya kwa kiasi fulani katika masikio ya wanafasihi hasa wakongwe, fasihi hii si mpya kwa maana ya watoto kutohusishwa katika fasihi kwa ujumla bali ni kutokana na kutotazamwa kwa kundi hili kwa upekee wake katika utunzi na uchambuzi wa kazi za fasihi.

Bakize (2013: 61- 70), wanaendelea kueleza kuwa fasihi ya watoto inafahamika katika jamii nyingi za Tanzania, Kenya, na maeneo mengi ya Afrika kwa kiasi kikubwa ni ile iliyo katika baadhi ya vitabu vya hadithi (ngano) na nyimbo za kitoto za makabila mbalimbali. Katika maeneo mengi kazi za watoto kama ushairi, riwaya na tamthiliya bado hazijafahamika vyema.

Fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zote zimepiga hatua kubwa kimaendeleo. Hii ni kutokana na kuwa fasihi simulizi kwa sasa na fasihi andishi ya watoto zinaonekana kupiga hatua katika vipengele mbalimbali. Kutokana na ukweli huu ni wazi kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua kimaendeleo kwa hoja zifuatazo;

Kuongezeka kwa uandishi wa kazi za fasihi ya watoto, kwa mujibu wa Mulokozi katika Semzaba (2008: 4), anasema kuwa kufikia mwaka 2008 mradi wa vitabu vya watoto ulikuwa umechapisha zaidi ya vitabu mbalimbali 250 na kuvipeleka mashuleni. CODE (2015), wanasema kuwa kufikia mwaka 2015 mradi wa vitabu vya watoto ulikuwa umechapisha na kupeleka mashuleni vitabu vya Kiswahili na Kiingereza zaidi ya 350. Baadhi ya vitabu hivyo ni pamoja na Vipaji vya Helena, Zindera, Sababu Mimi ni Mwanamke, Sara na Kaka Zake na vingine vingi vilivyo chini ya mradi wa vitabu vya watoto.  Ingawa uandishi wa vitabu wa fasihi ya watoto umekuwa lakini hatuna budi kukiri kuwa uandishi huo sio linganifu kwani machapisho mengi yanaonekana kuendelea katika riwaya fupi na hadithi andishi. Aidha, fasihi simulizi inaonekana kupiga hatua kimaendeleo ambapo baadhi ya kazi za fasihi simulizi zimewekwa kwenye maadishi na kusimuliwa kwa hadhira lengwa ambayo ni watoto. Mfano, katika kitabu cha Sababu Mimi ni Mwanamke mhusika mimi anasimulia visa mbalimbali tangu mwanzo wa kitabu hadi mwisho wa kitabu, kutokana na ukweli huu basi tunaweza kusema kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zote zimepiga hatua kubwa.

Kuongezeka kwa uchapishaji wa kazi ya fasihi ya watoto, kwa mujibu wa Ngugi (2009), anaeleza kuwa kutokana na kutambua kuwa watoto pia ni sehemu ya jamii pana inayohitaji kuhudumiwa kifasihi, kila shirika la uchapishaji ilitenga idara maalumu ya kushughulikia fasihi ya watoto na vijana. Mfano, katika shirika la Oxford University Press tunapata mradi wa kusoma, Phoenix ina Hadithi za Kwetu, Longhorn ina Hadithi Kolea na Sasa Sema, East African Publishing House ina msururu wa vitabu kwa viwango mbalimbali, Paukwa (umri wa miaka 0-7), Vitabu vya Nyota (umri wa miaka 7-9), na Vitabu vya Sayari (umri wa miaka 10-13). Aidha, katika fasihi simulizi kuna visasili, visakale na hadithi mbalimbali kama vile, hadithi za Abunwasi, kisakale cha Rwanda Magele, Alfu lela Ulela. Kutokana na mifano hii, ni wazi kuwa fasihi andishi ya watoto na fsihi simulizi zimepiga hatua hasa kwa kuongezeka kwa mashirika ya uchapishaji wa kazi za fasihi ya watoto.

Hali ya usomaji wa fasihi ya watoto, kwa mujibu wa CODE (keshatajwa), wanasema kuwa usomaji wa vitabu hasa nchini Tanzania bado upo chini. Kwa kiasi kikubwa watoto wanaosoma kazi hizi za fasihi ni wale walio katika shule zilizo ndani ya mradi wa vitabu vya watoto Tanzania, shule hizo ni zile zilizo katika wilaya kumi za mradi kama vile Kongwa mkoani Dodoma, Morogoro, Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro, Kibaha, Kisarawe, Bagamoyo, Rufiji mkoani Pwani na Dar es Salaam.

Watoto wengine walio nje ya mradi pengine husoma tu vitabu vichache vya hadithi wanavyo bahatika kupata katika maktaba au sokoni. Tunaona nchini kenya hali hii ya usomaji imeongezeka kwa mujibu wa Ngugi (2009), walimu walionekana kuwa na mielekeo chanya kwa vitabu vya ziada kwani walitumia mikakati mbalimbali kwa njia ya kuwahimiza watoto kusoma. Baadhi ya mikakati hiyo ni kuwapa watoto mazoezi kusoma, kuwa na majadiliano darasani kuhusu hadithi iliyosomwa na kuwa na usomaji wa pamoja darasani. Vilevile, hali ya usimuliaji wa kifasihi simulizi umeongezeka, mfano, kuna vipindi mbalimbali vinavyoonyeshwa kwenye runinga kuhusu watoto kama vile kipindi cha Watoto Bomba kinachoonehwa ITV na vipindi vingine vinavyohusu watoto, masimulizi yanayosimuliwa na mababu zetu kuhusu visa mbalimbali na hadithi hizi mara nyingi husimuliwa wakati wa jioni ambapo hadhira inakuwa imetulia. Kwahiyo, kutokana na kuongezeka kwa usomaji wa kazi za fasihi andishi ya watoto kama tulivyoona nchini Kenya ni wazi kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua kimaendeleo.

