Flower
Flower

Wednesday, September 13, 2017

JAMIILUGHA MBALIMBALI


                           JAMIILUGHA MBALIMBALI
2.1 Dhana ya jamii lugha
Wataalamu mbalimbali wa isimujamii kama vile (Hymes, 1996, Gampez, 1972, Labov, 1972, na Mekacha, 2000) wanakiri kwamba kufasili dhana ya jamiilugha siyo kazi rahisi kutokana na ugumu wa kuweka mipaka ya maeneo ya matumizi ya lugha ya watumiaji wake.
Wataalamu wa isimujamii, hasa hao waliotajwaja wanakubaliana kuwa jamiilugha ni watumiaji wa lugha wanaoishi katika eneo moja ambao hubainishwa na mahusiano yao ya kuendelea kutumia aina fulani ya lugha tofauti na watumiaji wengine wa lugha hiyohiyo.
Fasili hii ya jamiilugha inaonekana ni rahisi kueleweka, kiutendaji fasili hii huzua utata hasa katika kufanya uainishaji wa wazungumzaji na uchanganuzi wa data za isimujamii. Wanaisimujamii  wanachukulia dhana ya jamiilugha kuwa inawakilisha eneo msingi la matumizi ya lugha. Kwa maeneo mengine, jamiilugha ndio muktadha halisi wa kupatia taarifa zote muhimu za wazungumzaji wa lugha ili zifanyiwe uchunguzi kwa lengo la kuzichanganua na hatimaye kuzitolea ufafanuzi wa tofauti za matumizi na sababu zake.
Utata wa maana ya jamiilugha unatokana na fasili yenyewe kutokuwa wazi hasa katika mambo kadhaa yafuatayo:-
(a)    Utata unahusu eneo msingi la watumiaji wa lugha katika jamiilugha. Je, mipaka ya eneo hili inaanzia wapi na kuishia wapi?
(b)   Mipaka ya eneo la jamiilugha inawekwaje bila ya kuingilia mipaka ya eneo jingine la jamiilugha?
(c)    Wazungumzaji wa lugha waliomo ndani ya jamiilugha moja wanazungumza lugha ngapi? Wanatumia lahaja, lugha sanifu, misimu, lafudhi au wanatumia lugha zote?

(d)   Je, tunatumia vigezo gani kuwatambua na kuwa ainisha watumiaji wa lugha waliomo ndani ya jamiilugha moja kuwa hao ndio wanajamii wa jamiilugha hiyi? Kusema kweli, maswali haya na mengine mengi ndiyo yanayofanya fasili ya jamiilugha ionekane kuwa na utata zaidi hasa kinadharia na kiutendaji.

No comments:

Post a Comment

syliverymanyama@gmail.com

AddToAny