Ufundishaji wa fasihi andishi ya watoto, Wamitila (2008:338) anasema kuwa kozi ya fasihi ya watoto ilianza kufundishwa rasmi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam katika Idara ya Fasihi, Mawasiliano na Uchapishaji mwaka 2012 katika semista ya kwanza. Hii ndio inatufanya tuitazame fasihi ya watoto kwa upekee wake, mfano kwa upande wa Tanzania mpaka sasa fasihi ya watoto kama taaluma inafundishwa katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Mtakatifu Agustino (tawi la Mtwara), Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Dodoma na Chuo Kikuu cha Elimu cha Moshi. Aidha nchini Kenya vipo vyuo vikuu ambavyo vinafunza fasihi ya watoto kwa kiwango cha shahada ya kwanza na uzamili vyuo hivyo ni pamoja na Chuo cha Kenyatta, Bewa la Marst la Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki na Chuo cha Mount Kenya. Aidha, katika upande wa fasihi simulizi hali ya ufundishaji wa fasihi simulizi imepiga hatua kubwa kwani fasihi simulizi hufundishwa shuleni ngazi ya sekondari na vyuoni. Kutokana na mifano hiyo ni dhairi kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua kimaendeleo hususani katika ufundishaji.

Uenezaji wa fasihi ya watoto katika magazeti na mitandao ya kijamii, kutokana na utafiti uliofanywa na Ngugi (keshatajwa), kuhusu hali ya fasihi ya watoto hususani nchini kenya ulilenga kubainisha tabia ya usomaji wa magazeti miongoni mwa wanafunzi wa shule ya msingi, matokeo ya utafiti huu yalithibitisha kuwa watoto wanapenda kusoma aina mbalimbali ya magazeti, miongoni mwa magazeti ni pamoja na Daily Nation, Sunday Nation, Taifa Jumapili, Taifa Leo, Sunday Standard, Maneno na Sara. Gazeti la Daily Nation lilionekana kupendwa na watoto wengi wanaopata magazeti kwa sababu gazeti hili huwahudumia watoto na vijana kwa kuwa linalenga maudhui mbalimbali yanayo wavutia watoto na vijana wa viwango tofautitofauti. Aidha kwa upande wa mitandao ya kijamii Njue (2015), anasema kuwa zipo tovuti mbalimbali kwenye mitandao ambazo huwa na hadithi mbalimbali za watoto kwa lugha ya Kiswahili kama vile watoto wangu. blog sport.com, International Children`s Digital Library na Swahili Language. Pia, fasihi simulizi imeenea sana katika mitandao ya kijamii na kwenye magazeti. Kwa hiyo tunaona kuwa watoto wanaweza kujisomea hadithi na hata kusikiliza vitabu vinaposomwa katika mitandao, hii ni hatua kubwa kimaendeleo.

Kuongezeka kwa tafiti kuhusu fasihi andishi ya watoto, kwa mujibu wa Mulokozi (2012: 51-66), anasema kuwa mpaka sasa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuna tasnifu mbili za umahili zote za mwaka 2016 na tasnifu moja ya uzamivu ya mwaka 2014, hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni kuna tafiti zimefanywa katika fasihi ya watoto na nyingine zinaendelea kufanywa katika vyuo mbalimbali vinavyofundisha fasihi ya watoto, mfano wa tafiti hizo ni zile zilizofanywa na Njue (2015), Ngugi (2009) na Omuya (2017), tafiti hizi zinashughulikia mada mbalimbali kuhusiana na fasihi ya watoto. Lakini pia, kuna tafiti nyingi zilizofanywa kuhusu fasihi simulizi kama vile, Ruth Finegan, Rose Mwangi na Taban lo Liyong hawa walifanya tafiti mbalimbali kuhusu fasihi simulizi. Hii ni ishara kuwa fasihi andishi ya watoto na fasihi simulizi zimepiga hatua za kimaendeleo.
Kwa Ujumla, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia fasihi ya watoto na fasihi simulizi zinakwenda sambamba kimaendeleo. Hii ni kutokana na athari chanya za sayansi na teknolojia katika fasihi simulizi na fasihi andishi y watoto.








                                                 MAREJELEO
Bakize, L. H (2013) Changamoto Zinazoikabili Fasihi ya Watoto Tanzania katika Kiswahili,
                        Juzuu. 76 Dar es Salaam: Taasisi ya Taaluma za Kiswahili. Kur. 61-70.
CODE. (2015) Reading Code: Assessing a Comprehensive Readership Initiative in Tanzania.
                     Kutoka www. academia. edu/… /Reading Code.
Lymo, E. B (2014) Usaguzi wa Kijinsia katika Vitabu vya Kiswahili vya Fasihi ya Watoto na
                    Mtazamo wa Wadau nchini Tanzania: Tasnifu ya Uzamivu ya Chuo Kikuu cha Dar  
                     es Salaam (Haijachapishwa).
Omuya, R.  A (2017) Tathmini ya Usimilishwaji wa Biblia kama Fasihi ya Watoto Tanzania:
                     Tasnifu ya Umahiri ya Chuo Kikuu cha Kenyattta. (Haijachapishwa).
Mulokozi, M. M (2012) Makuadi wa Soko Huria (Chachange S. Chachange) katika Muktadha wa
                      Riwaya ya Kihistoria katika Fasihi ya Kiswahili: TATAKI: Kur. 51- 66.
Ngugi, P. M. (2009) Language and Literacy Education: The state of Children`s Literature in
                 Kiswahili in Primary School in Kenya. Tasnifu ya Uzamivu Chuo Kikuu cha Vienna
                 (Haijachapishwa).
Njue, G. J. (2015) Tathmini ya Hadithi za Watoto katika Mtandao. Tsnifu ya Umahiri ya Chuo
               Kikuu cha Kenyatta (Haijachapishwa).
Semzaba, E. (2008) Marimba ya Majaliwa: Dar es Salaam: E& D Vision Publishing Ltd.
Wamitila, K. W. (2003) Kazi ya Fasihi (1): Misingi ya Uchanganuzi wa Fasihi. Nairobi
                 Vide~Muwa Publishers Ltd.









Nadharia ni dhana iliyofafanuliwa na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo Wafula na Njogu (2007.7) nadharia ni jumla ya maelekezo yanamsaidia msomaji au mhakiki kuifahamu kazi ya fasihi kwa kufuata utaratibu maalumu.

TUKI (2004:300) nadharia mawazo, maelezo au muongozo uliopangwa ili kusaidia kueleza kutatua au kutekeleza jambo fulani. Tunakubaliana na fasihi iliyotolewa na Wafula na Njogu, kutokana na kwamba fasihi hii imetaja vitu muhimu kama vile maelekezo ambayo ndiyo yanayomuongoza msomaji au mhakiki ili asivuke mipaka ya mawazo ya hiyo nadharia aitumiayo ili kufanikisha kazi kwa ufasaha. Tumejadili nadharia ya uchanganuzi nafsi kama ifuatavyo;

Nadharia ya uchanganuzi nafsi imeasisiwa na Sigmund Freud, Carl Gustav na Jacques Lacan. Sigmund Freud (1856-1939) kuna utambuzi wa kawaida na utambuzi bwete. Utambuzi wa kawaida ni sehemu ya ubongo ambayo kimsingi hupanua na kudadavua yanayoendelea hususani mchana. Utambuzi bwete hufanya kazi wakati binadamu anapolemazwa na usingizi. Baadhi ya mambo anayoshuhudia binadamu mchana yanaingia kwenye utambuzi bwete wake na kutokea katika ndoto zake usiku. Mambo yanayopatikana katika utambuzi bwete yana sifa hasi, Sigmund Freud anasema kuwa, binadamu huyaficha na kuyabania kwenye utambuzi bwetemambo ambayo hawezi kuyasema hadharani. Matamainio yasiyokubalika, makatazo yajamii, fikra na kauli zilizoharamishwa na miiko ya kijamii hubanwa katika utambuzi bwete. Fikra hizo ndizo zinazochipuka kwa njia ya ishara za ndoto, mitelezo ya kauli yaani maneno au kauli zinazotutoka bila wenyewe kukusudia. Pia huhusisha masuala ya saikolojia, matukio yaliyomtokea mtu yanayomwathiri. Mgonjwa hupaswa kusimulia kila kitu kama vile ndoto, hadithi na visasili na matokeo mengine. Lakini Carl Gustav Jung alikataa kuwa binadamu huzaliwa na matamanio ya kingono. Aliona mtoto anazaliwa katika hali ya unyoofu na usafi. mfano katika hadithi ya mtoto shujaa tunaona ushujaa unaonesha unyoofu na ukweli wa watoto.

Tumejadili nadharia ya Umarx kama ifuatavyo; maana ya Umarx, Wamitila (2006:132) anasema, Umarx ni falsafa ya yakinifu hasa kwa kuwa pana msisitizo mkubwa kwenye msingi wa hali ya kiyakinifu ya maisha kama mazingira ya kuishi kuliko mawazo katika maisha ya binadamu likimaanisha kwamba mawazo yake hayategemei kwenye dhana dhahania kama vile urembo, ukweli au ndoto bali yanajiegemeza kwenye uhalisia unaooneka.

Nadharia ya Umarx iliainishwa na Karl Marx mwaka 1818-1863 na Fredrick Engles (1820-1895) katika nadharia hii Marx amejikita katika historia ya jamii kwa kupitia hoja zifuatazo. Historia ya maisha ya binadamu inaweza kuelezwa katika misingi yakinifu, kiuchumi ambayo itachukuwa njia za uzalishaji mali pamoja na miundo ya kiuchumi, kuondoa matabaka katika jamii. Mfano Urusi, Ulaya, Amerika Kusini umiliki njia kuu za uzalishaji mali uwe chini ya umma. Maendeleo ya kijamii yanasukumwa na ukinzani yakinifu. Urazini wa binadamu umeundwa na itakadi, urazini umeunda namna ya kufikiri tabaka tawala linaunda kila kitu kama dini, maadili, siasa na sheria za jamii.

Hivyo basi mawazo ya uchanganuzi nafsi na Umarx yanauhusiano kama ifuatavyo;
Nadharia ya Uchanganuzi nafsi na Umarx zinahusiana katika ndoto, nadharia hizi humuhusisha binadamu pale anapopiyia mambo mbalimbali, changamoto au matatizo hivyo huwa na wazo la kuyabadilisha mazingira yake na huja kama ndoto ya kuwa anatenda. Mfano, katika katika kitabu cha Roza Mistika kilichoandikwa na Kezilahab, nadharia ya Uchanganuzi nafsi imejitokeza kumuonyesha Rosa alipokuwa safarini kuelekea masomoni aliyaota yale mambo ambayo mama yake alikuwa akimuonya juu ya maadili. Pia katika nadharia ya Umarx tunaona tabaka la chini lina ndoto ya kutokea kwa mabadiliko ya uongozi mbaya wenye uozo, mfano katika kitabu cha Usiku Utakapokwisha mwandishi Msokile anamuonyesha Gonza akiwa na ndoto ya kuondokana na umaskini na kwenda kuishi Zambia ambapo aliamini maisha yatakuwa rahisi na ataweza kupata kazi (uk. 48). Hivyo, tunaona nadharia hizi humuonyesha binadamu kama mwenye ndoto ya kufikia kitu fulani au kupata kitu fulani.

Uhusiano mwingine upo katika matamanio, watu hutamani kufanya vitu mbalimbali ila kutokana na miiko ya jamii, mila na desturi au uongozi hushindwa kufikia haja zao au matamanio. Nadharia ya Umarx kupitia kitabu cha Vuta N`kuvute mwandishi Shafi Adam tunamuona Ysmini alikuwa na matamanio ya kuolewa na kijana wa rika lake na sio mzee kutokana na kwamba hakuwa na matamanio ya fedha (uk. 3). Aidha, katika nadharia ya Umarx tunaona jamii ina matamanio ya kuondokana na matabaka, rushwa, ubaguzi wa rangi, uongozi mbaya, ukoloni mamboleo. Mfano, tunamuona Denge katika Vuta N`kuvute anasema;
                   Pale inapoyumkinika kutumia mbinu za dhahiri basi tuzitumie kadri ya
                   uwezo wetu. Pale ambapo hapana budi kutumia njia ya siri kwani
                   mapambano yetu ni vuta N`kuvute wao wanavuta  kule sisi tunavuta   huku (uk. 113). 
Hivyo, tunaona matamanio ya kuondokana na umaskini na hali ngumu ya maisha.
Pia, uhusiano mwingine upo katika historia ya binadamu, binadamu na maisha yake yanayomzunguka huwa na tabia ya kubadilika kutokana na mazingira yake. Mienendo fulani huanzia zamani mtoto anapokuwa, malezi na baadae kujitokeza akiwa mkubwa. Katika nadharia ya Uchanganuzi nafsi katika riwaya ya Roza Mistika tunamuona Roza katika hatua ya ukuaji wake alikosa malezi mazuri kutoka kwa baba yake Zakaria. Hivyo, kupelekea kufanya mambo aliyoshindwa kuyafanya akiwa anakuwa kutokana na ukosefu wa elimu ya malezi. Mwandishi anasema;
                         Hivyo ndivyo alivyolelewa, hivi ndivyo alivyotunzwa, hivi ndivyo
                         alivyochungwa na baba yake, tangu siku hiyo alikoma kutembea na mvulana
                        yeyote hakufahamu kwamba Roza alikuwa katika rika baya na kwamba ukali
                       ulikuwa haufai (uk. 9).
Hivyo, tunaona Roza alipoenda masomoni alianza uhusiano wa kimapenzi na wanaume mbalimbali ambapo ilimpelekea kuachwa na mpenzi wake Charles. Katika Umarx tunaona historia ya jamii ipo katika utabaka, uongozi mbaya na rushwa. Mfano, katika tamthiliya ya Kivuli Kinaishi mwandishi Mohamed anasema;
                      Sote tunaishi, sote tuliangamia sura zetu zimo ndani ya viwliwili ndani ya
                     watoto wetu, mawazo yetu (uk. 118).
Hivyo, tunaoana mabadiliko huanzia na kuwepo kwa historia fulani katika jamii ambayo haikubaliki na wengi.

Pia nadharia ya Uchanganuzi nafsi na Umarx zinafanana kama ifuatavyo;
Zote zinazeleza matamanio ya binadamu, katika Uchanganuzi nafsi tunaona mtoto huzaliwa na matamanio ya kingono, na baadae kujidhihurisha anapokuwa mkubwa. Mfano katika riwaya ya Roza Mistika tunamuona Roza akiwa na matamanio pale aliopokuwa akitumiwa barua na pesa na mchumba wake Charles alikuwa akinunua nguo za nusu uchi na kuvaa, hivyo kupelekea ndugu zake kumgombeza. Katika nadharia ya Umarx kuwepo kwa matabaka, rushwa na uongozi mbaya hupelekea jamii kihitaji mabadiliko kutokana na mapenzi ya dhati kwa nchi yao. Mfano katika kitabu cha Usiku Utakapokwisha katika kuondokana na umaskini Gonza anasema
                 Panapo wezekana panawezeka panaposhindikana panashindikana na
                  sababu itafutwe na kutolewa hadharani ili kuondoa umaskini ni lazima
                   tutafute chanzo cha umaskini (uk. 8).
Hivyo, nadharia hizi zinafanana kwa kuonesha matamanio dhahiri na yale ya kisaikolojia yaani saikoanalisisi.

Zote zimeeleza utambuzi wa mwanadamu, katika nadharia ya Uchanganuzi nafsi tunaona binadamu hutambua kuwa jambo hili kulifanya kutokana na misingi ya jamii yake na katika Umarx jamii inautambuzi wa mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia kuleta mabadiliko. Mamba hayo ni kama vile uongozi bora, jamii yenye haki na usawa. Kwa mfano katika kitabu cha Vuta N’ Vute tunamuona Yasmini ana utambuzi kuwa hawezi kuolewa na mtu aliyemzidi umri na asiyempenda kwa ajili ya mali, hivyo aliamua kutoroka (uk. 3).  Pia katika kitabu cha Kivuli Kinaishi.  Mwandishi anasema;
                    Sote tunaishi sote tuliangamia sura zetu zimo ndani ya viwiliwili
                     ndani ya watoto wetu mawazo yetu yamo ndani ya bongo zao.
                     Imani na itikadi imo ndani ya maisha yao (uk. 118).

Aidha, zote huwa katika uhakiki wa nadharia za kazi za fasihi, nadharia ya Uchanganuzi nafsi na nadharia ya Umarx zote huelezea mambo yanayosawidi jamii. Hivyo, mhakiki hutumia nadharia hizi mbili katika kubaini kazi ya kifasihi mfano, katika riwaya ya Roza Mistika mwandishi ameonesha masuala ya unyanyasaji kwa kumtumia Regina anavyonyanyaswa na mumewe. Mwandishi anasema; Lakini Regina tangu aolewe hakuwa na raha (uk. 3). Hivyo, huonesha unyanyasaji wa wanawake katika jamii. Mawazo haya hujadiliwa katika nadharia ya Uchanganuzi nafsi. Pia, katika riwaya ya Vuta N`kuvute tunamuona mhusika Denge kama mwanaharakati ambaye anapinga vikali rushwa, matabaka na ubaguzi wa rangi. Mawazo haya hujadiliwa katika nadharia ya Umarx ambapo uozo katika tabaka tawala huondolewa kutokana na msuguano wa kiyakinifu.
             

Kutokana na nadharia hizi mbili tunaweza kubaini tofauti zifuatazo;
Nadharia ya Uchanganuzi nafsi imejikita zaidi juu ya masuala ya kisaikolojia, tunaona kuwa binadamu hupenda vitu vingi lakini haonyeshi hisia zote kulingana na mila na desturi. Mfano, katika riwaya ya Roza Mistika mwandishi anasema;
                    Roza alihitaji kuwafahamu wanaume kwahiyo kutokana na malezi ya namna,
                    Roza alianza kuwatazama wanaume kama watu asiopaswa kundamana nao
                    na hata kuzungumza nao (uk. 9).
Hivyo, tunamuona Roza aliathirika kisaikolojia. Umarx unajikita zaidi juu ya uhalisia msuguano wa kiyakinifu si wa kimawazo mfano kuondoa matabaka, uongozi mbaya, rushwa katika jamii. Mfano katika riwaya ya Vuta N`kuvute mwandishi anasema;
                        Wakati tunapambana na adui lazima tutumie mbinu zote tunazoweza kutumia
                        mbinu za dhahiri basi tuzitumie kadri ya uwezo wetu……. Pale ambapo
                        hapana budi ila kutumia njia ya siri basi itumike (uk. 113)
                        
Tofauti nyingine inajitokeza katika waasisi, nadharia ya Uchanganuzi nafsi imeasisiwa na Sigmund Freud, (1859-1939), Carl Gustav John pamoja na Jacques Lacan. Huku nadharia ya Umarx imeasisiwa na Karl Marx, (1818-1863) na Fredrick Engels, (1820-1895) walifahamiana kupitia Makala.
Katika Umarx nadharia hii imejikita zaidi katika falsafa yakinifu na kuangalia mawazo ambayo sio dhahania bali katika uhalisia unaoonekana katika maendeleo ya jamii. Mfano, katika riwaya ya Usiku Utakapokwisha mwandishi amejadili matatizo yanayoikumba jamii na matokeo yake, mwandishi anasema;
                 Kifo kilichotokea kati ya mama na watoto wake wawili hiko Buguruni
          kinasikitisha. Ukweli ni kwamba haya ni madhara ya ufukara na umaskini watu
         hawakuwa na kazi kwa muda mrefu na maisha yao yamekuwa yakitegemea mno chakula
       kilichotokana na kuuzwa kwa vyombo vyao vya ndani………..(uk.7)
 Lakini nadharia ya Uchanganuzi nafsi imejikita katika dhana dhahania na ufahamu. Mfano, katika Vuta N` kuvute tunaona Yasmini anashindwa kukataa kuolewa na Bwana Raza kutokana na mapenzi ya wazazi wake. Hivyo, alikuwa na matamanio ya kutoroka (uk. 3).
Hitimisho; nadharia hizi mbili zimechangia vilivo kuhusisha fikra, mawazo, ndoto na matamanio ya banadamu. Utanzi Fulani wa jamii unazaliwa kutokana na mfumio wajamii kisiasa, kiuchumi, itikadi pamoja historia ya miundo ya jamii. Hivyo mabadiliko yanajitokeza katika jamii kutokana na ukinzani yakinifu na matamanio ya mwanajamii kuwepo kwa haki na usawa katika kuongoza jamii nzima.



                                           MAREJELEO
Kezilahabi, E (2011). Roza Mistika. Nairobi: Kenya Literature Bureau.
Mohamed, S (1990). Kivuli Kinaishi. Oxford University Press.
Msokile, M (1990). Usiku Utakapokwisha; popular publications Ltd: Maisha na Muungano wake.
Shafi, A. (1999). Vuta N` Kuvute; mkuki na nyota publishers.
Wagula, R., Njogu, K (2013). Nadharia za Uhakiki wa Fasihi; Nairobi: Print point limited.
Wamitila, K. (2012). Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi; Nairobi English Press










Katika kujibu swali hili tumeligawa katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo istilahi zilizojitokeza katika swali zitafasiliwa kwa mujibu wa wataalamu mbalimbali, sehemu ya pili ni kiini cha swali na sehemu ya tatu ni hitimisho la swali.
Mgullu (1999) akimnukuu Hartiman na Mathew (1972), Richard (1985) na Mathew (1978) wanaeleza kuwa mofolojia ni taaluma ya isimu ambayo huchunguza maumbo ya maneno na hususa ni maumbo ya mofimu.
Massamba (2009) anaeleza kuwa mofolojia ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchambuzi na uchanganuzi wa kanuni na mifumi inayohusu upangaji wa mofimu mbalimbali ili kuunda maneno katika lugha.
Besha (2007) anafasili dhana ya mofolojia kuwa ni taaluma inayojishughulisha nakuchambua maumbo ya maneno katika lugha.
Habwe na Karanja (2012) wanaeleza kuwa dhana ya mofolojia ni tafsiri ya neno la kiingereza “Mophology”. Neno hilo limetokana na neno la Kiyunani “Morphe” lenye maana ya maumbo au umbo. Hivyo walifasili dhana ya mofolojia kuwa ni neno linalotumiwa kumaanisha utanzu wa isimu unaoshughulikia maumbo kwa ujumla.
Kwa ujumla dhana ya mofolojia ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo mbalimbali ya maneno katika lugha na kipashio chake cha msingi ni mofu, ambapo mofu ni kiapshio cha kimofolojia kinachowakilisha mofimu.
Mgullu (2010) amefasili dhana ya uainishaji wa lugha kuwa ni taaluma ya isimu inayojishughulisha na uainishaji wa lugha kwa misingi mbalimbali. Pia alibainisha misingi mitatu ya uainishaji wa lugha, ambayo ni msingi wa kimuundo/ sintaksia unaochunguza mpangilio wa vipashio katika sentensi. Mfano katika lugha ya Kiswahili sentensi huanza na kiima, kiarifu na yambwa (K+A+Y), msingi wa kiuamilifu ambao hubainisha lugha kwa kuchunguza matumizi au kazi ya lugha fulani katika jamii. Ambapo kwa kutumia msingi huu tunapata lugha rasmi na lugha kienzo (isiyo rasmi) na msingi wa tatu ni msingi wa kimaumbo/ kimofolojia ambao hubainisha lugha kwa kuchunguza mapangilio wa mofu katika maneno ya lugha fulani. Kulingana na swali hili tutajikita katika msingi wa uainishaji lugha kimaumbo/ kimofolojia, ambao huchunguza mpangilio wa mofu katika maneno. Aidha Mgullu (keshatajwa) anasema kuwa uainishaji wa lugha kwa kutumia msingi wa kimofolojia, umeainisha lugha kwa kuzingatia maumbo ya lugha mbalimbali za jamii na uainishaji huu unatupatia aina tano za lugha ambazo ni lugha tenganishi, lugha ambishi, lugha ambishi mchanganyiko, lugha ambishi bainishi na lugha muundo ghubi.
Mathew (1991) anaeleza kuwa lugha tenganishi ni ile ambayo maumbo ya maneno yake huonekana kama mofu moja moja tu. Anaendelea kueleza kuwa mfano wa lugha hizo ni Kituruki, Kichina na Kiingereza. Mathalani katika lugha ya Kiingereza maneno kama “with, what na Rice” ni mfano wa lugha tenganishi kwa sababu maneno hayo hayawezi kuongezwa viambishi vya aina yoyote. Pia Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha tenganishi ni aina ya lugha ambazo maumbo yake hayaambishwi, hayanyambuliwi, hayabadiliki na hayana viambishi vyovyote. Hii inamaanisha kuwa maana za tungo hudhihirika na kutofautishwa kwa kutumia mpangilio wa maneno ambapo maneno katika lugha za jamii huwa na mofu moja tu ambayo huwakilisha mofimu moja. Kutokana na maana hii tunaona kuwa mfano wa lugha ya Kiingereza uliyotolewa na Mathew (keshatajwa) una udhaifu kwa sababu kuna baadhi maneno ya Kiingereza ambayo huweza kunyambulika kwa kuongezewa viambishi mbalimbali. Mfano “do – done”. Hivyo lugha tenganishi ni lugha ambayo maneno yake huundwa kwa mofu moja huru ambayo huwa na maana kamili. Mfano wa lugha hizi ni Kichina na Kivietinamu.
Massamba (2004) anaeleza kuwa lugha ambishi ni lugha ambayo maneno yake hutumia viambishi kuwakilisha dhana mbalimbali. Naye Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha ambishi ni lugha ambazo maneno yake huambika viambishi mbalimbali ambavyo huwakilisha maana mbalimbali za kisarufi na lugha hizi hupokea viambishi katika mashina yake au katika mizizi yake. Mfano wa lugha hizi ni Kiitaliano, Kiingereza na Kiswahili. Mathalani katika lugha ya Kiingereza mofu “S” inaweza kuwekwa kwenye maneno mbalimbali na kuwa na dhima tofauti tofauti kama ifuatavyo;-
Play                           palys (njeo)
           Sara                           Sara’s (umilikishi)
Eye                            eyes (wingi)
Katika mifano hii mofu “S” imedokeza dhima mbalimbali. Vilevile lugha ya Kiswahili huruhusu uambikwaji wa viambishi mbalimbali katika maneno ambavyo hudokeza dhima mbalimbali. Mfano mashina kama vile “piga, cheza na soma” ikiongezewa viambishi inaweza kuwa kama ifuatavyo;-
Piga       -     pigia, pigisha, alipigwa, pigana na pigishwa
Cheza    -     chezea, chezesha, alichezwa, chezeana na chezeshwa
Soma     -     somea, somesha, alisomeshwa, someshana na someka
Kutokana na mifano hiyo inaonesha kuwa baada ya kuambika viambishi kwenye mashina yamedokeza dhima ya kauli mbalimbali ikiwemo kauli ya kutenda, kutendwa, kutendeka, ktendea, kutendeana na kutendewa.
Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha ambishi mchanganyiko ni lugha ambazo huambikwa mofu mbalimbali katika mizizi ama mashina kisha mofu hizo huchanganyika na mizizi kiasi ambacho ni vigumu kutenganisha Dhahiri kuwa mofu ni zipi na mizizi ni ipi, kwani mofu na mizizi huungana na kuwa kitu kimoja. Kuunganika kwa mofu na mizizi huweza kubainishwa na michakato ya kimofofonolojia, ambapo Rubanza (1996) anaeleza kuwa mofofonolojia ni kanuni ambazo huelezea mazingira ambapo mofu hutokea. Mathalani kanuni hizo ni udondoshaji, uyeyushaji, ukakaishaji na usilimisho pamwe wa nazali. Mfano wa lugha hizi ni Kiingereza na Kilatini. Katika lugha ya Kiingereza, maneno yenye umoja na wingi huweza kubadilika lakini nivigumu kutenga mofu na mizizi husika. Mifano ifuatayo inadhihirisha dai hili;-
Umoja                                 Wingi
                                                   Man                                     Men
   Woman                                 Women
                                                    Foot                                      Feet
  Mice                                    Mouse
Hivyo katika mifano hiyo, licha ya maneno yaliyokatika umoja kubadilika katika wingi bado ni vigumu kutenga mofu na mzizi wa neno husika.
Massamba (2004) anafasili lugha ambishi bainishi ni lugha ambayo maneno yake huundwa kwa mwandamo wa mofimu katika safu moja kuandamia mzizi, ambazo zinatenganishika kwa utaratibu ulio wazi na kila moja huwa na uamilifu mmoja tu. Pia Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha ambishi bainishi ni lugha ambazo maneno yake huweza kuwekewa viambishi mbalimbali, yaani mizizi na viambishi huwa havichanganyiki kwani ni rahisi kabisa kuweza kuonesha kuwa viambishi ni vipi na mizizi ya maneno ni ipi. Mfano wa lugha hizi ni Kiswahili. Mifano ifuatayo inadhihirisha dai hili;-
Analima                           a- na- lim- a
Atapika                             a- ta- pik- a
    Alipikiwa                          a- li- pik- iw- a
Hivyo kutokana na mifano hiyo, mizizi na viambishi vya maneno vimejidhihirisha wazi.
Mgullu (2010) anaeleza kuwa lugha muundo ghubi ni lugha ambayo huundwa kwa kuweka pamoja mfululizo wa mofu au wa maneno katika lugha moja. Na maneno ya lugha hii huwa na uchangamani zaidi kwani mzizi huunganishwa ili kujenga neno moja lenye muundo changamani. Mfano wa lugha hizi ni lugha ya Kieskimo.
Licha ya mofolojia kuwa na dhima yya kuainisha lugha, pia huweza kuwa na dhima nyingine kama zilivyofafanuliwa na Mathew (1991),
Mofolojia husaidia kubainisha vipashio vinavyounda maneno na dhima zake. Mfano neno Anacheza hujibainisha na kuwa (a- na- chez- a) ambapo mofu a- kiambishi awali cha nafsi ya tatu umoja, -na- kiambishi cha wakati uliopo, -chez- ni mzizi wa neno na –a ni kiambishi tamati maana.
Mofolojia husaidia kuunda maneno mbalimbali. Mfano neno piga likiongezwa viambishi huweza kuunda maneno mengine mapya kama ifuatavyo, anapiga, atapigwa, wanapigana, pigika na pigia.
Kwa ujumla licha ya uainishaji lugha kwa kutumia msingi wa kimofolojia lakini pia kuna misingi mingine ambayo ina mchango mkubwa sana katika suala zima la uainishaji wa lugha. Misingi hiyo ni pamoja na msingi wa kiuamilifu na msingi wa kimuundo/ kisintaksia.


MAREJELEO
Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es salaam: Macmillan Aidan Ltd.
Habwe, J. na Karanja, P. (2012). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Massamba, P. B. (2004). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu (SAMIKISA). Sekondari na Vyuo.  Dar es salaam: TUKI.
……………….. (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es salaam: TUKI.
Mathew, P. H. (1991). Mophology (Second Edition). United Kingdom. Cambridge University Press.
Mgullu, R. S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Kenya Ltd.
Rubanza, Y. I. (1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar es salaam: Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.








Wataalamu mbalimbali wamefasili dhana ya sentensi kama ifuatavyo Kapinga (1983), anafasili sentensi kuwa ni kipashio kikubwa kuliko vipashio vya kiisimu na huwa na wazo kamili. Anaendelea kueleza kuwa sentensi ni sehemu ya sarufi ambayo agharabu hujisimamia kimaana, mala nyingi sentensi huweza kuwa na maana anbazo huweza kuwa ni taarifa, ombi, mashariti, au hata amri.
 
Richard et all (1985), anasema sentensi ni dhana asilia ya lugha ambayo hufafanuliwa kudhihirisha sehemu ya sarufi yenye neno moja au zaidi inayosimamia wazo kamili nae Radford (1997), anasema sentensi ni sehemu ya sarufi ambayo hujisimamia kisintaksia na ambayo huwa na kiima na kiarifu ambacho kina kitenzi kimoja au zaidi. Kwaujumla sentensi ni tungo yenye muundo wa kiima na kiarifu na vilevile husimamia wazo kuu.
 
Sentensi huweza kuainishwa kwa mkabala wa kisemantiki (mapokeo) cha maana ambapo kuna sentensi swali, sentensi maelezo, sentensi mshangao na sentensi shurtia. 

Vilevile sentensi huainishwa kwa mkabala wa kisasa (kimuundo) ambapo kuna sentensi sahili, sentensi changamano, na sentensi ambatano. Sentensi ya Kiswahili huwa na muundo anuai kama inavyo fafanuliwa hapa
 
Sentensi huwa muundo wa kiima. TUKI (2004) wanaeleza kiima kuwa ni neno au kifungu cha maneno katika sentensi ambacho hutangulia kitennzi. Hivyo muundo wa kiima katika sentensi  ni sehemu ya sentensi ambayo inatawaliwa na nomino, vilevile kinaweza kushirikisha kikundi kivumishi au kishazi tegemezi, Mfano
          Matunda matamu huvutia
                         K
          Wanafunzi waliokuwa wametoka shuleni wameathibiwa
                              K
Muundo wa kiarifu. Kiaifu TUKI (2004), wanaeleza kuwa kiarifu ni sehemu ya sentensi yenye kitenzi, shamirisho na shagizo.hivyo muundo wa kiarifu katika sentensi ni sehemu ya sentensi yenye kitenzi ambayo hushirikisha kikundi kielezi au kikundi kivumishi, vilevile kinaweza kuwa na nomino kama shamilisho.
Mfano      Mvua inarutubisha vitu vyote
                                     A
                 Dunia huzunguka jua
                                     A    nzi kinaweza kuwa
Miundo ya Shamilisho ni miundo katika sentensi ambayo mtendwa au mtendewa katika sentensi ni sehemu ya sentensi inayowakilisha kitu kilichofanyiwa kitu. Aidha kirai kitenzi kinaweza kuwa na kirai nomino kama shamilisho.
Kwaujumla sentensi za Kiswahili huwa na dhima mahususi mahusiano yake ni tofauti na lugha ya ulaya vilevile sifa za lugha ya Kiswahili na lugha ya kibantu zinafanana, sifa hizo ni kama vile sentensi huwa na upatanishi wa kisarufi ambapo kiima hudhibiti virai vingine kwa kutumia viambishi vipatanishi. Mfano Mtu mrefu amekufa

Marejereo
Kapinga, M.C (1983), Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu:Dar es Salaam TUKI   

TUKI (2004) Kamusi ya Kiswahili Sanifu: Dar es saalama, TUKI

Massamba, D.P.B, Kihore, Y.M, na Hokororo J.I (1999), Sarufi Miundo ya Kiswahili Sarufi SAMIKISA Sekondari na Vyuo:Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili . Dar es Salaam


 Malengo ya isimujamii
Isimujamii ina malengo makubwa matatu yafuatayo:-
Kuchunguza tofauti za wazungumzaji wa lugha katika jamii.
Wanaisimujamii hufanya uchunguzi na kufafanua tofauti zilizopo za watumiaji wa lugha katika jamii na kueleza tofauti hizo za wazungumzaji husababishwa na nini. Kuelewa lugha ya jamii kunaendana na kuielewa jamii yenyewe ikiwa ni pamoja na kuyaelewa matabaka na makundi mbalimbali yaliyomo ndani ya jamii hiyo. Jamii imeundwa na matabaka na makundi mbalimbali ya watu. Kuna matabaka ya watawala na watawaliwa, wakulima na wasiowakulima, wafanyakazi wa kuajiriwa na wasiowakuajiriwa, waliosoma na wasiosoma, wafanyabiashara na wasio wafanyabiashara n.k. Pia kuna makundi ya vijana, wazee, wanawake, wanaume, wanafunzi, wanachuo, wanamichezo n.k. Ukichunguza kwa makini utabaini kuwa kila tabaka au kundi la watu katika jamii hutumia lugha inayotambulisha tabaka au kundi hilo. Kuchunguza na kufafanua tofauti za wazungumzaji wa lugha katika jamii kunasaidia watumiaji wa lugha kufahamu watumie lugha ipi katika mazingira rasmi na yasiyo rasmi miongoni mwa wanajamii wenyewe. Lugha rasmi ni ile lugha iliyokubalika na kutangazwa na chombo chenye mamlaka ili lugha hiyo itumike katika shughuli za serikali, bunge, mahakama, elimu nakadhalika. Pia umuhimu mwingine wa kuchunguza tofauti za wazungumzaji wa lugha ni kusaidia wazungumzaji kufahamu namna bora ya kutumia lugha katika mawasiliano ya jamii baina ya wazungumzaji na msikilizaji.
 
Kufanya uchunguzi na kufafanua uhusiano uliopo baina ya lugha na wazungumzaji wake. 
Lengo hili pia linalenga kuifahamu jamii kwa kuchambua lugha ya wazungumzaji wanayoitumia. Kwa kuchambua lugha wanayoitumia wazungumzaji, tunaweza kuitambua jamii inayohusika kama ina dini ua imani ipi, iko maeneo gani ya nchi (pwani, bara, kusini/kaskazini n.k), watu wake wanafanya kazi gani,  wanaume au  wanawake, vijana au wazee, wasomi au wasiowasomi n.k

Kuangalia uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine
Mwanaisimujamii anapaswa kuchunguza na kutolea ufafanuzi uhusiano uliopo baina ya lugha moja na lugha nyingine zinazotumika. Katika jamii au taifa kuna lugha zaidi ya moja zinazotumiwa na watu. Nchini Tanzania, kwa mfano, kuna lugha zaidi ya 120 zinazotumiwa na watu mbalimbali. Kidhima lugha hizi zimegawanywa katika makundi matatu. Lugha ya Kiingereza, lugha ya Kiswahili na lugha za kijamii. Ni kazi ya mwanaisimu kufanya uchunguzi na ufafanuzi wa mambo ya msingi yanayohusu uhusiano wa lugha hizi na wazungumzaji wake kwa kuzingatia mahitaji ya jamii ya wakati huo.
 
Isimujamii ya mawandafinyu
Huu ni makabala wa kiisimu unaozingatia lengo la kwanza na la pili la isimujamii katika uchunguzi na uchanganuzi wake. Ni makabala unaochunguza uhusiano wa tofauti za wazungumzaji wa lugha na kubainisha vitambulisho vya usemaji au utamkaji wa wazungumzaji au wazungumzaji ili kuhusisha na kundi la aina ya watu au matabaka ndani ya jamii. Mwanaisimu Labov (1972) katika utafiti wake alioufanya katika jiji la New York, Marekani ameonyesha kuwa, watu wa tabaka la chini hutamka sauti [r] kwa mkwaruzo zaidi katika maneno yenye fonimu /r/ kuliko watu wa matabaka mengine (tabaka la juu). Trughdill (1874), katika uchunguzi alioufanya nchini Uingereza, ameonyesha kuwa mbali na kuwepo kwa lahaja la kijiografia, pia kuna lahaja za kijamii yaani zinazoonyesha hadhi mbalimbali za watumiaji wa lugha ya Kiingereza. Kwa maneno mengine Trudgill anaeleza kwamba unaweza kupata lahaja za wazungumzaji wa hadhi ya juu na lahaja za wazungumzaji wa hadhi ya chini. 
 Isimujamii ya mawandamapana
 
Huu ni mkabala unaozingatia lengo la tatu la isimujamii ambalo linachunguza na kufafanua uhusiano wa lugha moja na lugha nyingine zinazotumika katika jamii. Kwa mujibuwa mkabala huu, mambo yanayozingatiwa ni yale yote yanahohusu utumiaji wa lugha kwa jumla. Kujua lugha zilizopo katika jamii na uhusiano wake kidhima na lugha nyingine ni moja ya mambo ya msingi ya mkabala huu. Kwa mfano mwanaisimujamii katika mkabala huu, hupenda kujua sababu za msingi zinazofanya lugha moja iteuliwe kuwa lugha ya taifa, lugha rasmi au lugha ya kufundis hia katika mfumo wa elimu. Sababu zinazotumika kuteua lugha kuwa na dhima kitaifa mara nyingi huwa hazina budi zitokane na sababu za msingi za kiisimu na kijamii. Kimsingi, hata zile lugha ambazo haziteuliwi kuchukua dhima yoyote kitaifa bado kwa mujibu wa mkabala huu, ni muhimu lugha hizo kufanyiwa uchunguzi ili kuona hali halisi ilivyo, kwa lengo la kutaka kujua hatma ya lugha hizo, hasa kule zinakotumika na pia kutaka kujua maendeleo ya lugha hizo ili kuweza kutoa mapendekezo ya nini kifanyike. Uhusiano huu wa lugha mbalimbali katika jamii hutegemea sana sera ya lugha ya nchi husika. Mkabala huu huhusisha watu wengi kijiografia. Mathalani, mkabala huu unaweza kuhusisha wazungumzaji wa nchi moja, nchi zilizoungana, jumuia ya nchi kadhaa, kanda za nchi mbalimbali na hata huweza kuhusisha wazungumzaji wa bara zima. Kimsingi, mkabala huu wa mawanda mapana ni mkabala ambao kusema ukweli, uchunguzi wake unalenga kutatua matatizo mbambali yahusuyo utumiaji wa lugha kitaifa na kimataifa kwa ujumla.

AddToAny